ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 13, 2013

Dk Ndalichako ‘achanachana’ ubora wa elimu Tanzania

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Nchini (Necta), Dk Joyce Ndalichako

Arusha: Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Nchini (Necta), Dk Joyce Ndalichako amesema karatasi za majibu ambazo wamekuwa wakizipata kutoka kwa wanafunzi zinaonyesha kuwa, watoto wengi wanahudhuria shuleni lakini hakuna wanachojifunza.
Dk Ndalichako aliyasema hayo jana jijini hapa alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa mabaraza ya mitihani ya Afrika, ambao umejikita kujadili suala la tathimini ya elimu kwa nchi za Afrika.
Hii ni mara ya kwanza kwa Dk Ndalichako kuzungumza tangu Serikali itangaze kufuta matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012 na kutaka yapangwe upya, suala ambalo lilipingwa na wadau wengi wa elimu.
Alisema kuwa wakati nchi nyingi za bara hili zikiwa zimejitahidi kuongeza upatikanaji wa elimu kwa watu, ubora wa elimu unaendelea kuwa tishio kwa watu wa bara hili kwa vizazi vijavyo.
“Kama mabaraza ya mitihani, tumekuwa tukiona karatasi za majibu kutoka kwa wanafunzi ambazo zinaonyesha kwa uwazi kabisa kuwa watoto wanahudhuria shuleni lakini hakuna wanachojifunza,” alisema Dk Ndalichako.
Kwa upande wake Profesa Justinian Galabawa, alisema ili kuendeleza elimu, lazima uamuzi wa kitaalamu usiingiliwe na siasa kwa namna yoyote ile.
Alitolea mfano kitendo cha Serikali kufuta matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2012 akisema hakikuwa sahihi hata kidogo.
Alisema lazima vyombo vilivyopewa mamlaka kisheria kama Necta viachwe vifanye kazi bila kuingiliwa kwani kufanya hivyo kutaporomosha elimu.
Alisema pia lazima kuwa na sera ya nchi ya kufanya tathmini ambayo ili ifanye kazi lazima ishirikishe wadau wote na kila anayehusika kuitekeleza awe nayo.
“Jambo la kwanza ni lazima tuheshimu wataalamu na wasiingiliwe na wanasiasa, taasisi zilizoundwa kisheria na kupewa mamlaka ya kupima na kutambua watu ni lazima ziheshimiwe. Kama mtoto amepata daraja la nne huwezi kumpa la kwanza,” alisema Profesa Galabawa.
Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Seif Ali Iddi alisema mkutano huo ni sehemu nzuri ya Tanzania kujifunza kutoka kwenye nchi nyingine kujua ni nini watu wengine wanafanya.
Alisema uzoefu utakaopatikana kutokana na mkutano huu utasaidia katika kujipima na kuendeleza elimu nchini.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo, Philipo Mulugo alisema kwa siku ya kwanza tu wamebaini kuwa zaidi ya asilimia 80 ya nchi za Afrika tayari wanatumia mfumo wa usahihishaji kwa kutumia mashine maalumu (OMR) ambao bado baadhi ya watu nchini wanaulalamikia.
Alisema baadhi ya nchi sasa wameanza kusahihisha kwa kutumia kompyuta hata maswali ya kujieleza, hivyo akawataka Watanzania waache kujirudisha nyuma.
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

wakati umefika serikali ya tanzania lazima iongeze bajeti kuwekeza katika elimi. lazima tupati shule bora, walimu bora, na kuhakikisha viwango bora yote haya yanahitaji fedha, utaratibu mzuri na usimamizi madhubuti. vile vile tuige kwa wenzetu wa nchi zilizoendelea masomo ya msingi ni english na math. hayo yakifundishwa vizuri yanawapa wanafunzi upeo mkubwa katika sayansi na arts, miaka ya kusoma sekondari ifupishwe iwe ni 10 na miwili ya high school. angalau tukiweza kuzalisha 50% ya wanafunzi wetu wapate elimu ya chuo kikuu basi miaka 10 ijayo tanzania itakuwa imebadilika sana kimaendeleo. wataalamu ndio huleta mabadiliko ya kiuchumi kisiasa na hata kijamii, tuwaamini na tuwasaidie. usahihishaji wa mitihani uwe kwa compyuta labda kama tunaogopa watoto wa wakubwa watafeli zaidi.