
Arusha. Matukio ya kigaidi yaliyolikumba Jiji la Arusha imevilazimisha vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha ulinzi kwa viongozi wa kitaifa wanaofika Arusha, ambapo wote wanaohusika kwenye ziara na mapokezi yao hukaguliwa kwa mitambo maalumu.
Waliofika uwanja mdogo wa ndege Arusha kumpokea Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilali, Julai 7 mwaka huu, wakiwemo waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali walikaguliwa kwa kupitishwa kwenye mashine maalumu za usalama.
Dk Bilal alifika Arusha juzi kufungua mkutano wa 32 wa mawaziri, makatibu wakuu, wakurugenzi watendaji wa mamlaka za mawasiliano, wakuu wa posta na wadau mbalimbali huduma za posta kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mashirika ya Posta Afrika (Papu).
“Ndugu wana habari, naomba wote wenye mabegi, mikoba, kamera na vitendea kazi vingine waviweke eneo maalumu kwa ajili ya ukaguzi wa vyombo ya usalama.” alisema Inocent Mungi, Meneja Mawasiliano wa TCRA ambao ndiyo wenyeji wa mkutano huo.
Arusha imekumbwa na matukio mawili ya milipuko ya mabomu ya kurusha kwa mikono yaliyopoteza maisha ya watu saba na zaidi ya 120 kujeruhiwa.
Mei 5, mwaka huu bomu lilirushwa kwenye kundi la waumini wa Kanisa Katoliki waliohudhuria Ibada ya kuweka wakfu Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, eneo la Olasiti na kuua watu watatu.
Tukio lingine ni lile la bomu la kijeshi iliyotengezwa China kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kurushwa kwenye mkutano wa kampeni ya Chadema kwenye Viwanja vya Soweto na kuua watu wanne.
Akifungua mkutano wa Papu jana, Dk Bilal aliwataka wanazuoni Afrika kutumia elimu yao kwa maendeleo ya jamii wanamoishi, nchi zao na bara nzima la Afrika ili kuiwezesha Afrika kufikia maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa kama ilivyo kwenye mabara mengine zilizopigwa hatua kubwa kimaendeleo.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment