
Wiki iliyopita utakumbuka nilianza kuzungumzia mada yenye kichwa cha habari hicho hapo juu. Ni mada ambayo imeonekana kuwagusa walio wengi na wiki hii nitaimalizia ili nihamie kwenye mada nyingine.
Kikubwa ambacho nataka kukisisitiza ni wanandoa na wapenzi kupeana uhuru wa kumiliki simu zao. Kitendo cha kudhani mpenzi wako anatumia simu yake katika kuwasiliana na mahawara zake inaonesha kwamba hakuna uaminifu baina yenu.
Haiwezekani simu ya mwenza wako ikiita tu tayari umeshainyakua na ukikutana na sauti ya jinsi tofauti tu unakosa uaminifu kwa mwenzako.
Jamani, huyo mpenzi wako hana kabisa marafiki wa kiume, hana ndugu wa kiume au wafanyakazi wenzake wa kiume? Kimsingi ukiwa mtu wa kumaindi vitu vidogovidogo kama hivyo mtakuwa mkikorofishana kila siku na mpenzi wako.
Hata hivyo, kaa ukijua kwamba ni vigumu sana kumchunga mwenza wako kupitia simu yake ya mkononi kwani akiamua kukusaliti anaweza kufanya hivyo bila hata kuhusisha simu yake na wewe usijue.
Mwenza wako anaweza kukupa uhuru wa kuishika simu yake na wewe kwa kuwa hukutani na mazingira ya kukushitusha ukaamini kuwa mpenzi wako ni muaminifu kumbe hamna kitu. Hivi hujui kwamba siku hizi wasaliti huwa na ‘line’ za kufanyia madhambi yao?
Sasa kama utakuwa ukijiaminisha kuwa mpenzi wako hakusaliti eti kwa kuwa hujawahi kuona sms kutoka kwa mwanamke au hujawahi kupokea simu yake ukakutana na sauti ya mwanamke utakuwa unajidanganya.
Kikubwa ni wewe kujenga imani naye na hata kama utakuwa unamfuatilia isiwe kwa wazi. Fanya hivyo bila yeye kujua na ikibidi ili kutojipa presha, acha kumfuatilia.
Aidha, uchunguzi wangu umenidhihirishia kwamba, kikubwa ambacho kimekuwa kikichangia katika hili ni wivu, wivu ambao naamini kabisa hauna lengo la kujenga bali kubomoa.
Nasema hivyo kwa sababu, ukichunguza sana utakuta wapenzi na wanandoa wengi ambao hawana uhuru na simu zao wamekuwa wakizozana mara kwa mara. Wamekuwa wakipeana shutuma zisizo na ukweli na matokeo yake kuishi katika mazingira yasiyo mazuri.
Kitu ambacho wengi walio katika uhusiano wa kimapenzi wanatakiwa kukizingatia ni kujiamini ili kuonesha simu zao hawazitumii katika kufanya madhambi. Kama kweli wewe ni mwaminifu kwa mpenzi wako, unatakiwa kujiamini kila unapokuwa karibu naye na wala usioneshe kujishtukia.
Wapo ambao kila wanapokuwa na wapenzi wao, wakipata sms tu, watajificha ili wasome haraka haraka kisha wa-’delete’. Wakipigiwa kama hamjui anayempigia basi atakwenda mbali kuipokea na wengine hulazimika kabisa kuzizima simu zao wanapokuwa na wapenzi wao wakijua wakati wowote bomu linaweza kulipuka.
Hivi unapofanya hivyo unataka mpenzi wako akufikirieje? Utamjengea mazingira gani ili akuamini kwamba hauna mtu mwingine? Kimsingi huwezi kubadili mawazo yake, atakaa akijua hayuko peke yake na matokeo yake sasa mapenzi yatapungua na amani inaweza kutoweka kabisa.
Kimsingi kutokujiamini kwako kunaweza kukuharibia kwa mpenzi wako na ndiyo maana nasema kwamba kama kweli unampenda huyo uliye naye usiweke mazingira ya usiri kwenye simu yako.
Wakati mwingine kuwa tayari kumjibu pale atakapokuuliza ni nani aliyekupigia simu au ujumbe huo unatoka kwa nani. Siyo kila mara atakuuliza lakini pale atakapokuuliza mjibu.
Lakini kikubwa ambacho unatakiwa kukiweka akilini mwako ni kumpa uhuru mpenzi wako atumie simu yake na wewe tumia yako. Tusizipe nafasi simu zetu zitutenganishe na wale tuliotokea kuwapenda.
Tusiwakoseshe amani wapenzi wetu kwa kuwafuatilia sana juu ya matumizi ya simu zao. Kama mpenzi wako anafanya kazi ambayo inahitaji awasiliane sana na watu, hilo lisikufanye uhisi unasalitiwa. Jipe amani ili na mwenza wako naye awe na amani.
Ila sasa ukibaini mwenzako amebadilika na ukahisi anaitumia simu yake kukusaliti, katika kumchunguza unaweza kuwa unaishika simu yake kwa ‘timing’ sana bila yeye kujua.
Kwa leo naomba niishie hapo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine. GPL
No comments:
Post a Comment