
ALI zenu mabibi na mabwana? Nasra miye nimetua tena kama dege la kivita ili kukupeni elimu ya bure.
Siwezi kuwa mchoyo kwa vile kufanikiwa kwenu ndiyo furaha yangu, binafsi huwa naumia sana pale ninapomuona mwanamke mwenzangu anakosa furaha katika ndoa kwa jambo ninaloweza kumsaidia ili akastarehe na mumewe.
Juzi nilifuatwa na mwari wangu mmoja huku akilia, eti mwanamke wa nyumba ya jirani amemchukulia mumewe.
Baada ya kuchukuliwa mume mwari wangu anasema mumewe amekuwa haoni wala hasikii kwa huyo kimada na imefikia hatua ya kudharauliwa na kuonekana si mali kitu.
Baada ya kumsikiliza kwa umakini mkubwa mwari wangu, akaniomba nimpe msaada wa kumrudisha mumewe.
Nikakumbuka kitu kimoja muhimu sana kwa wanawake walioolewa ambao wamekuwa wakiwapa nafasi wale wa pembeni kujilinia asali bila hofu na mwisho kumiliki mzinga mzima.
Kwa vile naheshimu ndoa, leo nataka niwaelezee sababu za nyumba ndogo kuwazidi kete wenye ndoa.
Najua siri hii itawachukiza wengi hasa wenye tabia ya kukwakupua mali za watu na kujimilikisha waume hao kama wa kwao, tena wako radhi kuona familia za wenzao zikiteketea huku wao wakipata neema kutokana na kuchuna bila huruma.
Wanawake wa aina hii wana tabia ya kula kwa mikono miwili bila kunawa, siwapendi na sitaki hata kuwasikia kutokana na tabia zao mbaya.
Kabla sijawapa siri za hao vishankupe wanaopenda kuchukua waume za watu kiasi cha kutuona siye tulioolewa si mali kitu, kwanza nataka niwaulize wale walioolewa maswali haya na kila mmoja ajibu kwa nafsi yake:
Swali la kwanza: Nani anayefanya usafi wa mwili wa mume wako, kama vile kumkata kucha, kumnyoa nywele za pembe ya chaki na mambo mengine?
Swali la pili: Nani anayemfanyia masaji mumeo?
Nawaona wengine macho yamewatoka pima kwa swali hilo la masaji, wengi hawajui kama mume anatakiwa kufanyiwa masaji.
Wengine hata masaji yenyewe hawaijui. Jamani ni kumkanda mwili mumeo kwa mafuta huku ukimnyoosha kiungo kimoja baada ya kingine akiwa mweupe kwenye sita kwa sita yenu ni jambo la kawaida, umenipata?
Eti mwari wangu, mara ya mwisho kupanda kitandani na kitambaa kabla ya chakula cha usiku ilikuwa lini?
Nina imani kila mmoja atajibu lake na wengine watageuka kuwa mabubu kwa kushindwa kujibu hata moja kati ya haya.
Basi huu ndiyo udhaifu unaozifanya nyumba ndogo kupata nguvu na kuwatawala waume zenu.
Sasa hujui lolote kati ya hayo niliyoyaeleza hapo juu, utaweza kumtuliza mumeo ndani?
Siku zote adui hawezi kukushinda kama hajui udhaifu wako, mbaya zaidi udhaifu wako anaujua pale anapokutana na mumeo.
Akimwangalia mumeo vidoleni anakutana na kucha zimechomoza kama kunguru wa Unguja, nywele zimemjaa kila kona, atashangaa, atamtia kwenye kumi na nane zake na wewe unakuwa ndiyo basi tena.
Mume ananogewa kwa majambozi, anakatwa kucha huku akikandwa na kupakwa mafuta, anasafishwa hadi kwenye kibendera cha kona, una nini tena mwari wangu?
Mali zako zinashikwa wakati wewe mwenyewe hujui hata ramani yake ikoje, niambie ni lini uliipiga deki ikulu ya mumeo?
Mwizi wako anapigilia msumari wa mwisho na kumzibua masikio mumeo, kisha mwanaume anagundua tofauti yako na ile ya nyumba ya pembeni, ikifikia hatua hiyo ujue umekwisha!
Unashangaa mume anakuwa na hasira hata kwa jambo dogo tu, hataki kula chakula chako na akirudi hata kukugusa hahitaji. Haya ni kati ya makosa mengi ambayo wanawake walioko ndani ya ndoa wanayafanya, wengine wanayafanya bila ya kujua na wengine hawayajui kabisa na hawajui kama hawajui, eti wanalingia shepu zao.
Mwari wangu utaendelea kusimangwa kutokana na udhaifu wako, unaitwa mchafu kwa kuwa mumeo hajasafishwa, kila kona amejaa manyoya kama kondooo.
Haya yote yanatokana na kufanya mambo kwa mazoea, kisha unalia kumbe matatizo umeyasababisha wenyewe.
Tuache tabia za kuwasubiri uwanjani, tunatakiwa kuwasubiri waume zetu wakitoka kazini ili tuingie nao bafuni kwa ajili ya kuoga pamoja.
Huko ndiko tutajua kama ikulu zao zina majani au la, huko ndiko tutaanzisha kampeni ya kulima mashamba yao na kukata nyasi na magugu yote.
Siku nyingine ukimuona mumeo amechoka mwambie unataka kumkanda mwili ili kuongeza thamani ya mapenzi yako kwake.
Waswahili wanasema zubaa uzikwe, basi kama unataka kuendelea kuchekwa wee mwache mumeo awe mchafu, utazikwa ukiwa hai.
Ataenda kufanyiwa usafi na nyumba ya pembeni, akirudi utaona tofauti, kesho na keshokutwa utaanza kulia na kuja kwangu, utakuwa umechelewa mwari wangu.
Ukiyafanya yote hakika nyumba ya pembeni haitakuwa na nafasi ya kuweza kukuibia, atakuibia nini ikiwa kila kitu umemaliza na kujimilikisha.
Kwa leo inatosha ni mimi Anti Nasra, Shangingi Mstaafu.
GPL
1 comment:
Samahani kaka mimi nimeoa naninampenda sana mke wangu. Hata kama anifanyii hivyo bado ninampenda. Waswahili wanasema kila shetani na mbuyu wake
Post a Comment