Ngasa alilazimika kuilipa Simba kiasi hicho cha fedha ikiwa ni sehemu ya adhabu aliyopewa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka (TFF) baada ya kubainika kuwa aliingia mkataba wenye thamani ya Sh. milioni 30 kwa ajili ya kuitumikia Simba msimu huu kisha kusaini mkataba mwingine na Yanga.
Akizungumza na NIPASHE baada ya kumalizika kwa mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara walioshinda 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi, Ngasa alisema imemuuma sana kulipa fedha hizo, hivyo anajipanga kulipa kisasi dhidi ya Simba.
"Imeniuma kupigwa faini kubwa wakati klabu (Simba) niliitumikia kwa nguvu zangu zote msimu uliopita. Kikubwa kwangu kwa sasa ni kucheza kwa kujituma zaidi ili Yanga ipate ubingwa msimu huu. Naamini kwa kufanya hivyo, nitakuwa nimewajibu Simba," alisema Ngasa.
Mzaliwa huyo wa jiji la Mwanza tayari ameonyesha kuwa ni muhimu katika kikosi cha Yanga kinachonolewa na kocha Mholanzi Ernie Brandts kilichoanza ligi kwa kusuasua, akikifungia goli moja na kutoa pasi ya mwisho katika mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting.
Akitoka kumaliza adhabu ya kukosa mechi sita aliyopewa na TFF, Ngasa alipika goli la ushindi dhidi ya 'maafande' wa Ruvu Shooting lililofungwa na Mganda Hamis Kiiza.
Mchezaji huyo wa zamani wa Kagera Sugar, Azam na Simba alifunga goli la kwanza dhidi ya Mtibwa juzi dakika tano tu baada ya kuanza kwa mechi hiyo iliyokuwa na ulinzi mkali wa vyombo vya usalama kutokana na hofu ya ugaidi.
CHANZO: NIPASHE

No comments:
Post a Comment