ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 27, 2013

WALIOPITISHA ‘UNGA’ WATIMULIWA

Waziri wa Uchukuzi, Dkt Harrison Mwakyembe akionyesha kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) picha ya dawa za kulevya zilizokamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere hivi karibuni.

*WAPIGWA MARUFUKU KUKANYAGA UWANJA WA NDEGE
HATIMAYE maofisa usalama wanne katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wamepewa barua zao za kuachishwa kazi.

Hatua hiyo imekuja baada ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyemba kuagiza waachishwe kazi mara moja kutokana na kutuhumiwa kuhusika kwao katika kusaidia watu kusafirisha dawa za kulevya kilo 180.

Maofisa hao kwa mujibu wa Dk. Mwakyembe ni Yusufu Issa, Jackson Manyonyi, Juliana Thadei na Mohamed Kalungwana. Baada ya kukabidhiwa barua zao wamepigwa marufuku wasionekane katika uwanja huo.

Hata hivyo, maofisa hao wataendelea kupata mishahara yao kama kawaida hadi kesi yao ambayo inayoshughulikiwa na Jeshi la Polisi itakapofikishwa mahakamani na kutolewa hukumu.

Kauli ya maofisa hao kukabidhiwa barua zao ilitolewa Dar es Salaam jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Ramadhan Maleta. “Sisi upande wetu tumewaambia waandike charge sheet mambo mengine tumewachia polisi wenyewe,” alisema Maleta.

Katika hatua nyingine, mmoja wa walinzi katika uwanja huo alidokeza gazeti hili kuwa mashine mpya zimefungwa kwa ajili ya kuongeza ulinzi eneo hilo.

Pia alisema mbwa wa ukaguzi wataendelea kuwepo uwanjani hapo kama kawaida ili kudhibiti wanaoingiza au kusafirisha dawa hizo. Alisema mbwa hao hawajaondolewa kama inavyovumishwa mitaani.

Ulinzi umeimarishwa katika uwanja huo ambapo kuna sehemu ambazo watu wanalazimika kuvua viatu na kupitishwa katika mashine maalumu za kukaguliwa ili kuhakikisha hakuna anayepita eneo hilo na kitu kisichotakiwa.

Pia kitengo cha kusindikiza au kupokea watu mashuhuri katika uwanja huo pamefungwa mashine maalumu.

Pamoja na mambo mengine, Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) lina mpango wa kuingia ubia na Kampuni ya Alhayat Investment and Development L.L.C The Sultanate of Oman ili kuleta ndege nane kwa safari za ndani na nje.

Katika suala hilo, Maleta alisema mipango hiyo ipo mbioni na wahusika wakuu wa jambo hilo ni Wizara ya Uchukuzi.

Maleta alikuwa na wageni wa kampuni hiyo kutoka Oman ambao walikuja nchini kwa ajili ya kukagua viwanja vya ndege kabla hawajasaini mkataba rasmi wa kujikita katika sekta hiyo. “Kwa kuanzia kampuni hiyo ina mpango wa kuleta ndege nane kubwa zitakazorushwa kwa nembo ya Air Tanzania,” alisema Maleta.

Alisita kutaja aina ya ndege pamoja na gharama zake kutokana na suala hilo kushughulikiwa zaidi na wizara husika.

CHANZO: GAZETI LA JAMBO LEO AGOSTI 27, 2013

No comments: