Advertisements

Wednesday, July 24, 2013

Rage auzika rasmi Uwanja wa Simba

Hati bado hawajapewa na watapewa siku yoyote.  Kiwanja kipo Bunju plot no. 226 block 1 Extension.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage ameifuta ndoto ya klabu hiyo kuwa na uwanja wake, baada ya kusema haiwezekani uongozi wake kujenga uwanja katika miaka miwili wakati Serikali imejenga Uwanja wa Taifa kwa miaka 50.
Rage alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki kwenye mkutano mkuu wa klabu hiyo uliofanyika Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay huku ukitawaliwa na vurugu zilizosababisha ajenda za muhimu za mkutano kushindwa kujadiliwa kwa kina.
‘’ Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi CCM imewachukua miaka 50 kujenga uwanja wa kisasa ule wa Taifa, sasa mimi Rage na Kamati yangu tutajenga uwanja wa kisasa kwa miaka miwili uwezo huo tunatolea wapi? “alihoji “Vitu vingine vinahitaji kufikiria kwa kawaida tu jamani. Tunaomba muwe wavumilivu tunaenda polepole, lakini kwa uhakika tumeshalipia eneo la ujenzi tunasubiri hati yetu.
Kauli hiyo ilizua majadiliano kutoka kwa wajumbe, lakini Rage aliendelea kusema  ‘’nipo kwenye agenda ya saba nyie pigeni kelele tu mimi naendelea (huku akicheka).
Hapa kuna watu wanataka kwenda kuangalia mpira, tena mtaingia bure na  vitambulisho vyenu, vya mkutano, Simba oyeeee’’.
Licha ya Rage kutoa kauli hiyo, mwenyekiti huyo amekuwa akitoa kauli tofauti tangu alipoingia madarakani juu ya ujenzi wa uwanja huo ambao umebaki kuwa ni ndoto.
Baadhi ya kauli zake ambazo amewahi kuzitoa ni hizi, Desemba 17/2010, alisema mradi wa kujenga uwanja huko Bunju kwa ajili ya timu yao unaendelea vizuri, lakini  mwekezaji wao kutoka Uturuki ambaye alitarajia kuja hivi karibuni atawasili mwakani mara baada ya kupita Sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya.
 “Kwa sasa tumebuni mradi ambao utasaidia kupata fedha kama sh 100 milioni ambazo zinatakiwa kulipia uwanja wetu.
 Mradi huo ni uuzwaji wa jezi ambazo zitauzwa kati ya sh10,000 na 15,000 kwa wanachama wa Simba kwa ajili ya kuchangia gharama za kulipia kitalu hicho.
Novemba 29/2010, Rage alitangaza mipango ya kujenga uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 30,000, eneo la Bunju na ujenzi utasimamiwa na Kampuni ya Uturuki GIDS, na akajikamba ni mabingwa wa ujenzi wa viwanja.
“Uwanja utazungukwa na maduka ya kisasa (Mall) na aliunda timu akiwemo aliyekuwa Makamu Mwenyekiti aliyebwaga manyanga Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Francis Waya, Katibu Mkuu wao Evodius Mtawala.
Mwaka 2011, Rage alitangaza ujenzi wa uwanja huo utagharimu Sh 74 bilioni, lakini bila ya kusema fedha nyingi kiasi hicho zitapatikana wapi. 
Juni 6 2011, Rage alisema Serikali ya Tanzania na Uturuki, kwa pamoja, zimekubali kuwasaidia upatikanaji wa fedha za ujenzi wa uwanja na kutiliana saini ya mkataba wa awali na kampuni ya Petroland ya nchini Uturuki kwa ajili ya kutafuta fedha za ujenzi wa uwanja wa kisasa wa klabu hiyo.
 Rage hakuishia hapo.  Septemba 26, 2011, alisema wataalamu wa masuala ya ujenzi kutoka nchini Uturuki wanakuja nchini Oktoba 5 mwaka huo kwa ajili kulifanyia tathmini eneo linalotarajiwa kujengwa ‘Simba Sc Arena’, huko Bunju.
Januari 2 2012, Rage alisema Simba tayari wamepata kibali cha kumiliki kiwanja chao cha Bunju na kwamba wanatakiwa kulipa Sh85 milioni ili wapatiwe hati halali ya kumiliki uwanja huo na kwamba tayari wameshalipa Sh50 milioni na kudai ndani ya miezi sita ambayo wamepewa watakuwa wamemaliza deni hilo.
Rage alisema hata wadhamini wa ujenzi wa uwanja wao kutoka Uturuki walikuwa wajanja kwani walikataa kuanza ujenzi wa uwanja huo mpaka wakione kibali hicho. “Sasa tumeshapata kibali hicho ujenzi utaanza mara moja.
Agosti 5 2012, Rage alifanya harambee kila mwanachama atoe Sh1,000 katika mkutano mkuu wa mwaka wa klabu hiyo uliofanyika Bwalo la Maofisa wa Polisi na kusema anahitaji Sh30 milioni ili wapate hati ya uwanja wao.
Katika Harambee hiyo, Rage na Makamu wake (Kaburu), kila mmoja alitoa kiasi cha Sh5 milioni, Zakaria Hans Pop (mil 10), Mjumbe Swed Mkwabi (Mil. 3), Said Pamba (mil 2), Lameck Patel na wadhamini  TBL kupitia kwa muwakilishi wao George Kavishe, Sh1 milioni.
Mwananchi

No comments: