ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 25, 2013

Maalim Seif: Matusi hayatavunja Serikali ya umoja

  Asema atagombea ukatibu mkuu
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar,Maalim Seif Sharif Hamad

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kuna watu wachache ambao hutumia lugha za matusi wakiwa katika majukwaa ya kisiasa kwa kuwakashifu viongozi, lakini matusi yao hayawezi kuivunja serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari hapa jana Maalim Seif alisema licha ya matusi na kashfa zinazotolewa na wanasiasa dhidi yake, lakini bado anajivunia hali ya utulivu na amani iliyopo katika serikali ya umoja.

Alisema kingine anachojivunia katika serikali hiyo ni nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma kulinganisha na miaka mingi iliyopita kabla ya serikali ya umoja wa kitaifa kwa kuwa kilio kikubwa cha wafanyakazi kilikuwa ni kiwango kidogo cha mishahara.

Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), alisema mchakato wa kuelekea katika chaguzi ndani ya chama chake umeshaanza na mwezi ujao utaanza chaguzi wa ngazi za chini huku wa ngazi ya taifa ukifanyika mwakani.

Alisema nia bado anayo ya kugombe nafasi hiyo ya ukatibu mkuu pamoja na urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

“kwa nini nisigombee ukatibu na uraisi wakati uwezo ninao, endapo nitapata ridhaa ya wanachama wangu nitagombea panapo majaaliwa na kustaafu kwangu katika siasa mpaka nitakapoishiwa na nguvu au sheria ikinikataza,” alisema.

Akizungumzia kuhusiana na matumizi mabaya alisema vitendo vya kihalifu ikiwemo matumizi mabaya ya tindi kali Zanzibar ni mageni na kuvitaka vyombo vya dola kuhakikisha vinadhibiti vitendo hivyo.

Akizungumzia utendaji wa kazi katika ofisi yake, alisema bado kuna changamoto mbalimbali ikiwamo kuongezeka kwa kiwango cha maradhi ya ukimwi na kwamba tangu mwaka 2012 hadi 2013 maambukizi ya virusi vya ukimwi yamepanda kwa alisilimia 1.0 kutoka asilimia 0.6.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

shame on you! viongozi wa kiafrika kug'ang'ania madaraka tu. tujifunze kwa wenzetu kina Al Gore na wengineo imeshindikana unawapisha wengine, hususan vijana. basi tu kupenda madaraka na kutajwa tajwa sana hamna kimoja mnachokizalisha, hususan wewe! ng'atuka tena wapishe vijana nao wagombee!!!