ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 1, 2013

POLISI WAKINZANA MAUAJI YA MERERANI ARUSHA, TANZANIA


WAKATI Jeshi la Polisi mkoani Manyara likiendelea na uchunguzi kuhusu tukio la mauaji ya mfanyakazi wa Kampuni ya Tanzanite One, Willy Mushi, aliyepigwa risasi akiwa chini ya ardhi mgodini, mtuhumiwa Joseph Mwakipesile ‘Chusa’, aliyekuwa akishikiliwa kwa kuhusishwa na mauaji hayo amehamishiwa mjini Babati kutoka kituo cha Mirerani.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa, alisema jana kuwa jeshi hilo linafanya upelelezi wa kina kuhusu mauaji hayo, kuhakikisha wahusika wote wanatiwa mbaroni na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria kujibu tuhuma dhidi yao.

“Kwamba mtuhumiwa anashikiliwa kituo gani cha polisi baada ya kutolewa Mirerani hilo sitakueleza, ila ni kweli tunaendelea kumshikilia kwa mahojiano zaidi,” alisema Mpwapwa.
Marehemu Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi usiku wa kuamkia Julai 21, mwaka huu alipokuwa kazini na wenzake katika migodi ya Tanzanite One eneo la kitalu ‘C’, baada ya kuvamiwa na wachimbaji wadogo walioingia katika migodi ya kampuni hiyo kwa nia ya kuiba madini.

Katika hatua nyingine, taarifa ya polisi Mkoa wa Manyara iliyotumwa makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam imebainika kujichanganya kuhusu umiliki na mahali marehemu alipopigiwa risasi, ambapo badala ya kueleza kuwa mauaji yalitokea kitalu ‘C’ kinachomilikiwa na Tanzanite One, taarifa hiyo inadai yalitokea kitalu ‘D’.

Kitalu ‘D’ kinamilikiwa na wachimbaji wadogo kama ilivyo kwa kitalu ‘B’, hivyo taarifa ya polisi Manyara kudai mauaji yalitokea kitalu ‘D’ inamaanisha wafanyakazi wa Tanzanite One ndio walivamia migodi ya wachimbaji wadogo, jambo ambalo si kweli.

Kwa mujibu wa taarifa ya awali ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO) wa Manyara, Bernard Msuya, iliyotumwa kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, inaonesha eneo la Delta Sharft Level 23 ndiko mauaji yalikotokea kitalu ‘D’, tofauti na ukweli kwamba eneo hilo ni kitalu ‘C’.

Taarifa hiyo yenye kumb. namba MRN/CID/SCR/146/2013/3 ya Julai 23, mwaka huu inadai marehemu na wenzake walifyatuliwa risasi ambazo mbili zilimpiga kifuani na kumuua papo hapo walipokuwa wakikagua eneo la mtobozano katika kitalu ‘D’, ambalo linamilikiwa na wachimbaji wadogo, wakati kiuhalisia mauaji yalitokea kitalu ‘C’ kinachomilikiwa na mwekezaji.

Bila kujulikana iwapo ni makusudi au bahati mbaya, taarifa hiyo pia imepotosha ukweli kwa kudai mgodi wa mtuhumiwa Chusa unapakana na eneo la Delta Shaft Level 23 la Tanzanite One yalikotokea mauaji, jambo ambalo si kweli.

Akizungumzia mkanganyiko huo, Kamanda Mpwapwa alisema hiyo ni taarifa ya awali iliyopatikana baada ya upelelezi wa awali kuhusu mauaji hayo, hivyo si ajabu kuwa na makosa madogo madogo ambayo yatarekebishwa wakati upelelezi wa jumla utakapokamilika na polisi kukusanya ushahidi na nyaraka za kutosha.

No comments: