
Wachezaji wa Simba na viongozi wao wakiwa katika picha ya pamoja jana baada ya kutembelea ofisi za gazeti hili Tabata Relini, Dar es Salaam. Picha na Micheal Matemanga
Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Abdallah Kibadeni amesema kutokujitambua kwa wachezaji wa sasa ni tatizo linalokwamisha soka la Tanzania kupiga hatua za kimaendeleo.
Kibadeni alisema hayo jana wakati klabu ya Simba ilipotembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen.
“Unajua Tanzania ina vipaji vya soka kama nchi nyingine zenye maendeleo ya soka, lakini tatizo letu kubwa liko kwa wachezaji wenyewe, hawajitambua na kuweka nia na malengo katika kile ambacho wanakifanya. Ni tatizo kubwa ambalo linatukabili kwa sasa.”
Alisema mbali na kutokuwa na ligi imara, pia suala la kutokuwa na shule za kulea na kukuza vipaji katika misingi iliyo bora ya soka.
“Wachezaji ni wavivu kujifunza na kuridhika mapema kwa mafanikio kidogo wanayopata.
Nafikiri ni ambavyo vinaturudisha nyuma kwa kiwango kikubwa.”
Alifafanua kuwa kutokana na hayo yote yamesababisha klabu nyingi zinazoshiriki Ligi Kuu kusaka mabeki wa kati na wafungaji kutoka nje ya nchi kitu ambacho kinazidi kulididimiza soka letu katika harakati za kutaka kupiga hatua moja mbele. “Elimu nayo kwa kiasi fulani imechangia. Idadi kubwa ya wachezaji katika mpira elimu zao ni kidato cha nne na darasa la saba. Nadhani ni tatizo lingine,” alisema Kibadeni.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itangare alisema siri ya mafanikio ya timu hiyo ni umoja na mshikamano wa viongozi na wanachama wa klabu hiyo. “Siri kubwa ya timu yetu kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ukilinganisha na klabu nyingine hapa nchini yamechangiwa na umoja pamoja na mshikamano kati ya viongozi na wanachama.
“Kila timu yetu inapokuwa katika mashindano akili zetu mara nyingi ni kuhakikisha tunafanya vizuri na ndiyo maana huwa tunafika mbali,” alisema Itangare.
Akizungumzia michuano ya Ligi Kuu ambayo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi hivi karibuni, Itangare alisema kuwa kwa upande wao kama viongozi wamejipanga kuhakikisha kikosi hicho ambacho kinaundwa na vijana wengi wenye umri chini ya miaka 25 kuhakikisha wanarudisha heshima yao.
Alisema wamejitahidi kusajili wachezaji wazuri ambao pia wapo chini ya kocha bora wa msimu uliopita, Abdallah Kibaden hivyo tuna matumaini ya kufanya vizuri katika msimu huu.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment