ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 26, 2013

TANZANIA DMV YAIBAMIZA VIATAMBI FC 6-4


 Timu ya Vitambi FC
Tanzania DMV
Na Mwandishi wetu, DMV
Timu ya Tanzania DMV jana Jumapili Aug 25, 2013 iliisambaratisha timu ya Vitambi FC (DMV) 6-4 katika viwanja vya Layhill Park vilivyopo Silver Spring, Maryland mpaka mapunziko Tanzania DMV ilikua mbele kwa goli 3-0.

Mchezo wa jana ulikuwa ni mchezo wa kirafiki wa kujipima nguvu na wasukuma kabumbu timu inayoundwa na  Wakenya wanaoishi hapa DMV kwa ajili ya kujiweka sawa na michuano ya siku moja itakayofanyika Labor Day Weekend siku ya Jumamosi Aug 31, 2013 kuanzia saa 4 asubuhi katika Viwanja hivyo vya Layhill Park.

Mashindano hayo yameandaliwa na Vitambi FC na yameshilikisha timu mbalimbali zikiwemo timu ya Wakenya kutoka New Jersey(New Jersey Stars), Wakenya kutoka Baltimore (Watembezi FC), Malawi (DC Flames), Tanzania DMV na wenyeji Vitambi FC.


Katika mchezo wa jana timu ya Tanzania DMV ilicheza vizuri hasa kipindi cha kwanza na kujipatia bao la kuongoza kunako dkk ya 5 ya mchezo baada ya kutokea makosa ya mabeki wa Vitambi FC kusita kuokoa krosi ya mchezaji wa Tanzania DMV, Yusuf aliyeipiga kutokea winga ya kushoto na mpira kuwambaa kuelekea golini huku ukiwapita mabeki wa Vitambi FC akiwemo golikipa wao Victor na kumkuta mfungaji aliyeuweka mpira kimyani kirahisi na kuhesababu bao la kwanza kwa Timu ya Tanzania.

Bao la pili la Tanzania DMV lilifungwa na mchezaji Yusuf ambaye kawaida hucheza beki ya kulia lakini jana alicheza kama fowadi wa kati na kuweza kuimudu namba hiyo kama kwamba alikuwa akiicheza kila siku. Na kunako dkk ya 38 ya mchezo Adam DC aliipatia timu ya Tanzania bao la 3 kwa shuti kali nje ya 18 lililomshinda golikipa wa Vitambi FC  kuipeleka Tanzania DMV mapumziko ikiwa kifua mbele ya bao 3-0.

Kipindi cha pili kilifanyika mabadiliko ya wachezaji kwa timu zote mbili, yaliisaidia sana timu ya Vitambi FC kwa kufufua safu yake ya ushambuliaji ambayo ilionekana butu kipindi cha kwanza na kuipatia bao la kwanza kunako dkk ya 57 ya mchezo mfungaki akiwa Kenny baada ya kushirikiana vyema na mchezaji Yahaya kwa kupigiana pasi za one, two na kumkuta mfungaji akiwa peke yake na golikipa Said Mwamende na kuiandikia Vitambi FC bao la kwanza, bao lililoiamsha timu ya Tanzania DMV usingizini na kuanza kufanya mashambulizi ya mara kwa mara na kuzaa matunda dkk ya 69 na kujipatia bao la 4 mfungaji akiwa David baada ya kujikuta peke yake na kipa kwa makosa ya mabeki wa Vitambi FC kudhani mfungaji alikua ameotea.

Vitambi FC walijitahidi kupunguza mabao hayo kwa kujaribu kucheza mpira kwa kutumia pasi ndefu na kupeleka mashambulizi kwa kushtukiza lakini ukuta wa timu ya Tanzania DMV uliokua ukiongozwa na Libe, Dullah, kwa kushirikiana na Adam NY bila kumsahau Mude walikua imara muda wote kujaribu kuzuwia mashambulizi ya Vitambi FC.

Kunako dkk ya 75 timu ya Tanzania walijipati bao la 5 bao lilitiwa kimiani na Mude baada ya kutokea piga ni kupige katika goli la Vitambi FC. Baada ya bao hilo lilizidi kuwatia hasira timu ya Vitambi FC na kuanza kulishambulia goli la Tanzania DMV kama nyuki na kuweza kupata bao la 2 kwa shuti dhaifu nje ya 18 mfungaji akiwa Yahaya na kumkuta kipa wa Tanzania DMV asijuwe la kufanya.

Kunako dkk ya 83 Tanzania DMV walipachika bao la 6 kutoka kwa mfungaji wao mpya aitwae Peter kwa kumpiga kanzu golikipa wa Vitambi FC aliyejaribu kuuwahi mpira na Peter kujikuta yupo yeye na nyavu na bila ajizi akaujaza mpira wavuni na kuiandikia bao lililofunga kitabu cha magoli kwa timu ya Tanzania DMV. Vitambi FC walijipatia mabao ya mawili ya haraka haraka dkk ya 87 na 89 na kuonekana kama wangeweza kurudi kwa kijaribu kutumia mwanya wa kuchoka kwa mabeki wa timu ya Tanzania DMV lakini bahati haikuwa yao mpaka dkk ya 90 Tanzania DMV 6 Vitambi FC 4.

No comments: