ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 9, 2013

Shauri la Makada Chadema sasa Mahakama Kuu

Tabora. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Tabora, imesema haina uwezo wa kusikiliza kesi ya ugaidi inayowakabili makada watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kutaka kesi hiyo ipelekwe Mahakama Kuu Kanda ya Tabora.
Kesi hiyo ambayo sasa itaanza kusikilizwa Julai 22, makada hao wa Chadema wanatuhumiwa kummwagia tindikali Mussa Tesha, Wilayani Igunga wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo mwaka 2011.
Kesi hiyo ya ugaidi ilifunguliwa mahakamani hapo mwezi Juni 24 baada ya washitakiwa hao kuachiwa awali na Mahakama ya Wilaya ya Igunga.
Awali watuhumiwa walikuwa; Evodius Justunian, (30) mkazi wa Bukoba, Oscar Kaijage (Shinyanga), Seif Magesa (Nyasaka Mwanza), na Rajabu Daniel mkazi wa Dodoma, wanashitakiwa na Mahakama ya Wilaya ya Igunga katika kesi ya kumteka Mussa Tesha na kummwagia tindikali kabla ya Henry Kilewo naye kuunganishwa katika kesi hiyo.
Juni 31, mwaka huu watuhumiwa waliachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Igunga kabla ya kukamatwa tena baada ya kuachiwa na kupelekwa mkoani Tabora na kufunguliwa kesi mbili za ugaidi na kudhuru mwili kwa tindikali.
Mahakamani jana
Washitakiwa hao walifika mahakamani jana majira ya saa 10:12 wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia, FFU na kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Tabora, Issa Ibrahim Magori.
Baada ya Wakili wa Serikali Juma Masanja kutaja kesi hiyo, Hakimu alitoa maelezo yake kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa mamlaka wa kutolea uamuzi wa maombi yaliyowasilishwa na mawakili wa upande wa utetezi.
Akiendelea kusoma uamuzi huo Hakimu Magori alisema kuwa maombi yaliyowasilishwa katika mahakama hiyo yapelekwe Mahakama Kuu ili yapatiwe ufumbuzi wa kisheria.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alisema kuwa mahakama hiyo imeshindwa kutoa uamuzi wa maombi yao wakati Katibu wa Chadema mkoa wa Tabora, Athumani Khalfan Balozi aliwataka wanachama wa chama hicho kuwa wavumilivu wakati huu mgumu.
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Wapuuzi woote wanaotaka kuharibu amani ya nchi yetu!! Kama kweeli wameshiriki tukio hilo naomba wapoteleee jela tu maana Tanzania hatuhitaji wavuruga amani nchini mwetu!!! kuwa na vyama vingiii haimaanishi vurugu inamaanisha kuwa na mawazo tafauti tu. sasa wao kama wanavuruga amani ya nchi yetu hatuwataki katika jamaniii wakae humo Jela kabisaaaaa.