ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 1, 2013

MAMBO 10 YANAYOSABABISHA MWANAMKE KUSALITI - 10

TUPO kipengele cha tisa, jinsi mwanaume mwenye gubu anavyoweza kumfanya mwanamke wake asaliti.
Inapotokea mwanaume anakuwa hodari wa kuzungumza kwa ukali na makaripio, humfanya mwanamke ajione kama yupo kwenye uhusiano usio na amani. Haraka sana, huangalia uhusiano wa wanawake wengine jinsi wanavyoishi na wanaume zao.

Kitendo cha kubaini kuwa mwanaume wake ana kasoro ya kimawasiliano na mwanamke, humfaya atamani kumpata mwanaume ambaye atakuwa tofauti na mwenzi wake. Wazo hilo linapopita kwenye kichwa chake, huwa hachukui muda atakuwa amekwishasaliti.
Ni vizuri sana kuchunga tabia ambayo itakuwa inamfanya mwenzi wako akuone kero. Tambua kwamba mwenzi wako hapo alipo, kuna wanaume wengi wanatamani wangekuwa naye, kwa hiyo unaposhindwa kumfanya awe mwenye furaha, yupo atakayejitokeza kugharamia furaha yake. Utasalitiwa.
Gubu ni janga, hebu jitahidi kujidhibiti kwa sababu itakuweka kwenye mazingira rahisi ya kuchokwa na mwenzi wako. Anapokuchoka hatakuwa na kizuizi cha kukusaliti. Kwa kifupi ni kwamba mwanamke anapomchoka mwanaume, anakuwa hamhesabu kama mwenzi wake tena, isipokuwa anaweza kuendelea kuwa naye kwa sababu za kimazoea tu.
Chazo cha kuwa na gubu ni wivu uliopitiliza ambao humfanya mtu awe mwingi wa kulalamika, kugomba na kususa. Anaweza kufanyiwa jema lakini akatafsiri baya. Mwenzi wako anapokufayia kitu kizuri, hutamani kuona mapokeo yako yakiwa chanya. Unapopokea hasi, humnyong’onyesha kabisa.
Unadhani baada ya kunyong’onyea ataendelea kuwa na moyo uleule wa mapenzi? Atakutoa kasoro, baada ya hapo, atahitaji fumbato. Mwanaume wa pembeni atakayejitokeza na kumwonesha hali ya ukarimu na ushirikiano ambao aliuokosa kwako, moja kwa moja atampa mapenzi yake yote.
Chunga sana tabia ya gubu. Kuwa mwangalifu kwenye uhusiano wako. Hupendi kukaripiwa, nawe usimfanyie hivyo mwandani wako. Tenda vile unapenda kutendewa. Unapokuwa tatizo kwenye uhusiano wako, unampa kero mwenzi wako, mwisho wake ni kusaliti kabla ya kukukimbia jumla.

10. ANAPOONA MWANAUME WAKE SI MWELEWA
Kuna kitu ambacho kipo kwa kila mwanamke. Mbali na kutaka awe na mwanaume anayekidhi hitaji la moyo wake, vilevile humtamani ambaye atamfanya atembee kifua mbele kwa watu wengine. Hivyo basi, tengeneza mwonekano na tabia zako ili mwenzi wako aone fahari kuwa nawe.
Fanya makosa yote lakini inapotokea mwanamke wako anakutafsiri kuwa wewe siyo mwelewa, mara moja ataanza kukudharau. Akishakushusha thamani na msisimko wake juu yako hutoweka. Hali ikiwa hivyo, hicho ni kipindi cha hatari, kwani wakati wowote anaweza kumpokea mwanaume mwingine atakayemwona ana uelewa kuliko wewe.
Usipende kuwa mtata, jambo linapotokea onesha namna unavyoweza kuchanganua mambo. Inapotokea mwenzi wako anaujua ukweli halafu wewe unakuwa mgumu kuelewa, unamfanya akushushe thamani. Kwa kawaida, mwanamke huwa hapendi kupingwa ikiwa ukweli anaujua.
Mathalan, yupo mwanaume ambaye ni rafiki au mshirika wake wa kazi. Wewe unapingana na ukweli ambao yeye anakwambia, badala yake unamtuhumu kwamba ana uhusiano naye wa kimapenzi. Tuhuma zako zinamfanya akuone wewe siyo mwelewa, matokeo yake atakusaliti, yaani ataamua kufanya kweli.
Ikiwa unamwona mwenzi wako ana ukaribu na mwanaume, halafu unatilia wasiwasi. Jambo la kufaya ni kuhakikisha unamwelewesha mwenzi wako kuachana naye. Kukimbilia kushusha tuhuma, maana yake unapoteza pointi, sasa yeye ndiye atakuona una kasoro katika uelewa wako. Mwisho atamtamfuta mwelewa na kumpa penzi ambalo ni haki yako.
Epuka kuzungumza maneno ya kipuuzi. Kama jambo huna uelewa nalo, usichagie, maana unaweza kuboronga, sasa kwa vile yeye anajua, moja kwa moja atakushusha thamani. Siku zote tambua kwamba mapenzi ni mchezo wa kulinda hadhi na heshima yako mbele ya mwandani wako.
Mpaka hapo utakuwa umeelewa kwamba kuna nyakati ambazo wanawake wanasababishiwa kutenda usaliti, kwa hiyo usimweke majaribuni. Kuhakikisha hatoi penzi lako kwa mtu mwingine kiholea, wewe cheza vizuri katika uhusiano wako. Uhusika wako ndiyo unaoweza kuamua mwanamke wako awe mtulivu au arukeruke.

GPL

No comments: