ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, October 13, 2013

Tuienzi `Nyerere Day` kwa vitendo

Kesho, Taifa linaadhimisha miaka 14 tangu Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alipofariki dunia katika hospitali ya Mtakatifu Thomas, jijini London nchini Uingereza Oktoba14, 1999.

Siku hii ni ya mapumziko kwa wananchi wote nchini huku wakiendelea kutafakari namna Mwalimu, ambaye ni muasisi wa taifa hili alivyolitumikia kwa uaminifu mkubwa, uadilifu na weledi wa hali ya juu wakati wa uhai wake.

Historia ya nchi hii haitamkiki bila ya kumhusisha Baba wa Taifa, marehemu Mwalimu Nyerere, na sababu kubwa ni kutokana na misingi ya utawala wa haki, demokrasia na uwazi, pia uhuru wa kufuata haki za binadamu katika nyanja zote za maisha, alivyovithamini na kuvienzi. Hakika, Mwalimu alikuwa kioo cha uongozi bora barani Afrika.

Mengi aliyoyafanya Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake yamebaki kama kumbukumbu isiyoweza kufutika haraka miongoni mwa wapenda amani nchini na duniani kote. Alikuwa mstari wa mbele katika harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, na siyo siri aliamini zaidi katika ukombozi wa nchi zilizokuwa bado zinatawaliwa hata kuliko maslahi ya nchi yake ambayo ilikuwa tayari huru.

Kuendelea kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa hotuba na maneno mengi ya kumsifia bila kufuata misingi mizuri aliyoturithisha, itakuwa sawa na kuwa wanafiki na watovu wa adabu mbele yake, tutakuwa tunajidanganya na kukidanganya kizazi kijacho ambacho kinatakiwa kiishi kwa misingi aliyotuachia Mwalimu.

Yapo masuala mengi ambayo Mwalimu aliyapigania wakati wa uhai wake, lakini yapo machache muhimu zaidi ambayo aliyapigania zaidi ili yatokomezwe kwa juhudi zote.

Mwalimu alikemea sana vitendo vya rushwa, ubaguzi kwa misingi ya dini, ukabila, rangi, itikadi na kadhalika. Vitendo hivyo aliamini ndivyo vilivyokuwa vinadhoofisha utawala bora na mshikamano thabiti wa kitaifa.

Tangu Mwalimu afariki, taasisi mbalimbali nchini na nyingine za kimataifa zimekuwa zikikutana kwa nyakati mbalimbali ili kujadili maudhui ya Mwalimu kwa mustakabali wa uongozi wa karne ya sasa. Maazimio mengi yamejadiliwa katika vikao hivyo pamoja na mapendekezo kadhaa kutolewa ili kuboresha pale palipoonekana kuwa na mapungufu.

Nia ya makongamano hayo, yaliyokuwa yakifanywa na wasomi wa taaluma mbalimbali yalikusudia kurejesha uongozi wa pamoja na kwenda sambamba na matarajio ya wananchi. Na wakati mwingine yalikuwa yakianzisha mada za kusisitiza umuhimu wa Mwalimu kwa kubatiza majina ya msisitizo wake kama wakati wa 'Kigoda cha Mwalimu' na kadhalika.

Tunaamini kuwa maadhimisho ya miaka 14 ya kifo cha Mwalimu, ambayo mwaka huu kitaifa yanafanyika mkoani Iringa, yatawakumbusha wananchi mambo mengi aliyoyafanya na kuweka msisitizo wa kuyaenzi yote aliyoyaasisi kwa maslahi ya umoja, mshikamano na ustawi wa taifa letu.

Misingi aliyoiacha Mwalimu inatakiwa ifuatwe kwa kuitekeleza kwa vitendo, na hatua hiyo itakuwa ni namna pekee ya kutafsiri jinsi Watanzania tunavyoheshimu maadhimisho ya kifo chake kwa vitendo ili kumbukumbu zake ziendelee kudumu kizazi hiki hadi kingine.

Mchango wa Mwalimu Nyerere katika kuimarisha umoja, mshikamano pamoja na amani ya nchi hii umeelezwa ndani ya vitabu vingi ambavyo baadhi aliviandika mwenyewe, na vingine vingi vimeandikwa na watu binafsi, taasisi mbalimbali pamoja na watafiti wa masuala ya uchumi, utamaduni na mila.

Mengi aliyoyafanya Mwalimu akiwa Rais wa nchi hii na hata baada ya kustaafu uongozi mwaka 1985, yamekuwa msingi mkubwa wa kuendeleza umoja wa kitaifa, ameacha mwangwi wa upendo usioweza kusahaulika.

Tunao wajibu mmoja tu wa kuyaenzi yote mema aliyotuachia Baba wa taifa hili, na kuenzi kwake ni kutekeleza kwa vitendo yote aliyoyafanya ili kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania wote.

Tunaamini wapenda amani wote watashirikiana pamoja katika maadhimisho hayo ya kukumbuka miaka 14 ya Tanzania bila uwapo wa Mwalimu kwa kudumisha upendo, mshikamano na umoja wa kitaifa.

Zidumu daima fikra sahihi za Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere .
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

1 comment:

Anonymous said...

baba yetu mungu akulaze mahali pema hupo ulipo tunakukumbuka sana kwa busara zako na hekima zako.

lakin nawaomba jamani mmrekebishe siku aliyokufa si hii jamani nakuombeni sana hii si siku aliyekufa kabisa na wala sitaniii jamani muugopeni mungu wenu rekebisheni siku hii siyo ahsante

luke mkuu nakuomba tafadhali comment yangu iweke kwa faida ya wenzangu watanzania please sipo hapa kubishana wala kulumbana ila turekebishe siku ya baba yetu wa taifa ahsante