ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 29, 2013

Wanajeshi 2 wafungwa kwa uporaji Kenya

Wanjeshi walionekana wakibeba mifuko ya plastiki kutoka katika duka moja ndani ya jengo la Westgate

Wanajeshi wawili nchini Kenya wamefutwa kazi na kufungwa jela kwa kitendo cha uporaji waliofanya wakati wa shambulizi la kigaidi dhidi ya jengo la Westgate mwezi jana. Hii ni kwa mujibu wa mkuu wa jeshi Julius Karangi.

Karangi alisema kuwa mwanajeshi wa tatu aliyeshukiwa kwa uporaji anachunguzwa.
Awali Karangi alikanusha kuwa wanjeshi walifanya uporaji baada ya kutokea picha za CCT zikionyesha wanajeshi wakibeba mifuko ya plastiki ya moja ya maduka makubwa yaliyokuwa ndani ya jengo la Westgate.

Wanamgambo wa Somalia, al-Shabaab walikiri kufanya shambulizi hilo ambapo waliteka nyara wakenya kadhaa waliokuwa ndani ya jengo hilo kwa siku nne.

Watu 67 walifariki na mamia ya wengine kujeruhiwa.

Wakati huohuo, mkuu wa kitengo cha uchunguzi wa uhalifu katika idara ya polisi,Ndegwa Muhoro alisema kuwa mmoja wa magaidi waliokuwa ndani ya jengo hilo walipiga simu nchini Norway wakati walipovamia jengo hilo.

Mmoja wa washukiwa wa shambulizi hilo ametajwa kuwa Hassan Abdi Dhuhulow mzaliwa wa Somalia ingawa raia wa Norway.

Jeshi limesema kuwa magaidi wote wanne waliofanya shambulizi hilo waliuawa.

Lakini katika ripoti za awali, iliarifiwa kuwa washambuliaji walikuwa kati ya kumi na kumi na watano.

Bwana Muhoro alisema kuwa watu wengine watano wamezuiliwa kwa uchunguzi zaidi na kuwa watafikishwa mahakamani hivi karibuni.

No comments: