KAMA ada tumekutana tena kwenye kona yetu ya Mapenzi na Uhusiano ili kujuzana mawili matatu kuhusiana na uhusiano wetu wa kila siku.
Leo ni chungu 17 Ramadhani kwa wafungaji. Hiki ni kipindi ambacho kwa wenye watoto wapo kwenye maandalizi ya nguo za sikukuu.
Tunaendelea na mada zetu kama kawaida, nimekuwa nikipata maswali mengi kutoka kwa wapenzi juu ya matatizo yanayojitokeza kiasi cha mmoja kushindwa kumwelewa mwenzake.
Wengi penzi lao huanza kwa kasi ya ajabu, kila mmoja akionyesha mapenzi kwa mwenzie, hapo kila mtu huamini mwenzake anampenda kama anavyompenda yeye, ndipo neno tunapendana linaleta maana. Lakini baada ya muda penzi huonekana kupoteza mwelekeo baada ya mmoja kuonekana kama haonyeshi ushirikiano kwa mwenzake.
Jambo hili humfanya mmoja awe njia-panda, asielewe kipi kinaendelea kwa vile mwanzo haikuwa vile, kama kuwa pamoja kwa muda mrefu na mawasiliano yasiyokatika.
Hii ni pamoja na uwazi katika penzi lenu ambalo kila mmoja alionekana kumpa uhuru mwenzake, lakini sasa mawasiliano yamekuwa adimu, ukaribu umepotea, penzi limeingiwa usiri mkubwa pia uhuru wa awali umepotea na watu kuwekeana mipaka.
Hapo ndipo anayeumia anaanza kung’amua kuwa yeye na mpenzi wake wanapendana sana, lakini hivi sasa hamuelewi baada ya kutokea tofauti kwa niliyoyabainisha nyuma.
Hapa watu wengi huwa wanakosea kusema wanapendana, wakati mpenzi wako yote mliyokuwa mkifanya mwanzo wa penzi yenu, yamepotea. Swali linakuja: Je, mnapendana au unampenda?
Kama mwenzako haonyeshi ushirikiano wa awali uliofanya uamini unapendwa basi elewa hampendani bali wewe ndiye unayempenda pekee kwa vile maumivu unapata wewe.
Sehemu hii ndiyo inayowachanganya watu wengi na kujiuliza yapo wapi mapenzi ya mwanzo? Kama ni mfuatiliaji wa mada zangu ungejua penzi lenu lipo kwenye kundi gani. Penzi lenu lipo kwenye kundi la mtu kupenda kwa sababu fulani.
Kwa sababu gani?
Pengine utanashati wako na kuamini kuna kitu atapata kwako, umbile na sura nzuri ambalo humjengea picha fulani ambayo unayo mwilini mwako.
Watu wa aina hii huwa hawana mapenzi, hivyo wakivikosa walivyovifuata au kupata walichokitaka basi huondoka bila kwa heri au penzi huingia kwenye migogoro. Basi ukiona mpenzi wako haonyeshi mapenzi ya zamani na visingizio kibao, jua hapo hakuna mapenzi na tayari kapata alichokitaka kwako.
Kwa hiyo ondoa wazo la mnapendana, sema nampenda mwenzangu lakini yeye hanipendi. Ukilijua hilo jipange kufungua ukurasa mpya huku akijifunza makosa ya awali ya kukurupuka kwa mtu kuonyesha anakupenda kumbe kuna kitu anatafuta kwako.
Anayekupenda huonyesha ushirikiano, anayekwenda kunyume hana mapenzi na wewe, jua huyo unampenda wewe siyo mnapendana kwa vile wewe ndiye unayeteseka.
Kwa leo haya yanatosha tukutane wiki ijayo.
Global Publishers
No comments:
Post a Comment