ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 1, 2013

SASA TANZANIA TUMEKUWA TAIFA LA WAUZA UNGA

Moja ya sifa ambazo Tanzania imejizolea katika medani za kimataifa katika miaka ya hivi karibuni, ni sifa ya kuwa moja ya vinara wa biashara ya dawa za kulevya duniani. Tofauti na sifa nyingine ilizonazo, ikiwamo sifa ya kuwa taifa lenye amani na utulivu, mara hii sifa ya kubobea katika biashara ya dawa za kulevya siyo sifa ya kujivunia hata kidogo.
Ni sifa inayochafua taswira ya nchi yetu, kwani hivi sasa Watanzania wanaosafiri nje ya nchi wanaficha nyuso zao kwa aibu kutokana na upekuzi wa aina yake wanaofanyiwa na mamlaka za forodha na uhamiaji. Msafiri mwenye pasi ya kusafiria iliyotolewa na Serikali ya Tanzania kila anapoingia katika nchi ya kigeni anapata msukosuko mkubwa.
Matukio ya Watanzania kukamatwa ughaibuni wakiwa na dawa hizo hakika ni matukio yanayotoa taswira ya taifa linaloanza kupotea njia. Katika kipindi cha wiki mbili tu, Watanzania wanne wamekamatwa katika nchi mbalimbali wakiwa na dawa hizo na wakiwa wametokea Tanzania.
Mwezi uliopita, wasichana wawili Watanzania walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo, Afrika Kusini wakiwa na kilo 150 za dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya Sh6.8 bilioni wakitokea Dar es Salaam. Hata hivyo, kitendawili cha namna shehena hiyo kubwa ilivyoweza kupita uwanja wa ndege Dar es Salaam bila kugunduliwa na mamlaka husika bado hakijateguliwa. Hivi sasa wasichana hao wamefunguliwa mashtaka nchini humo.
Katika tukio la aina hiyo, Watanzania wawili wiki iliyopita walikamatwa Hong Kong, China wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya Sh7.6 bilioni wakitokea Dar es Salaam kupitia Dubai. Maofisa wa Uwanja wa Ndege wa Hong Kong (HKIA) wamesema kwamba katika wiki hiyo, walimkamata kijana mwenye miaka 26 akitokea Tanzania akiwa na dawa za kulevya kilo 1.6 aina ya heroin zenye thamani ya Sh1.5 bilioni na kwamba jioni ya siku hiyo, walimkamata Mtanzania mwingine mwenye miaka 45 akiwa amemeza gramu 240 za dawa za kulevya aina ya heroin.
Tatizo la biashara ya dawa za kulevya hapa nchini limekuwa kubwa, kwani takwimu zinaonyesha kuwa, kuna orodha kubwa ya Watanzania waliokamatwa ughaibuni wakiwa na dawa hizo na wengi wao wanasubiri kunyongwa. Jambo la kusikitika ni kuwa, pamoja na kwamba kwa muda mrefu Serikali imekuwa na orodha ya magwiji wa biashara ya dawa hizo, imekuwa ikishikwa na kigugumizi cha kuwataja au kuwafungulia mashtaka. Hata pale baadhi yao walipofunguliwa mashtaka, kesi zao zimekuwa zikipotea hivihivi tu pasipo maelezo.
Sisi tunadhani katika hili Serikali inastahili kubeba lawama kwa kuwalea na kuwakingia kifua magwiji wa biashara hiyo. Lazima tutambue kwamba Watanzania wanaokamatwa na dawa hizo hapa nchini na huko ughaibuni ni dagaa tu, kwani wenye biashara hiyo wamekaa kando na Serikali inawafahamu.
Mwishoni mwa wiki, katika mhadhara wa kongamano la kidini lililofanyika jijini Mbeya, vijana wawili waliokuwa wakitumiwa kusafirisha dawa hizo, walisalimisha kilo tano za dawa aina ya heroin baada ya kuguswa na mahubiri katika kongamano hilo, huku wakitaja majina ya wamiliki wa dawa hizo, wakiwamo baadhi ya mawaziri na wabunge. Sasa tumekuwa taifa la wauza unga.

2 comments:

Anonymous said...

Kweli inasikitisha sana kuona nchi yetu inafuata nyayo za Colombia na nchi nyingi za marekani kusini ambazo ni mabingwa wa kuuza madawa ya kulevya. Hayo siyo maendeleo ya kujivunia miaka 50 baada ya uhuru. Nashangaa kuona kwamba suala la madawa halikupewa nguvu wakati wa ujio wa Rais Obama. Ingekuwa vyema atusaidie kutuletea wataalamu wa DEA (Drug Enforcement Agency) badala ya kutuletea umeme! Pia hao viongozi wanaohusika na biahara hiyo haramu nao wawekewe vipingamizi (sanctions) wasitoke nje ya nchi kama bwana Mugabe wa Zimbambwe; na mali zao zitaifishwe. Nina imani Marekani inaweza kutusaidia vyema kuwakomesha hao wakuu serikalini kama walivyomkomesha bwana Noriega wa Panama miaka ya 80s. Napata uchungu kusikia wabongo tunaoishi ughaibuni tunatazamwa vibaya daima tuonyeshapo pasi zetu za safari.

Anonymous said...

Hivi kweli tupo dhahirina makini katika kulikomesha swala hili la hayo madawa yenu ya kuwalewesha watu wengine nanyi kujichukulia hizo hela kumwangamiza maisha mwenzio? Hebu turudi nyuma na kumwogopa mungu kidogo kwa haya matendo. Unamdanganya binadamu mwenzio kwa kumlipa ujira akusafurushie hilo janga lako na anaacha familia inayomtegemea na kuhatarisha maisha kuyaweka tumboni mauchafu hayo we umekaaa kusubili aufikishe ulipwe hela uendelee kujenga magorofa na magari ya kifahali mwenzio aendelee kuwa maskini. Ni wakati sasa geuka nyuma chukua.kioo jiangalie afu mwangalie unae mwangamizia maisha na familia kiujumla. Wewe waziri, mbunge au kiongozi au kiongozi yeyote uliyepewa dhamana ya kuwaongoza wenzio acha huo ujinga wa kutumia nafasi ulio nayo kinyume na maadili kuwa na imani na raia walio kuamini na kukupa dhamana yao. Achani tamaaa ridhikeni na mpatacho.na wewe unae danganywa na dhiki zako kama maisha ya mjini hayaendi rudi kibugumo kwenu tafuta eneo la kulima utapewa uwezo kwa kusaidiwa kwa kufanya ya maana nasio kuhatarisha maisha yako kwa taama za dola kadhaa. Inasikitisha sana na inauma sana kwa nyie wahusika tafuta hela kihalali na sio kijangili jangili.