ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 27, 2013

Brandts, Morocco watunishiana misuli

Huku timu zao zikiwa zimeshinda mechi za kwanza za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, kocha wa Yanga, Ernie Brandts amesema kuwa kikosi chake kina uwezo wa kushinda mechi ya kesho huku kocha Hemed Morocco wa Coastal Union ya jijini Tanga akitamba 'kuwavurugia' mabingwa hao watetezi.

Yanga ilianza ligi kwa ushindi wa magoli 5-1 dhidi ya Ashanti United wakati Coastal Union iliyosukwa upya ilishinda 2-0 dhidi ya JKT Mgambo ugenini Arusha Jumamosi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Brandts alisema kuwa timu yake imejiandaa kukabiliana na ushindani kutoka katika timu zote hivyo hawatarajii kupoteza mechi hiyo ya raundi ya pili itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Brandts alisema kwamba anajua mechi hiyo itakuwa na ushindani kwa sababu wapinzani wao wamefanya mabadiliko katika kikosi chao na wana morali baada ya ushindi wa mechi yao ya ufunguzi.
Mholanzi huyo alisema kwamba timu yake iko katika hali nzuri na watatumia faida ya uwanja wa nyumbani kuwakabili wapinzani wao.

Morocco ambaye waliwasili jijini juzi usiku amewataka mashabiki wa timu hiyo kujiandaa kuona soka la kisasa ambalo lengo lake ni kushinda na kutoa burudani.

Alisema kwamba hawaidharau Yanga na anafahamu ni wachezaji gani 'hatari' wanafaa kuzuiwa (hakuwataja majina) ili kuwadhibiti katika mechi hiyo.

"Najua nani anafaa kutulizwa na njia zipi za kuzuia ili kuvuruga mipango yao," aliongeza Morocco, ambaye alikuwa kocha mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Zanzibar Heroes.

Alimtaja mchezaji wa timu ya taifa ya Kenya (Harambee Stars), Crispin Odulla na Daniel Lyanga kuwa ndio nyota watakaoongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo iliyowahi kutwaa ubingwa wa Bara mwaka 1988.

Alisema pia nyota wa zamani wa Simba ambao wametua kwenye kikosi hicho, Juma Nyosso, Uhuru Suleiman na Haruna Moshi ' Boban' wanatarajia kuisaidia timu yake kupata ushindi hapo kesho.

Daktari wa Yanga, Nassor Matuzya, aliwataja wachezaji ambao wametoka kuwa majeruhi na wanafanya mazoezi mepesi kuwa ni pamoja na Kelvin Yondani, Athumani Iddi 'Chuji' na Ibrahim Job.

Baada ya mechi za kesho kumalizika, ligi hiyo itasimama kupisha kambi ya timu ya Tanzania (Taifa Stars) itakayoanza keshokutwa ili kujiandaa na mechi ya kukamilisha ratiba ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Gambia.
CHANZO: NIPASHE

No comments: