Advertisements

Wednesday, July 31, 2013

Wanyarwanda wengi wakimbilia Uganda

Idadi kubwa ya raia wa Rwanda wameendelea kukimbia nchini mwao na kuomba hifadhi katika nchi jirani ya Uganda.

Licha ya juhudi za Rwanda kutaka raia wake walioko ugenini kurejeshwa nyumbani wakiwemo waliokimbia nchi mwaka wa 1958, kufuatia mapinduzi ya Ufalme, Wengi wa Wanyarwanda wangali na hofu ya usalama wao.

Waziri wa Uganda anayehusika na wakimbizi amesema wamepokea maombi 1800 kutoka kwa raia wa Rwanda. Afisa wa Shirika la Kimataifa linalowashughulikia wakimbizi-UNHCR, ameambia BBC kwamba wakimbizi hao waliingia Uganda mwezi Mei mkwaka huu.

Huenda idadi hii imeongezeka baada ya raia wengine kudaiwa kukimbia Rwanda katika siku za karibuni.Afisa wa serikali ya Uganda amesema raia wa Rwanda wameendelea kuomba hifadhi Uganda kwa madai ya kutishwa na serikali kutokana ma misimamo yao ya kisiasa, baadhi wanadai kuwepo na ukiukaji wa haki za binadamu.

Hata hivyo siyo wote walioitikiwa maombi yao.Miezi miwili iliyopita, wanafunzi 16 wa Rwanda walitorokea Uganda kwa madai ya kulazimishwa kujiunga na wapiganaji wa M23 wanaoendesha harakati zao Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Baadhi ya wakimbizi wamedai kutoroka makundi ya waasi baada ya kulazimishwa na serikali kujiunga nayo.Wataalamu wa Umoja wa Mataifa, Marekani na Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo wamelaumu Rwanda kwa kuwafadhili waasi wa M23, lakini mamlaka ya Rwanda imekanusha madai hayo na kutaka ushahidi kutolewa kudhihirisha wanaunga mkono M23.

Takriban wakimbizi 20,000 wa Rwanda wanaishi nchini Uganda wengi kutoka jamii ya Wa-Hutu. wanadai kudhulumiwa na utawala wa sasa wenye Wa-Tutsi wengi.

No comments: