ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 16, 2013

CHANGAMOTO KUBWA KWETU NI RASLIMALI WATU

Mhe. Anne Makinda ( Mb),Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, akichangia uzoefu wa Tanzania katika ujenzi wa utawala wa kidemokrasia na ushirikishwaji wananchi na nafasi ya Bunge na wabunge katika ujenzi wa demokrasia hiyo ni katika mkutano uliokuwa ukijadili mada kuhusu utawala wa kidemokrasia na nafasi yake katika malengo ya maendeleo endelevu, Mhe. Spika alikuwa ni miongoni wa jopo hilo lilowashirikisha kutoka kushoto Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan. Eliasson, Balozi Pauel Seger wa Usiswi katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Anne Makinda, Balozi Eduardo Ulibarri wa Costa Rika katika Umoja wa Mataifa, Senator Aitzaz Ahsan kutoka Pakistan, na Ms. Gunilla Carlsson aliyewahi kuwa mjumbe mashuhuri kuhusu masuala ya ajenda za maendeleo baada ya 2015 na pia aliwahiki kuwa Waziri wa zamani wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden .

kwa kusikiliza alishosema Mhe. Spika katika mkutano huu sikiliza hapa chini
Mhe. Spika akisisitiza jambo katika siku ya pili ya mkutano wa mwaka wa maspika na wabunge kutoka mabunge mbalimbali duniani wakati walipokutana hapa Umoja wa Mataifa
Sehemu ya wabunge wakifuatiliana na kushiriki majadiliano hayom, aliyekaa kwenye kiti kirefu ni muongoza majadiliano, Nermeen Shaikh Mtangazani na mtayarishaji wa vipindi kuhusu masuala ya Demokrasia sasa
Mhe. Anne Makinga akitia saini kitabu cha wageni wakati alipofika katika Ofisi za Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa kulia kwa Spika ni Naibu Katibu Mkuu, Balozi Rajab Gamaha ambayo kikazi hapa Umoja wa Mataifa.
Mhe. Spika akibadilishana mawazo baadhi ya maafisa na wafanyakazi wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, wapo pia maafisa kutoka Wizara za fedha na Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa wanaohudhuria mijadala ya Kamati mbalimbali za Umoja wa Mataifa
Maafisa wakimsikiliza Mhe. Spika
wafanyakazi wengine

Na Mwandishi Maalum
Pamoja na mafanikio mengi ambayo Tanzania imepiga yakiwamo ya ujenzi wa utawala shirikishi na wa kidemokrasia, zikiwamo pia juhudi na kazi kubwa ya kuwafikishia wananchi maendeleo na upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii bado Tanzania inakabiliwa na changamoto ya raslimali watu

Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Anne Makinda (Mb) wakati alipokuwa akichangia namna gani Tanzania imekuwa ikitekeleza utawala wa kidemokrasia na ambao ni shirikishi tangu nchi ilipopata uhuru wake, na vilevile mchango wa bunge na wabunge katika ujenzi wa demkorasia hiyo.

Mhe. Anne Makinda ( Mb) alikuwa kati ya wanajopo watano wachokoza mada kuhusu utawala wa kidemokrasia na nafasi yake katika maendeleo endelevu baada ya 2015. Mada hiyo ilijadiliwa katika siku ya pili ya mkutano wa mwaka wa siku mbili unaowakutanisha wabunge wakiwamo maspika kutoka zaidi ya nchi mia moja wanaliokutana hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Katika mchango wake kuhusu uzoefu wa Tanzania , Mhe. Makinda pia alifafanua namna ambavyo Bunge na wabunge wa Tanzania wanavyotekeleza majukumu yao na kubwa zaidi katika kusimamia matumizi na mapato ya serikali, uibuaji wa vyanzo vipya vya mapato na kuhakikisha kwamba huduma muhimu za kijamii kama vile elimu, afya na maji zinategewa bajeti ya kutosha.

“Tangu nchi yetu ilipopata uhuru tulijitahidi sana kuhakisha kwamba tunakuwa na utawala shirikishi kuanzia ngazi ya chini kabisa, lakini pia tulihakikisha kwamba huduma muhimu za kijamii zinapatikana na zinasimamiwa, tumepiga hatua kubwa na nzuri lakini bado tunachangamoto ya raslimali watu katika baadhi ya maeneo na tumeshaaanza kutekeleza mikakati ya kuikabili changamoto hii” akafafanua Makinda

Na kubainisha baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni pamoja na utoaji wa ufadhili kwa baadhi ya masomo kama vile ya sayansi na teknolojia, lakini pia bunge limeunda kamati ya kutathimini ubora wa elimu na kuongeza kwamba itaudwa pia kamati ya kupitia utoaji wa huduma za afya.

Akijibu swali la jumla ambalo pia lilijibiwa na wanajopo wengine, kuhusu mkanganyiko katika demokrasia na suala matumizi ya fedha katika chaguzi na rushwa, Makinda alisema, wabunge ndio wawakilishi wa wananchi na kwa sababu hiyo, uwezo wao wa kupambana na matumizi ya fedha katika uchaguzi na mapambano dhidi ya rushwa mafanikio yake yatategemea namna na jinsi bunge Yule ameingiaje bungeni.

Kwa mfano akasema itakuwa vigumu kwa mbuge ambaye ameingia kwa rushwa kupiga vita rushwa, na kwamba matumizi ya fedha katika chaguzi yatamalizwa ikiwa wananchi watakuwa wameondokana na umaskini kwa kile alichofafanua kwamba umaskini wa wananchi ndio unaowafanya baadhi ya wagombea wengi kutumia fedha zao ilikupa nafasi ya uongozi.

Wakati huo huo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan Eliasson amewataka wabunge kuhakikisha kwamba wanashiriki kikamilifu kuutokomeza umaskini uliokidhiri kwa wananchi wao na inakuwa ajenda ya kudumu na endelevu.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ameyasema hayo wakati alipokuwa akichangia majadiliano kuhusu mada ya utawala wa kidemokrasia na nafasi yake katika maendeleo endelevu.

Katika mchango wake, Bw. Elliason, alisema,wakati Jumuiya ya Kimataifa ikiwa katika majadiliano ya kuangalia ni masuala gani yaingizwe katika malengo mapya ya maendeleo endelevu baada ya 2015, umaskini ni moja ya lengo linalopashwa kuwa sehemu ya malengo hayo, na kwamba wabunge nao ambao ni wawakilishi wa wananchi wanatakiwa kuufanya umaskini kuwa moja ya ajenda yao.

Hata hivyo Naibu Katibu Mkuu, akasema ili wabunge waweze kuwasaidia wananchi wao kuondoka na umaskini ikiwa ni pamoja na kushughulika utafutaji wa ufumbuzi wa changamoto nyingine wanatakiwa pia kuwa na ufahamu na uelewa mkubwa wa masuala muhimu yanayoendelea hivi sasa duniani na namna yanavyotafutiwa ufumbuzi katika ngazi ya Jumuiya ya kimataifa kwa kile alichoeleza kwamba yanauwiano mkubwa na kile kinachoendelea ndani ya nchi zao.

Kwa mfano akasema suala la umaskini , matatizo ya uhamiaji, mabadiliko ya tabia nchi ni kati ya ajenda nyingi muhimu zinazojadiliwa katika ngani ya kimataifa ili kuyapatia ufumbuzi.

“ sisi tunajadili katika ngani ya kimataifa, lakini matatizo haya yanauwiano mkubwa na kile kinachotokea katika nchi zenu. Kwa hi kama wabunge mnatakiwa kuwa na ufahamu mpana wa mambo haya na kujua ufumbuzi wake ni nini ili muweze kuwasaidia wananchi wenu”

Akaongeza kwamba, maendeleo endelevu hayataweza kuwa endelevu kama tatizo la umaskini halitafanywa kuwa ajenda endelevu.

No comments: