Advertisements

Wednesday, July 31, 2013

Mambo ya kuzingatia wakati wa mfungo


Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum

Na Sheikh Alhad Salum

BISMILLAHIR Rahmanir Rahim. Hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu (SW), aliyetuneemesha neema ya Imani na Uislamu, Mungu hakumuumba mwanadamu ila kwa lengo la kumuabudu.

Waislamu duniani kote hivi sasa tuko katika utekelezaji wa nguzo ya nne kati ya nguzo tano za Uislamu ambayo ni kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Hivyo niwakumbushe waumini wote wanaoshiriki katika utekelezaji wa nguzo hii muhimu mambo ya msingi na kuzingatia ili funga zetu ziwe salama na kukubaliwa na Mwenyezi Mungu (SW).

Kimsingi tunapaswa kufahamu kuwa funga ina nguzo zake ambazo ni mbili. Kwanza ni nia, kwamba mtu anayefunga anapaswa kuwa na makusudio ya kufunga ndani ya moyo wake kuwa kesho utafunga.

Nguzo ya pili kujizuia na vitu vyenye kuharibu funga kuanzia kuchomoza hadi kuchwa kwa jua.

Hizi nguzo mbili muhimu lazima kila mtu aliyefunga azitekeleze kwa pamoja. Hiyo nguzo ya pili inaonesha wazi kwamba kufunga si kujizuia kula na kunywa tu, bali ni zaidi ya hayo.

Hivyo tunatakiwa tujizuie na maovu mbalimbali yaani kujizuia kusema uongo, kuteta watu, kuvunja sheria na kutozuia macho kutazama mambo ya haramu.

Pia tunapaswa kujizuia kula vyakula haramu katika futari zetu tunazoziandaa. Vyakula haramu ni pamoja na vile vilivyopatikana kwa njia zisizo halali yaani kumpora mtu, rushwa na kutapeli.

1 comment:

Anonymous said...

Vyakula haramu (Vyakula haramu ni pamoja na vile vilivyopatikana kwa njia zisizo halali yaani kumpora mtu, rushwa na kutapeli) - the whole ruling class in Tanzania would not be able to eat anything then!!! You know what I mean!!