SERIKALI imesema klabu ya Yanga haiwezi kupewa eneo la ziada kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wake wa kisasa wa soka.
Ofisa Habari wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rehema Isengo alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, tayari eneo la Jangwani liko katika mipango ya maendeleo.
Msimamo huo wa wizara huenda ukawa pigo kubwa kwa Yanga, ambayo ilipanga kujenga uwanja wa kisasa katika maeneo ya Jangwani, Dar es Salaam.
Mbali na kujenga uwanja wa kisasa, Yanga pia ilipanga kujenga maduka, hoteli, viwanja vya mazoezi, ukumbi wa mikutano na eneo la kuegesha magari.
Klabu hiyo, juzi ilsitisha mkataba wa ujenzi wa uwanja huo na Kampuni ya Beijing Contractors Engineering ya China, ikisubiri majibu ya barua yao ya kupata eneo la nyongeza kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Rehema alisema katika mazungumzo ya awali kati ya wizara na manispaa, tayari eneo la Jangwani liko kwenye mradi wa kujengwa City Garden, hivyo Yanga haiwezi kupewa eneo hilo.
Alisema Yanga ilishapewa majibu hayo kupitia ofisi ya mipango miji na kuongeza kuwa, wizara haihusiki na ugawaji wa viwanja kwa vile suala hilo lipo chini ya halmashauri. Alisema kazi ya wizara ni kupitia faili lililowasilishwa kabla ya kutia saini.
Mbali na hilo, Rehema alisema Yanga inadaiwa deni la kodi ya ardhi tangu mwaka 1997 hivyo ameitaka kulilipa mara moja.
"Yanga siyo walipaji wazuri wa kodi, wanadaiwa kodi tangu 1997, wameshapewa maelezo wafuatilie na kulipa kodi hiyo,"aliongeza.
Ofisa Habari huyo aliweka wazi kuwa, athari inazoweza kupata Yanga endapo itashindwa kulipa deni hilo ni kunadiwa kwa mali zake au kupelekwa mahakamani.
Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo jana.
1 comment:
Asante, Kwa ujumla hizo ni habari nzuri kwa waTanzania kuendelea kupata viwanja mathubuti kwa michezo. Hivi kweli hatuoni ni muhimu kuweka uwanja nje kidogo ya mji kama Kibaha,Bagamoyo hata Mbweni kuelekea na makazi ya wtu yanavyopanuka na hii itakuwa ni mojawapo ya kuweka hayo maduka na biashara nyinginezo. La msingi Serikali ikubali kusaidia kuimarisha babaraba, maji,umeme hospitali na mashule. Kuna sababu gani ya kuwa na viwanja zaidi ya viwili maeneo ya karibu kiasi hicho na ukizingatia ni kati ya mji, na lazima kuwepo na barabara pana ya kuingia na kutoka. Wahusika ombeni eneo lingine kubwa yapo mengi tu na mtawezafanikisha azma yenu sivyo mtayumba miaka na miaka na hela zitayeyuka. asante.
Post a Comment