Rais Dkt. Jakaya Kikwete
Mabalozi wa Heshima toka kushoto ni Ahmedi Issa, Kjell Bergh na Suzanne Alyce Terrell
Mabalozi wa Heshima kutoka kusho ni Charles Gray, Cemil Teber, Robert Samuel Shumake na Dallas Browne
Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa kazi kubwa ya mabalozi wa Tanzania katika nchi za nje ni kutetea maslahi ya nchi yao na kuijengea marafiki.
Aidha, alisema kuwa ni wajibu wa kila Balozi wa Tanzania popote alipo kuonyesha sura nzuri ya Tanzania, kuvutia wawekezaji katika maeneo mbali na kutangaza nafasi nyingi za uwekezaji nchini.
Alisema Tanzania ina utajiri mkubwa wa utalii duniani na ni kazi ya mabalozi hao kuutangaza hasa Marekani ambayo kwa sasa ndiyo nchi inayoongoza kwa kuleta watalii wengi nchini Tanzania.
Alitoa maelekezo hayo kwa mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchi za nje wakati alipozungumza nao katika halfa ya kutiwa saini kwa makubaliano kati ya Balozi wa Tanzania katika Marekani, Liberata Mulamula na mabalozi wa heshima saba ambao wataiwakilisha Tanzania katika sehemu mbali mbali, Marekani.
Katika halfa hiyo iliyofanyika Tanzania House, kwenye Ubalozi wa Tanzania mjini Washington,D.C., Rais Kikwete aliwaambia mabalozi hao wa heshima: “Kazi yenu kubwa ni kulinda na kutetea maslahi na heshima ya Tanzania katika maeneo yetu ya mamlaka. Jengeni jina la Tanzania katika maeneo yetu.
Itengenezee nchi yetu marafiki wa kila aina na vutieni wawekezaji kutoka kwenye maeneo yenu waje kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.”
“Tunataka kuwaeleza watu wenye fedha na rasilimali za kuwekeza nchi za nje kuwa Tanzania ni nchi nzuri kupeleka mitaji yao na kuwa mitaji yao itakuwa salama.Tangazeni utajiri mkubwa wa utalii Tanzania. Tuna imani nanyi kuwa mtaifanya kazi hiyo vizuri na kwa mafanikio. Natawakieni kila la heri.”
Mabalozi hao wa heshima ni Ahmed Nassoro Issa Al Qasimi ambaye atawakilisha Tanzania katika Jimbo la California, Cemil Teber (New Mexico), Robert Shumake (Michigan) na Charles Gray (Philadelphia, Pennsylvania).
Wengine ni Suzanne Terrell (New Orleans, Louisiana), Dk. Dallas Browne (Illinois) na Kjell Bergh (Minneapolis, Minnesota).
Mabalozi wa heshima wa Tanzania katika sehemu mbali mbali huteuliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa ushauri na mapendekezo ya balozi mbali mbali za Tanzania duniani.
No comments:
Post a Comment