ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, October 5, 2013

MCHAKATO KATIBA MPYA:JK: Hoja ya Z`bar irudishwe bungeni

*Apinga maandamano ya wapinzani
  *Awakaribisha Ikulu kwa majadiliano
  *Amshushua Tundu Lissu, asema mzushi
  *Kuvunjwa Tume ya Warioba afafanua
Rais Jakaya Kikwete, amekata mzizi wa fitina katika suala la mchakato wa katiba kwa kushauri ile hoja ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria  na Utawala kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau wa Zanzibar, ilirudishwe Bungeni ili wabunge walizungumze na kulifanyia uamuzi muafaka.
Aidha, amevitaka vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi kuachana na mipango ya maandamano na kufanya ghasia kama dhamira yetu ni kutaka kupata Katiba mpya kwa mujibu wa Katiba na Sheria.
Kauli hiyo ya Rais imekuja kukiwa kumebakia siku tano zilizotangazwa na viongozi wakuu wa vyama hivyo kwa ajili ya kufanya maandamano nchi nzima kupinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa wakati wa mkutano wa 12 wa Bunge mwezi uliopita.

Rais Kikwete alisema aliambiwa kuwa kuliwepo madai ya Zanzibar kutokushirikishwa ipasavyo katika kutoa maoni kwenye muswada huo.
“Nimeeleza kwa kiasi gani Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeshirikishwa na kutoa maoni yake yaliyojumuishwa katika Muswada.  Hivyo basi napata tabu kuyaelewa madai kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikushirikishwa msingi wake nini!  Labda kuna kitu sikuambiwa,”alisema
Hoja kwamba Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau wa Zanzibar, aliambiwa kuwa kanuni za Bunge hazina sharti hilo, hivyo kamati haistahili kulaumiwa.
Rais Kikwete alishauri kama ni hivyo, suala hilo lirudishwe Bungeni ili wabunge walizungumze na kulifanyia uamuzi muafaka, vinginevyo watu wataendelea kulaumiana isivyostahili. 

Alisema, “kuligeuza jambo hili kuwa ni suala la kukataa Muswada au kususia vikao vya Bunge au kufanya maandamano sidhani kama ni sawa”. 

MAANDAMANO YA WAPINZANI
Rais Kikwete alisema kuandamana nchi nzima au kuchukua hatua za kutotii sheria kama Mwenyekiti wa Chadema, freeman Mbowe anavyotaka hakutaleta mabadiliko wanayoyataka katika sheria hii.
“Kuna msemo wa wahenga kuwa “historia hujirudia”.  Naomba hekima ziwaongoze viongozi wa Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi na zituongoze sote kutumia utaratibu tulioutumia mwaka 2012,”alisema.
Alisema kuwa mwaka jana, kulipotokea mazingira ya kutoelewana katika suala la katiba, pande zote zilikaa pamoja na kuzungumzia hoja moja baada ya nyingine na kukubaliana nini kifanyike na  baada ya kuridhiana hatua zipasavyo za kisheria na kanuni zilichukuliwa na kumaliza mzozo.

Alisema kufanya kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo huu na badala yake tutaliingiza taifa kwenye matatizo yasiyokuwa ya lazima na kwamba tukikataa kufanya hayo Watanzania wanayo kila sababu ya kuhoji dhamira zetu na kutilia shaka nia zetu.
 “Watanzania watakuwa na haki ya kuuliza nia ni hii yetu sote ya kupata Katiba Mpya kwa kutumia njia za kikatiba na kisheria au tuna dhamira nyingine iliyojifisha?, alihoji Rais Kikwete.

Alisema viongozi wa vyama hivyo watumie njia halali zinazotambulika kikatiba na kisheria kujenga hoja za kufanya marekebisho wanayoyaona wao yanafaa kuboresha  Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kufanya hivyo kutasaidia  kujenga Taifa badala ya kubomoa.
Aliongeza kuwa baadhi ya hoja zilizotolewa na Kambi ya Upinzani zimemsikitisha sana na madai na tuhuma za uongo kwamba katika uteuzi wa Tume ya Katiba hakuheshimu mapendekezo ya Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), Baraza la Kikristo (CCT) na walemavu.
AMSHUSHUA LISSU
“Siyo tu kauli hiyo ya Tundu Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki) ni uzushi na uongo mtupu bali pia ni ya unafiki, fitina na uzandiki wa hali ya juu.  Nasema hivyo kwa sababu, sipendi kuamini kuwa mbunge amesema yale kwa kutokufahamu ukweli au kwa bahati mbaya.”
Rais alisema mbunge huyo aliamua kupotosha ukweli ili pengine isaidie kujenga hoja yake ya kutaka Rais asiteue wajumbe 166 wa Bunge Maalum la Katiba.
Alisema hashabikii jukumu hilo, lakini kwa kutimiza wajibu na maslahi ya taifa akiagizwa na sheria za nchi atalifanya.

Akilinganisha na uteuzi wa wajumbe 30 wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Rais Kikwete alisema haikuwa rahisi hata kidogo na hii ya uteuzi wa watu 166 watakaoingia katika Bunge Maalum la Katiba itakuwa ngumu zaidi.
Alieleza kuwa licha ya kutakiwa kuteua watu 30 wajumbe walioteuliwa na wadau walikuwa zaidi ya 500  akieleza kuwa kwa Zanzibar zilikuwa asasi zaidi ya  60  wakati Bara  zilikuwa asasi zaidi ya 170 zikiwa na waombaji zaidi ya 500.
Alisema uteuzi ulihakikisha kuwa wawakilishi wa  vyama vya siasa vyenye wabunge na wajumbe Baraza la Wawakilishi wanapatikana,  mashirika ya dini kubwa ya  TEC, CCT na Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata)  pia wanakuwepo.
Alisema kwa upande mwingine Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ilipendekeza uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum ufanywe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na kuafikiana na Rais wa Zanzibar.  Pia SMZ ilishauri kwamba kama Bunge Maalum litashindwa kufikia maamuzi ndani ya siku 70 zilizopendekezwa, liongezewa muda hadi kufikia siku 90.
“Ndiyo maana naiona mantiki ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akishirikiana na Rais wa Zanzibar wa kuwateua wajumbe wa Bunge Maalum.”
Alisema dhana kuwa kila kikundi kiteue chenyewe watu ingefaa kama kungekuwepo na nafasi za kutosha kwa  kila kundi nchini.  Rais alisema pendekezo hilo haliwezekani, labda kuwe na Bunge Maalum lisilokuwa na ukomo wa wajumbe.
MUSWADA BUNGENI
Rais Kikwete aliwaambia wapinzani kuwa  mapendekezo yao kuhusu marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba hayawezi kuzungumzwa nje ya Bunge.
Alisema maoni yao yangezungumzika na hata baadhi yangekubalika kama wasingetoka nje wakati wa mjadala huo uliozua tafrani bungeni mwezi uliopita.
Aliongeza kuwa baada ya wapinzani kupoteza fursa halali kutoa mapendekezo yao na sasa kutaka kupata ufumbuzi nje ya Bunge ni jambo lisilowezekana.
“ Haya ni masuala yanayohusu Bunge ambayo hujadiliwa na kuamuliwa Bungeni na si vinginevyo,”alisema.
Aliwaambia kuwa kwa vile hawakuwepo ndani ya mjadala na  hakuna aliyewawakilisha hivyo hakuna kinachoweza kufanyika.

WAJUMBE BUNGE LA KATIBA 
Rais Kikwete alisema kulikuwa na hoja ya kutaka idadi ya wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka Tanzania Bara na Zanzibar iwe sawa kama ilivyo kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema sababu ya idadi ya wajumbe wa tume kuwa sawa inatokana na utaratibu wao wa kufikia uamuzi, kwani ni kwa maelewano ya wote (consensus) na siyo kwa kupiga kura.
Alifafanua kuwa, Bunge maalum la Katiba lina sharti la kufanya uamuzi kwa theluthi mbili ya kura za kila upande kukubali, bila ya hivyo hakuna uamuzi, hivyo katika bunge hilo nguvu si uwingi wa kura ambazo upande fulani unaweza kupata bali ni ulinganifu sawa wa kura za kila upande peke yake.

“Zanzibar ina majimbo 50 ya uchaguzi na Tanzania Bara ina majimbo 189, hivyo ukiamua kwa wingi kila wakati Wazanzibari watashindwa.  Lakini, hapajakuwepo madai ya Zanzibar nao kutaka kuwa na idadi sawa ya majimbo kama Bara au kupunguza majimbo ya Bara yawe sawa na ya Zanzibar kwa sababu wingi si hoja,”alisema.

Alisema msingi unaotumika ni kutoa nguvu sawa za uamuzi kwa kila upande wa Muungano wakati wa kuamua masuala ya Katiba, hakuna mdogo wa kumezwa na mkubwa, wote wako sawa.

 KUVUNJWA TUME YA WARIOBA

Alisema kumekuwepo na madai ya wapinzani kuhusu suala la uhai wa Tume ya Katiba ambao wanataka usiishe wanapokabidhi rasimu ya pili kwa Bunge Maalum bali waendelee kuwepo mpaka mwisho wa mchakato.

Aliongeza kuwa  suala la ukomo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba siyo mapendekezo ya Serikali wala ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala bali lilitokana na pendekezo la Mbunge katika Bunge wakati wa kupitia vifungu na kuungwa mkono na wabunge wengi.
 “Nami naiona hoja ya wajumbe wa tume kuwa na wajibu wakati wa Bunge Maalum hasa wa kusaidia kufafanua mapendekezo ya Tume.  Je ushiriki huo uwe vipi? Je ni Wajumbe wote au baadhi yao ni jambo linaloweza kujadiliwa,”alisema.
Jumanne wiki hii, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, akizungumzia suala la ukomo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema suala hilo lilipendekezwa na Mbunge wa Kisarawe, Suleman Jaffer.
Chikawe alisema mbunge huyo alipendekeza kuwa tume hiyo itakapowasilisha ripoti yake ivunjwe sababu haitakuwa na kazi na kama Bunge la Katiba litahitaji ufafanuzi wowote ataitwa Mwenyekiti wa Tume hiyo kutoa ufafanuzi.


MUSWADA KUHODHIWA NA CCM

Chikawe alisema kama unachukua Bunge kwa misingi ya chama siyo sawa lakini bunge halikukutana na kupitisha muswada huo kwa misingi hiyo.

“Kitu cha msingi ni kwamba kolamu ya wabunge ilitimia wakati wa kupitisha muswada huo, hivyo sheria haikuvunjwa,sikuona sababu ya wabunge wa upinzani kutoka Bungeni,”alisema.

Alisema tabia ya wabunge wa vyama vya upinzani kutoka bungeni na kukimbilia mitaani na kwenda kuwapotosha wananchi siyo sahihi.

KUMTISHA RAIS ASIPOSAINI MUSWADA

Alisema yeye (Chikawe) hana ubavu wa kumtisha Rais kwani Rais ana hiari ya kuusaini muswada huo au kutousaini.
“Ni imani yangu kwamba Rais atasaini muswadam atatumia ustaarabu wake,”alisema Chikawe.

Juzi viongoz wa Kamati ya Ufundi ya Ushirikiano wa Vyama vya CUF,Chadema na NCCR-Mageuzi walisema maandalizi kwa ajili ya maandamano hayo yatakayofanyika Oktoba 10 mwaka huu, yameanza kufanyika baada ya kuwasiliana na viongozi wa mikoa yote.

SHAMBULIZI LA KIGAIDI NAIROBI

Rais Kikwete alisema tangu shambulio lililotokea mwaka 1998, Serikali imekuwa inajenga uwezo wa vyombo vya ulinzi na usalama kupambana na ugaidi katika nyanja mbalimbali.

”Tunaendelea kujiimarisha bila kusita siku hadi siku.  JWTZ, Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa ajili hiyo.  Juhudi zetu hizo ndizo zinazotufanya tuwe salama hadi sasa,”alisema.

Rais Kikwete alisema baada ya tukio la Kenya, vyombo vya ulinzi na usalama vimeimarisha mikakati yao maradufu na kwamba pamoja na kujizatiti kwetu huko hatuwezi kusema kuwa tukio la kigaidi halitaweza kutokea nchini.

Alisema uhakika huo haupo kwani hata mataifa makubwa na tajiri yameshambuliwa, hivyo jambo la muhimu ni kuendelea kuchukua tahadhari na wananchi kusaidia ili  vyombo vya ulinzi na usalama  vifanikiwe zaidi. 
 
Aliongeza kuwa watu wote wenye shughuli zinazokusanya watu wengi kama vile maduka, maofisi, mahoteli, migahawa waweke kamera za ulinzi nje na ndani ya maeneo yao na kuweka vifaa vya upekuzi (metal detectors and x-rays). 

Rais Kikwete alisema wananchi waendelee kufanya shughuli zao bila ya hofu ingawaje wasiache kuwa makini na kuchukua tahadhari, na kwamba maafisa husika wa vyombo vya ulinzi na usalama wataendelea kuelimisha umma kuhusu hatua mbalimbali za tahadhari za kuchukua. 
*Gaudensia Mngumi na Thobias Mwanakatwe
 
CHANZO: NIPASHE

11 comments:

Anonymous said...

Inna lillahi wa inna ilayhi raji’un (إِنَّا لِلّهِ وَإِنَّـا إِلَيْهِ رَاجِعونَ) Leo Zanzibar inatetewa na wasio Wazanzibar haliyakuwa viongozi wetu wa Zanzibar wao ndio wenye kuiteketeza Zanzibar kutokana na njaa zao wasio ziweza.

Hufanya hivi eti kuchunga unga wao usimwagike na ndio huisaliti Zanzibar na kila moja mdomo juu kwa kuwadifend wale wenye kuihujumu Zanzibar kwa kuwakingia kifua na kuwasaidia kazi.

Hii Katiba Tanzania Bara ilikuwa ikushanye maoni yake na Zanzibar ikushanye maoni yake halafu ndio yafanyiwe kazi, hii ni mapendekezo ya Mh Jussa alio yapeleka kwa Spika wa Zanzibar Mzee mwenye kuangalia Dunia zaidi kuliko Ahera.

Mswada wa Mh Jussa haukufika hata kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kujadili, Kificho ali uficha na hali ndio hii leo Wazanzibaru kutiwa kwenye kundi la Watanganyika million 35.

Anonymous said...

Rais anadanganywa na hao wanaoitwa washauri wake. Nimeisoma hotuba yake, karibu kila alilosema anasema ameambiwa au ameelezwa! Hayo mambo yanayolalamikiwa yapo wazi...hiyo tume ya bunge haikwenda ZNZ, waziri anasema kwenda au kutokwenda ni hisani tu, kwa hiyo anaona ni haki kukusanya maoni ya upande moja? Vipi ingekuwa wanakusanya maoni ya ZNZ pekee, je wasingelalamika watu wa upande wa
bara? Au mkuki kwa nguruwe? Au kuna lililojificha? Tendeni haki ninyi wabunge wa CCM, kutetea serikali hata pale isipotenda haki siyo sahihi. Hotuba ya rais inashangaza inaonekana imeandikwa na wasio na weledi wa kutosha imejaa "eti" au 'ati', imekuwa kama mipasho ya uswahilini. Ninashangaa rais kuhangaika na kuwataja wabunge wa upinzani akitegemea huruma ya wananchi badala yake wengi tunaona haikuwa sahihi kwa kiongozi wa nchi ku-crash maoni na fikra ambazo waliozitoa wanaona ni dhahiri na zenye ukweli, ningeona ni vyema kama rais alitaka kupinga angepinga kwa hoja wala si kwa kushambulia kwa mipasho. Suala la Rwanda siyo jukumu la blog wala magazeti kuimarisha uhusiano ni suala la serikali na maofisa wake, blunder alifanya rais mwenyewe, angenyamaza au kumweleza yeye Kagame mwenyewe mkutanoni yasingetokea yaliyotokea, lakini kwa sababu viongozi wetu wanalewa madaraka na wanajiona wao kama miungu-watu, matatizo yasiyo ya muhimu yanatokea. Sasa bandari inakimbiwa kutokana na mlundikano wa matatizo lakini badala ya kutatua rais anakimbia kimbia huko duniani, analofanya halieleweki na inaonekana hajali hata kama bandari zetu zitakosa biashara.

Anonymous said...

Kama wasingeamdamana, hiyo rasimu ungeirudisha bungeni? Wazanzibari wasiposhirikishwa kuhusu swala la muungano kikatiba, basi muungano utaendelea kuwepo iwapo CCM itandelea kushinda Z'bar. Iwapo akichaguliwa rais kutoka nje ya CCM na akawaunganisha wa Z'bari kujitoa katika muungano, utapeleka jeshi kwenda kukabiliana na watu wanaodai nchi yao? Tuwe makini sana tunapojadili muungano.

Anonymous said...

Muheshimiwa achana na wazanzibari waendeleze masiasa yao ya chuki za upemba na uunguja. Ukafu na usisim. Weye endelea kujenga na kuendeleza taifa la Tanganyika aka Tanzania.

Anonymous said...

ndio achana na sisi na chuki hizo si ndo mmejipandikiza nyinyi tulikuwa hatuko hivyo mmekuja kujazana huku na kupandikiza chuki zenu na uonevu wenu sasa tunasema tunataka kupumua si wajinga tena hatutaki kuvaa koti la viraka wandawazimu ndo wanavaa koti la viraka tupeni nchi yetu muona kama tutakuja kukuombeni kitu kwa nini mnashikilia nchi ambaya watu wake hawataki kwa nini mnataka kuungana na sisi na hatutaki chuki zote mmezileta nyinyi mnafikiri hatujui au wajinga sisi.

tunataka nchi yetu tafrani tumechoka hatutaki rasimu ya katiba hii waa ile tunataka nchi yetu tafrani tumechoka na ukoloni wenu. zanzibar ni nchi si mkoa kama mwanza tabora etc tunataka nchi yetu na tuweni lakini kuna siku tatapata nchi yetu innshallah amin

Anonymous said...

ccm inajua wazi hawezi kuishinda zanzibar ila kama kushinda inakuwa ni wizi tu wa kura au kutaawala kimabavu na wakoloni wao bara kuja kuwapa ushindi ndo wanachojua cha kufanya other than that ccm haina kushinda huku asikudanganye mtu vitimba kwiri tu vinavyo chunga tonge za riski zao ndo peke wapo ccm kama mnajidanyanya watanganyika endeleeni kujidanganya hakuna mtu anayeipenda ccm labda kama yupo kwa manufaa yake ndo ataipenda mchana ccm usiku anakuwa na chama chake mpo kavirondo waheed.

Anonymous said...

kwa taarifa yako mdau wa mwisho wewe ndo mwenye chuki na walio kukuzaa hapa visiwani tulikuwa tunaishi vizuri sana na wapemba na wa cuf na wakiristo mmekuja nyinyi imekuwa kiroja balaa tupu na tafrani zenu kwa vile mnajua mnachokitaka huku kwetu halafu mnasingizia mnatubeba tubwageni basi na muone kama tuta kufa tukiwa na nchi yetu huru ndo maaana hamtaki kupaachia na visa na vituko vya kumwagiana tindikali mnaviaazisha nyinyi huko na kutuletea huku kwa sababu tunataka na kudai nchi yetu yenye mmamlaka kamili kwa nini mnatulazimisha tuungane na nyinyi katika karne hii ya leo muungano huu tu peke ndo wenye vituko duniani kote hakuna muungano kama huu wa balaa na biizni lillahi tutashinda na kuikomboa nchi yetu allah ma ammin.

nyinyi si mungu hakuwa firauni na ujeuri wake wote na ubabe akaangamia mtakuwa nyinyi,nyinyi si mungu

Anonymous said...

Mheshimiwa Rais J.K. usipokuwa makini na hawa watendaji wako basi umeliingiza taifa kwenye dimbwi la damu nzito. Sijui unaelewa ni jinsi gani ulivyo na washauri waongo kwenye serikali yako!. Hili swala la katiba lisifanyiwe dhihaka kamwe. Wazanzibari wapewe haki yao ya kupitia huo mswada. Watanzania chama tawala kimehodhi mkataba mzima na hakuna mnaloona upinzani una haki ya kudai, Isitoshe sijui kama tunajali taifa au maslahi ya wachache. Wakati watanzania wanalimana makonde wewe utakuwa umetulia huko kwenye kiota chako ukitizama TV. Tusaidiane jamani. Asante.

Anonymous said...

Ndugu Rais J.Kikwete. Wewe ni Raisi wa wote sio wa CCM pekee, Hivyo ni vyema ukatizama mbele na ukae na washauri wako kwani wanayokuletea mezani ni uongo na uchochezi mtupu na unaonekana kuwakubali. Kwani hao wapinzania wakiandamana wanavunja sheria?, Si muwaache waandamane msikie sauti yao na mrudi upande wenu muone makosa yenu. Hamuwezi kujikosoa wenyewe kwani wapo wenye uchu wa madaraka na wanaona wakikosa kuwepo humo ndani basi ndo kiama chao!.

Anonymous said...

chuki mmeanza kutuletea nyinyi watanganyika mlipokuja huku tulikuwa hatuna chuki hizo na ndo maana tumeungana na ccm na kaafu kuwa kitu kimmoja kuanda serikali ya msetoo mpoo acheni uongo wenu na fitna zeneu mtatuona hivi hivi tuna outshine always

Anonymous said...

mtoa maoni wa tano mungu akusaidie, inaonekana kichwa chako kina matatizo