Hii ni moja kati ya taarifa ambazo nimeona umuhimu wake na kuipa nafasi kama ilikupita mtu wangu, ni kuhusu habari iliyoandikwa na gazeti la Habari leo kwamba kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation ya Beijing, imesema iko tayari kuja Tanzania kuijenga upya reli ya kati , ambayo kwa sasa imechakaa na inashindwa kuhimili shehena kubwa ya mizigo kuwa ya kisasa.
Injini na Mabehewa ya reli hiyo kongwe Tanzania vimechakaa wakati ni tegemeo kubwa kwa wakazi wengi wa baadhi ya mikoa ya Tanzania na pia ni sehemu nyingine ya kuukuza uchumi wa nchi.
Rais wa kampuni hii ya China amemwambia Waziri mkuu kwamba tayari wameanza mazungumzo na Wizara ya uchukuzi na kama watakubaliana, wako tayari kuja Tanzania na kuijenga hii reli ikiwa ni kampuni ambayo pia iliijenga reli ya Tazara baada ya Hayati Mwalimu Nyerere kuiomba serikali ya China.
Amesema pia ujenzi wa kiwango hicho kinachotakiwa ni gharama na hawawezi kufumua reli yote kutoka Dar es salaam mpaka Kigoma na Mwanza ila watafanya kwa awamu ili usafirishaji wa abiria na mizigo uendelee wakati huohuo ujenzi ukiendelea.
Waziri mkuu Mizengo Pinda alisema kuna kampuni kadhaa kutoka mataifa mbalimbali ambazo zimeonyesha nia ya kujenga reli hiyo lakini waliona wawasiliane na China kwanza ambayo kuna historia ya ushirikiano mzuri.
Kutokana na uchakavu wa hii reli ya kati, kiwango cha kusafirisha mizigo ya ndani na nje ya nchi kimeshuka ambapo siku za safari za treni ya abiria zimeshuka kutoka safari saba kwa wiki mpaka safari mbili kati ya Dar es salaam, Mwanza na Kigoma.
No comments:
Post a Comment