ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 4, 2013

NIYONZIMA APATA PIGO, AUNGULIWA NA NYUMBA NA AFIWA NA MWANAE

  • MOTO WATEKETEZA NYUMBA YAKE
Na Elizabeth Mayemba 
 Kiungo wa kimataifa wa Yanga, Haruna Niyonzima amepata pigo kubwa baada ya jana kuunguliwa na nyumba yake iliyopo maeneo ya Magomeni Makuti, Dar es Salaam
.
 Kwa mujibu wa Meneja wa timu hiyo, Hafidh Ally ambaye alikuwa katika eneo la tukio alisema moto huo ulisababishwa na shoti ya umeme na kusababisha hasara kubwa kwa mchezaji huyo.
 
"Kwakweli nipo hapa eneo la tukio baada ya kupata taarifa za mchezaji wetu kuunguliwa na nyumba, tunashukuru Mungu majirani walijitokeza kwa wingi na kusaidia kuuzima moto huo ambao tayari ulikuwa umeshaleta hasara kubwa," alisema Hafidh.
 
   Alisema moto huo uliibuka sebuleni kwa mchezaji huyo na kuteketeza fenicha zote zilizokuwepo ikiwemo na laptop, lakini thamani halisi ya vitu vilivyoungua haijajulikana kwa kuwa ni vitu vingi vilivyoteketea kwa moto.
 
   Inadaiwa kuwa, janga hilo lilitokea wakati mchezaji mwenyewe akiwa ndani ya nyumba hiyo na kama si jitihada za majirani kujitokeza kumsaidia kuuzima moto huo, athari ingekuwa kubwa zaidi.
 
   Imeelezwa kuwa nyumba hiyo ina wapangaji wawili na upande ulioathirika kwa moto ni ambao anaishi mchezaji huyo. Mchezaji huyo amekumbwa na tukio hilo ikiwa ni siku moja tu, tangu adaiwe kuwa anashindwa kuripoti mazoezini kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kifamilia yeye pamoja na beki Mbuyu Twite..

Mtoto wa Niyonzima aanguka sebuleni afariki dunia

Na Saleh Ally
KIUNGO wa Yanga, Haruna Niyonzima amepata msiba mkubwa baada ya mwanaye kuanguka na kufariki dunia wakati akicheza na wenzake.
Mtoto huyo wa Niyonzima, Akbar aliyekuwa na umri wa miaka miwili na nusu, alianguka ghafla na kufariki dunia wakati akicheza na wenzake jijini Kampala, Uganda, mwanzoni mwa wiki hii.
“Mtoto wa Haruna ameanguka na kufariki dunia kule Uganda,” mtoa habari kutoka Kigali, Rwanda alilipasha Championi Ijumaa.
Gazeti hili liliamua kufuatilia ili kupata uhakika kuhusiana na tukio hilo na lilifika nyumbani kwa mchezaji huyo jijini Dar es Salaam na kumkuta mwanaye mwingine, Ramzey na mkewe.
Niyonzima raia wa Rwanda, alionekana kutopenda kulizungumzia kwa undani suala hilo.
“Ni kweli nimepata msiba wa mwanangu lakini nimekuwa na matatizo mengi yanayoniandama hadi nachanganyikiwa kwa kweli. Ningependa mniache kidogo,” alisema kiungo huyo kwa sauti ya taratibu.
Kweli Niyonzima ameandamwa na majanga kwa kuwa jana aliunguliwa na nyumba aliyokuwa akiishi katika eneo la Magomeni Makuti jijini Dar.
Hivyo, gazeti hili likaendelea kufanya uchunguzi zaidi na kugundua mtoto huyo wa Niyonzima alikuwa akiishi na mama yake nchini Uganda.
“Tayari Haruna amempa nauli mdogo wake akashughulikie masuala ya msiba, yeye alikuwa na majukumu mengine lakini pia kama unavyoona, nyumba yake imeungua,” kilieleza chanzo kingine na kuendelea:
“Yule mtoto awali alikuwa Kigali lakini baadaye akahamia Kampala baada ya mama yake kupata kazi huko Uganda na walikuwa wakiishi huko.”
Niyonzima anaishi Magomeni Makuti jijini Dar pamoja mkewe na mwanaye Ramzey mwenye miaka takribani mitano.
Awali kulikuwa na taarifa za kuchanganya baada ya kusikika kuwa amepata msiba wa mwanaye, lakini ukweli si yule anayeishi naye jijini Dar ambaye anajulikana kwa rafiki zake na kwa mashabiki wengi wa soka nchini.

Majira na GPL

No comments: