Waziri wa Katiba na sheria,Mathias Chakawe
Akizungumza na waandishi wa habari jana, jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Wizara, Farida Khalfan, alisema kutungwa kwa sheria hiyo kunafuatia kilio cha muda cha wananchi, ambao wamekuwa wakipata shida katika kupata haki kutokana na uwezo mdogo wa kifedha.
"Maandalizi ya muswada kwa ajili ya sheria hiyo yapo katika hatua za mwisho serikalini kabla ya kuwasilishwa bungeni. Lengo la serikali ni kuwa ifikapo Januari, 2014 sheria hii iwe imekamilika," alisema.
Alisema pamoja na mambo mengine, sheria itakayotungwa itaunda chombo huru kitakachokuwa na majukumu mbalimbali, ikiwamo kusajili taasisi zinazotoa msaada wa kisheria nchini pamoja na kusajili watoa msaada wa kisheria.
Pia alisema chombo hicho kitaweka viwango vya ubora katika utoaji misaada ya kisheria na kuvisimamia viwango hivyo, kusimamia nidhamu na maadili ya watoa huduma za msaada wa kisheria, kutambua wasaidizi wa kisheria na kutafuta fedha ili kutekeleza majukumu yake.
Alisema kutokuwapo kwa sheria, kumesababisha kuwapo kwa watu wasio na taaluma ya sheria, maarufu kama "Bush Lawyers", ambao wamekuwa wakiwarubuni wananchi na kuzalisha migogoro ili wapate fursa ya kuitatua kwa malipo.
Alisema sheria hiyo itasaidia kupata haki ya msaada wa kisheria bila malipo kwa makundi maalum, kama vile watoto, wajane na wasio na uwezo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment