Advertisements

Wednesday, July 31, 2013

"NIPO TAYARI KUPIGWA RISASI KAMA ITATHIBITIKA NINAHUSIKA NA MADAWA YA KULEVYA "....MBUNGE AZZAN

Wakati Jeshi la Polisi likitoa visingizio kwamba linashindwa kunasa watuhumiwa wanaosafirisha dawa za kulevya wanaopitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kutokana na kukosekana kwa vitendea kazi, Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan, amesema yupo tayari kupigwa risasi au kunyongwa hadharani kama itathibitika anahusika na biashara hiyo.

Azzan alitoa kauli hiyo jana wakati akihojiwa na kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One kuhusu kuwapo kwa madai ya barua iliyoandikwa na Mtanzania aliyefugwa Hong Kong nchini China akimtaja kuhusika na biashara ya dawa hizo.

Alisema hahusiki kwa namna yoyote ile na biashara ya dawa za kulevya au biashara yoyote haramu na kwamba taarifa zilizoandikwa kwenye mitandao ya kijamii ni za upotoshaji na zimetolewa kwa lengo la kumchafua.
“Nimejipeleka polisi kwa mara nyingine tena na nimewaomba wafanye uchunguzi wa kina na kama nitabainika nahusika na biashara hiyo niko tayari kupigwa risasi hadharani, lakini pia sitendewi haki kwa wale ambao wanazusha jambo hili wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema. 
Azzan aliongeza kuwa hayupo juu ya sheria hivyo ikithibitika kuna mtu anamtuma dawa za kulevya kupitia bandari fulani pia atakuwa tayari kuwekwa hadharani na kunyongwa maana atakuwa hafai kuendelea kuwapo Tanzania.
Alisema makundi yanayomwandama ni ya kisiasa kwa lengo la kutaka kumdhoofisha katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015.
Mahojiano kati ya Azzan na radio yalikuwa kama ifuatavyo;

RADIO: Mhe Idd Azzan wewe ni mbunge wa Kinondoni inaelezwa kuwa wewe ni mmoja kati ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya na mmekuwa mkipokea mizigo kupitia maboti makubwa yanayotoka Pakistan yanayopitia Bagamoyo, Tanga, Mtwara na Dar es Salaam, hebu tujuze na wajuze Watanzania hili lina ukweli gani.

AZZAN: Hata mimi nimesikia hilo na bahati nzuri nimesoma kwenye mitandao kadhaa imeandika hivyo na kuna barua inayodaiwa kuandikwa na mfungwa mmoja ambaye amedai mimi ndiye nahusika kumtuma yeye.


Napenda kuwajulisha Watanzania sihusiki kwa namna yoyote ile na biashara ya dawa za kulevya na siyo dawa za kulevya tu lakini pia biashara yoyote haramu sijawahi kufanya katika maisha yangu.

Niseme tu kuwa hizo ni taarifa ambazo zimetolewa kwenye mitandao ili kuaminisha watu hivyo, lakini kimsingi sihusiki na sijihusishi na biashara ya namna hiyo. 

Baada ya kuziona habari hizi kwenye mitandao nilichokifanya na sababu ilishawahi kujitokeza tena na viongozi wangu wa CCM walishawahi kuyasema hayo kwenye mkutano wa vijana nikawaambia polisi wachunguze ili kupata ukweli wa hilo jambo.

Kama itabainika nahusika basi nichukuliwe hatua za kisheria mimi siyo Mungu wala sipo juu ya sheria, nimefanya hivyo kwa maana ya kuongea na Jeshi la Polisi nimejipeleka nimetoa maelezo na nimewataka polisi kwa sababu ni kazi yao wafanye uchunguzi wa kina, pili kama nahusika na tuhuma hizo hatua za kisheria zifuatwe dhidi yangu na kama siyo kweli hao wanaoeneza uzushi huo pia wachukuliwe hatua.

RADIO: Unadhani kwa nini Mtanzania aliyeshikiliwa Hong Kong amekutaja wewe kuhusika na biashara hiyo?

AZZAN: Kwanza mimi siamini kwamba kuna Mtanzania anayeshikiliwa Hong Kong ambaye amenitaja mimi, sababu hiyo biashara kwanza sijawahi kuifanya, mimi niliiona hiyo barua haina jina la huyo Mtanzania mnayemsema, wala hakuna namba ya mfugwa sasa mfungwa anatakiwa kuwa na namba, asitaje jina ataje basi walau namba yake pia hakuna jina la gereza, kwa hiyo mimi siamini Mtanzania ambaye amefugwa kwa tuhuma za dawa za kulevya anitaje mimi kuwa nimemtuma. Hakuna hicho kitu na hakuna Mtanzania ambaye niliwahi kumtuma hicho kitu kimetengenezwa kwa nia ya kunichafua.

RADIO: Mheshimiwa unatafsiri vipi tukio hili?

AZZAN: Mimi ninachotafsiri tayari mapambano ya 2015 ndiyo yanaanza na watu wanatafuta jinsi ya kunichafua sababu hata tukienda kwenye kura nitawashinda, lakini si kutafuta mbinu chafu za kunichafua.

Yapo maneno ambayo nayazungumza bungeni hayawafurahishi wengine, lakini kwa Watanzania wengi yana manufaa, kwa hiyo kwa wale ambao hayawafurahishi wanaweza wakawa wamechangia katika kunichafua.

RADIO: Lakini Mheshimiwa Idd Azzan mara nyingi tu umekuwa ukitajwa na watu mbalimbali kwamba unajihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya ama wewe ni mmoja kati ya watu wanaowaagiza watu mbalimbali kusafirisha mizigo hiyo ya dawa za kulevya hilo kwa upande wako unalizungumza vipi.

AZZAN: Nasema binafsi nimejipeleka polisi na nilishajipeleka mara ya kwanza baada ya kutokea tuhuma kama hizi, nikawaambia polisi wafanye uchunguzi kama nahusika nichukuliwe hatua za kisheria, nimekwenda tena kuwaambia polisi na nasisitiza polisi wafanye uchunguzi wa kina kama nahusika hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yangu.

Kama nitabainika nahusika na biashara hiyo niko tayari kupigwa risasi hadharani, lakini pia sitendewi haki kwa wale ambao wanazusha jambo hili wachukuliwe hatua za kisheria.

RADIO: Lakini Mheshimiwa kwa upande mwingine tayari taarifa zimeshatolewa kama hivyo kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, sasa endapo itabainika kweli umehusika ama hujahusika ni kitu gani ambacho utakifanya.

AZZAN: Naomba niweke wazi kama itathibitika ninamtuma mtu madawa ya kulevya kupitia bandari gani mimi nipo tayari kuhukumiwa sababu sipo juu ya sheria na pia nipo tayari niwekwe hadharani waninyonge sifai kuendelea kuwapo Tanzania kama nahusika na hilo, na kama sihusiki serikali initendee haki kwa watu wanaosambaza uvumi huu nao wachukuliwe hatua siyo wakae tu na kumrushia mtu vitu vya uongo.

Awali Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege, Deusdedit Kato akihojiwa katika kipindi hicho juu kwanini JNIA umeonekana kuwa kitovu cha kupitishia dawa za kulevya, alisema sababu kubwa ni kwamba kuna tofauti kati ya nchi na nchi katika masuala ya teknolojia katika kubaini dawa za kulevya.

Kamanda Kato alisema nchi nyingine wana vifaa vya kisasa zaidi na kwamba wakati sasa umefika kwa serikali kuwekeza katika kupata vitendea kazi zaidi ili kufanikisha mapambano ya dawa za kulevya.

Aliongeza kuwa wamekuwa wakishirikiana na viwanja vingine vya nchi mbalimbali kwa kubadilishana taarifa lengo likiwa ni mapambano ya biashara hiyo.

“Kimsingi wanaokamatwa wanakuwa ni wabebaji tu na siyo matajiri wa dawa za kulevya, bahati mbaya wabebaji wamekuwa wagumu sana kutoa ushirikiano kwa polisi, nasisitiza vitendea kazi vinachangia kuponya mtu asikamatwe nchini na kwenda kukamatwa nje,” alisema.

Kamanda Kato alisema katika kipindi cha miezi sita hadi nane watu 14 wamekamatwa wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya nchini.

•Julai 5, mwaka huu wasichana wawili, Agnes Jerald (25) na Melisa Edward (24), walipita JNIA na shehena ya dawa za kulevya kilo 150 na walikamatwa Afrika Kusini na kushtakiwa nchini humo kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya.

Hawa walikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo wakiwa na shehena ya dawa hizo aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 6.8.

•Ijumaa wiki iliyopita yaani Julai 26, mwaka huu, Watanzania wengine wawili, walikamatwa Hong Kong wakiwa na dawa za kulevya aina ya cocaine na heroine zenye thamani ya Sh. bilioni 7.6 akiwamo mmoja aliyekamatwa akitokea Dar es Salaam kupitia Dubai hadi Hong Kong.

Taarifa kutoka Hong Kong za Ijumaa wiki iliyopita zinaeleza kwamba, maofisa ushuru wa Uwanja wa Ndege wa Hong Kong (HKIA), walimkamata kijana mmoja mwenye umri wa miaka 26 akitokea Tanzania na alikuwa na dawa za kulevya aina ya heroine kilo 1.6 zenye thamani ya Sh. bilioni 1.5, kwenye mzigo wake wa mkononi.

•Siku hiyo hiyo jioni, maofisa hao walimkamata Mtanzania mwingine mwenye miaka 45 ambaye alipelekwa hospitali na kutolewa gramu 240 za dawa za kulevya aina ya heroine. Taarifa zaidi zilieleza kuwa Mtanzania mwingine mwenye miaka 28 alikamatwa akiwa na kilo 2.03 za cocaine.


Source: Nipashe.

8 comments:

Anonymous said...

Mheshimiwa Azzan unasema huamini kuwa kuna mtanzania amefungwa Hong Kong aliyeyaongelea hayo? Mbona juzi wamekamatwa wengine wawili hapo Hong Kong? Inaonekana umetuma watu wengi sana hadi wengine umewasahau! Kwa taarifa yako kuna zaidi ya watanzania 500 walio magerezani kuanzia Ugiriki, Pakistan, China hadi Brazil. Wengine wanasubiri kunyongwa huko Middle east. Kusema eti kama unahusika unyongwe, unajua kabisa kwamba kwa Tanzania yetu huwezi kunyongwa na polisi wote ni wala rushwa na wala hawana nia ya kufanya uchunguzi wowote. Nadhani mwenyekiti unatakiwa unyongwe kwa sababu umeshatajwa tayari huko Hong Kong na siyo na mtu mmoja tu ila na watu wengi sana. Kuanzia miaka 14 iliyopita mbona watu wengi walikuwa wanafahamu biashara unazozifanya, ni kuwa tu hapa nchini kwetu hakuna haki na pia ukiwa na pesa huwezi fanywa chochote licha ya kuwa mheshimiwa unashirikiana na polisi. Nakushauri kitu kimoja tu, wewe kama mbunge una kinga ebu jaribu kufanya ziara huko China au Hong Kong na ukiweza kurudi salama Tanzania tutajua kweli huhusiki. Kule wanatenda haki tu, hawasingizii.

Anonymous said...

ISIWE KISINGIZIO, UKWELI NA UONGO UNAO MWENYEWE, MNATUHARIBIA SIFA ZA NCHI TU, HII NI MICHOSHO SANA, TUNAONEKAN TAIFA LOTE NI LA WALE WALE, UMASKINI TUSIUVALIE KITKOT JAMANI,

Anonymous said...

Huyu jamaa wanamchafua tu na ndio ilikua lengo la ile barua maana waliotajwa wengine ni magumashi ..wameandikwa nicknames wakati huyu ndo jina lake halisi..kwa hio hapo ujue huyu ni mlengwa wa barua ile na hayo ni MAJUNGU TU!!!!kuna watu wnataka ubunge 2015!!

Anonymous said...

kati ya majina yaliyotajwa nani kaonewa? Migomigo na K'ndoni nzima wajulikana, Au umekuwa kama Jerry Slaa kwamba yeye ana macho mawili na serikali ina macho ishirini kwa hiyo sio jukumu lake kupambana na madawa. na huko polisi unapokimbilia wao ndio moja ya sababu hii biashara kushamili. # Samuel Sitta tume nyingi za uchunguzi ni kanyaboya. kama we mkweli nyamaza acha kuapia, yote yatajulikana. kwana, "hakuna mapana yasiyo na mwisho".

Anonymous said...

wewe jamaa hapo juu unaesema hayo ni majungu, una tokea wapi? una ndugu au marafiki walio athiririka na madawa? hao watu waliotajwa na hayo majina ya nick name ndio majina yao wanojulika nayo kabla hata hawajaanza hiyo biashara, majina yao ya kweli yakitajwa hata ndugu zao hawayakumbuki vizuri. labda wewe ni miongoni mwa wanaonufaika na biashara hii. hii sio kuhusu uchaguzi 2015, imefika wakati wa kuambiana ukweli na kuoneana huruma. Iddi akiwa kama mbunge, ameusika hakuhusika na jimbo lake ni kama makao makuu ya watu waliotajwa, Anaitaji kujiuzulu.Au badala ya yeye kusimama na kujitetea na kulia anatakiwa ahanzishe vita dhidi ya madawa ya kulevya ndani ya jimbo lake akianza na majina yaliyotajwa. kuanzia leo hii.

Anonymous said...

Hiyo barua imetokaje huko jela hadi kufika huku? Kaileta nani? Si amino kama ni ya kweli na inazidi kuchafua jina la Tanzania. Lakini Sioni ajabu kwa hilo maana watanzania tumezoea kuamini na kushikilia mabango habari za kizushi ila kizuri ni kwamba baada ya wiki chache kila mmoja anasahau na maisha yanasonga mbele

Anonymous said...

Walioandikwa nicknames wanajulikana kwa hayo majina mitaani, mbona ni jambo la kawaida tu. Iddi Azzan hapa Kinondoni nani asiye mjuwa, binamu yangu yuko jela South Africa na alishasemaga marafiki zake ndiyo waliomponza kwa kumpeleka kwa kundi la Iddi Azzan awe punda. Huyu mtu ni muuza sembe mkubwa tu. Hayo yote anayoyasema ni kujitapatapa tu kwani hapa Tanzania nani atampiga risasi ikiwa rais mwenyewe hafuatilii kitu.

Anonymous said...

wewe anonymous at 11:17 PM, ni nini kinachochafua jina la Tanzania, je ni barua iliyoandikwa kutoka jela au ni idadi ya watanzania wanaoshikiliwa nje ya nchi kwa usambazaji wa madawa ya kulevya?
Watanzania we need to think better than this, kah!