ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 17, 2013

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni mfano wa aina yake- Profesa Ali Mazrui

 Profesa Ali Mazrui akizungumza wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya  Baba wa Taifa Mwalimu Julius K.  Nyerere ambayo hufanyika  kila  Octoba 14, kwa mwaka huu   maadhimisho hayo yamefanyika kwa mara ya kwanza   katika Umoja wa Mataifa na kuhudhuriwa na  mabalozi wa mataifa mbambali  pamoja na watanzania waishio  jijini  New York na vitongoji vyake. Akizungumza  wakati wa maadhimisho hayo  ambayo  mgeni rasmi alikuwa Naibu  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Jan Elliasson kwa  niaba ya Katibu Mkuu, Profesa alimuuelezea Mwalimu Nyerere kama kiongozi   ambaye ameawachia watanzania na dunia uridhi wa aina yake na hasa urithi wa muungano ambao anasema licha ya changamoto zake bado unaendelea kudumu na kuwa mfano wa kuigwa barani afrika na duniani kote.
Profesa Ali Mazrui akiwa ameshika kitabu alichokiandika kwa kushurikiana   Profesa Lindah Mhando,  kitabu hicho kuhusu Mwaliumu Julius   Kambarage Nyerere kilizinduliwa rasmi  wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya  Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere Day ambayo hufanyika Octoba 14.  Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo  ambayo kwa mara ya kwanza yalifanyika katika Makao   Makuu ya Umoja wa Mataifa kwa  kuratibiwa na Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Profesa Ali Mazrui anasema alimfahamu Mwalimu kwa zaidi ya miaka  40, walishirikiana katika mijadala ya kisiasa,  walitaniana lakini waliheshimiana pia.  Anasema  daima  hata sahau  muda  na nyakati  alizokuwa na  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

Na Mwandishi Maalum
Imeelezwa kwamba  licha ya  changamoto mbalimbali,  muungano kati ya Tanganyika na  Zanzibar  uliozaa Tanzania  bado umeendelea kudumu  na kuwa  mfano wa aina yake   Barani Afrika na Duniani kwa ujumla
Hayo yameelezwa  na Profesa Ali Mazrui  siku ya   Octoba 14  wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya  Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage  Nyerere maarufu kama   Mwalimu Nyerere Day. Maadhimisho hayo   yaliandaliwa na uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, na kufanyika  kwa mara ya kwanza   katika  Makao Makuu ya Umoja  wa Mataifa  hapa Jijini New York Marekani.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa  Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Jan Eliasson akimwakilisha Katibu Mkuu Ban Ki Moon. Maadhimisho hayo yalikwenda sambamba na  Uzinduzi wa Kitabu  kinachomhusu Mwalimu Nyerere Kitabu  kijulikanacho kama “ Julius Nyerer African’s Titan on a Global Stage: Perspective from Arusha to Obama”  kilichoandikiwa   kwa ushirikiano wa   Profesa  Ali Mazrui na  Profesa Lindah  Mhando.
“  Uridhi wa Mwalimu  Nyerere siyo ujamaa tu , Muungano wa Tanganyika na Zanzibar  ni uridhi m  mwingine, huu ni muungano ambao umeweza kudumu hadi leo hii, kuna nchi za Afrika  na hasa baada ya  kupata uhuru ambazo  zilijaribu kuungana lakini zikasambaratika  baada ya kipindi kifupi na nyingine hata kuingia vitani. Lakini muungano huu  wa Tanganyika na  Zanzibar,  si kwamba hauna changamoto , la  hasha, unachangamoto zake lakini pamoja na changamoto hizo bado umeweza kudumu kwa muda mrefu tangu mwaka 1964 hadi ” akabainisha Professa  Mazrui.
 Profesa  Mazrui,  msomi, mwandishi wa vitabu, mwanataaluma na   mkufunzi  aliyebobea,aliwaeleza wageni waliohudhuria maadhimisho hayo wakiwamo  mabalozi mbalimbali  na watanzania waishio jijini New York na Vitongoji vyake kwamba Mwalimu Julius Nyerere alikuwa kiongozi wa aina yake aliyeijengea sifa kubwa Tanzania katika duru za kimataifa.
Anauelezea  uridhi mwingine wa  Mwalimu Nyerere ni namna ambavyo  watanzania wameendelea kudumisha utamaduni wakuachiana uongozi wa juu   nchi kwa njia ya amani na bila ya kujali tofauti zao za   dini.
“ Mwalimu alikijenga na kukiinua sana Kiswahili , kupitia  Kiswahili  Mwalimu aliwajengea  watanzania utamaduni wa kuheshimiana bila kubaguana kwa misingi ya kabila au  rangi, Wanabadilishana uongozi wa juu wa  nchi ( urais)katika namna ambayo wala haimo kwenye Katiba yao na wala  si lazima kuuingiza kwenye Katiba. Anashika madaraka ya uongozi mkristo na baada ya muda wake kwisha anashika muislam anamaliza muda wake anakuja mkristo anamaliza muda wake anakuja muislam, ni utaratibu ambao wamejiwekea wenyewe na ni utaratibu unaotoa fursa ya kila mtanzania kushika madaraka ya juu” anaeleza  Profesa Mazrui.
Akielezea zaidi namna alivyomfahamu Mwalimu Nyerere na uridhi wake lukuki aliowaachia watanzania na dunia kwa ujumla,  Profesa  Mazrui anasema
“Nashukuru sana kupata fursa hii ya kuhudhuria maadhimisho ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere pamoja na kuzindua kitambu kunachomuhusu. Nyerere ni  kiongoz niliyemfahamu vizuri  kwa zaidi ya miaka 40 , kuanzia wakati ule nikiwa   Profesa wa Chuo Kikuu cha Makarere,  alikuwa akija mara kwa mara   katika   Kampasi  ya Makerere na  kuna wakati  kwa kipindi kifupi   aliwahi kuwa Chancellor wangu. Mimi na yeye tulikuwa na uhusiano wa karibu, tuliwahi hata kushiriki pamoja kwenye mijadala ya kisiasa  ,  tuliheshimiana na hata kutaniana” Anaeleza
Na kuongeza.  “  kwa  mfano  nakumbuka  niliwahi kumuuliza,  Mwalimu,   umetafsri kwa Kiswahili  kitabu cha Willam Shakespeare  ili hali  wakati huo huo unajaribu  kuutangaza     ujamaa,  kwa nini  usitafsri manifesto ya ukomunisti kama vile Karl Max badala yake . Mwalimu alicheka . Huu ni  mmoja wa  mfano wa utani wetu na Mwalimu Nyerere.  Nitendelea kuyaenzi  matukio haya kwa ufahari wa hali ya juu”.
Anabainisha kwamba  Mwalimu alikienzi sana Kiswahili na alikitangaza sana kiasi cha kuwafanya hata viongozi wengine wa  Afrika kuanza kuenzi lugha zao za asili.  Mwalimu alitumia Kiswahili hata kutafsiri vitabu ambavyo vilitumika katika   kufundishia Tanzania hata   Kenya
Kama hiyo haitoshi,  Profesa  Mazrui anasema daima  ataendelea kuenzi na kukumbuka safari yake ya mwisho aliyokutana na Mwalimu Julius Kambarage  Nyerere. Anaisimulia  siku hiyo kwa kusema
“ Daima nitakumbuka  mara ya mwisho kukutana na Mwalimu. Wote mimi na yeye tulialikwa kwenda kuhudhuria kuapishwa kwa Rais Obasanjo. Sasa wakati wenyeji wetu wakiendelea na shamrashamra,  tulijikuta tukiwa tumebaki peke yetu katika chumba  kimoja . Kwa karibu saa nzima tulikuwa sisi wawili tu. Na tuliitumia saa ile moja kuzungumza na kubadilishana mawazo na tulizungumza kwa Kiswahili. Hata sikujua kwamba wakati ule   Mwalimu alikuwa akiumwa,  hakuonyesha kwamba alikuwa anaumwa. Nilipata mshtuko mkubwa   nilipopata taarifa kwamba alikuwa amelazwa  hospitalini. Daima nitaienzi saa ile moja tulipokuwa pamoja  kwa   mara  ya mwisho. Asanteni sana”  Akasema    Profesa kwa ufahari  mkubwa.

No comments: