ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 29, 2013

Simba yalala kwa Coastal

Kocha wa Simba  Abdallah Kibadeni

Simba ya Dar es Salaam jana ilishindwa kufungua makucha yake wakati ilipokubali kipigo cha goli 1-0 kutoka kwa Coastal Union katika mechi ya kirafiki ya kujiandaa na msimu mpya kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Wekundu wa Msimbazi waliwaanzisha katika kikosi cha kwanza viungo, Abdulhalim Humoud na Ramadhani Chombo 'Redondo', lakini walikuwa ni wenyeji walioibuka wababe kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Hata hivyo, matokeo hayo hayapaswi kuwapa hofu mashabiki wa Simba, kwani kocha Abdallah 'King' Kibadeni alisema mapema kuwa anawajaribu nyota wake hivyo matokeo hayana maana yoyote kuelekea msimu mpya.

Timu hizo ziliutumia mchezo huo kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakayoanza Agosti 24, mwaka huu.

Humoud, ambaye aliruhusiwa kuondoka Azam baada ya kupata ofa ya kujiunga na timu inayoyumba nchini Afrika Kusini ya Jomo Cosmos, alisema anaipenda Simba ndiyo maana amerejea kujifua katika timu hiyo aliyoichezea kabla ya kutua Azam.

Redondo naye amerejea kikosini baada ya kuomba radhi kufuatia kusimamishwa na uongozi pamoja na wachezaji wengine kwa makosa ya utovu wa nidhamu.

Wenzake Redondo waliokuwa wamesimamishwa pamoja, beki wa kati Juma Nyosso na kiungo Haruna Moshi 'Boban', wote wamesajiliwa na Coastal Union ambayo inasukwa upya ili kurejea katika chati zake baada ya kuyumba kwa muda mrefu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: