ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 20, 2013

HII NDIO SABABU YA WANAMICHEZO KUBEBA NA KUUZA MADAWA YA KUELVYA

KATIBU Mkuu wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui amesema kitendo cha wanamichezo wengi kutojiandaa na maisha baada ya kung’ara katika michezo ndicho chanzo cha wanamichezo wengi kujiingiza katika biashara ya dawa za kulevya.
Hivi karibuni wanamichezo Joseph Kaniki (mwanasoka) na Mkwanda Matumla (bondia) walikamatwa wakituhumiwa kukutwa na dawa za kulevya nchini Ethiopia wakiwa njiani kwenda Sweden.
Mpaka sasa watuhumiwa hao wanasota katika mahabusu za nchi hiyo huku wakisikiliza kesi yao ambayo inaweza kusikilizwa na kama wakitiwa hatiani wanaweza kufungwa Ethiopia kwa kuwa nchi hiyo haina makubaliano ya kubadilishana wafungwa na Tanzania.
Nyambui aliuambia mtandao huu kwamba, wanamichezo wengi wanaingia katika michezo bila kujiandaa na maisha ya uanamichezo na hata wanapopata fedha huwa hawawezi kuziingiza katika mfumo wa kujizalisha.
“Wanamichezo wengi hawana usimamizi wa mambo ya kiuchumi, tazama wanapata fedha nyingi lakini wakitoka nje ya mchezo huo maisha yao yanakuwa magumu na yenye kusikitisha ndipo hapo wanapoamua kujiingiza katika matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
“Kitu kingine kinachowafanya wanamichezo kuingia katika biashara hii ni tamaa za kutaka kutajirika bila kufuata taratibu husika. Haraka hii ya maisha ni tatizo kwa vijana wetu na ndiyo maana kila kukicha wanakamatwa,” alisema Nyambui ambaye wakati wake alikuwa mkimbiaji maarufu.
Kabla ya Kaniki ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars kukamatwa na dawa za kulevya huko Ethiopia, msanii wa filamu na ‘video queen’, Agnes Gerald ‘Masogange’ naye alikamatwa hivi karibuni huko Afrika Kusini akiwa na shehena ya dawa za kulevya na raia mwingine wa Tanzania.
Wimbi la biashara ya dawa za kulevya limeshamiri nchini Tanzania miongoni mwa wanamichezo kutokana na urahisi wa safari zao kwenda nje ya nchi na hata sasa wamekuwa wakifanyiwa upekuzi wa hali ya juu kila wanapotaka kuingia katika nchi nyingine.
Tayari serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na serikali ya Uingereza imeshaweka mitambo maalum ya kung’amua madawa hayo katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

No comments: