ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 28, 2015

MJUE HASHIM RUNGWE MGOMBEA URAIS KUPITIA CHAMA CHA CHAUMMA

HISTORIA YAKE

Hashim Rungwe Spunda, ni Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania akifanya kazi zake kama wakili binafsi. Alizaliwa tarehe 01 Januari 1949 katika eneo la Ujiji, mkoani Kigoma (Ametimiza miaka 66 mwezi Januari mwaka huu).

Hashim alianza elimu ya msingi katika shule ya msingi Kipampa iliyoko mkoani Kigoma kati ya mwaka 1959 – 1966 na akajiunga na masomo ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Chuo Kikuu cha Cambridge kati ya mwaka 1967 – 1969 na kuhitimu kidato cha nne, kabla ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita hapa hapa Tanzania.

Mwaka 1975 alisoma ngazi ya Cheti katika Taasisi ya Kukuza Mauzo (Tafsiri yangu) ya Dar Es Salaam, mwaka 1977 alisoma Lugha ya Kifaransa kwa ngazi ya cheti katika taasisi ya “Alliance Francais” ya jijini Dar Es Salaam na kisha akasoma lugha ya kiarabu na elimu ya dini ya kiislamu kwa ngazi ya shahada katika Chuo Kikuu cha Mfalme Abdul kilichoko Saudi Arabia kati ya mwaka 1979 – 1982.

Mwaka 1989 – 1989 alisoma Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam ngazi ya Cheti, akichukua masomo ya Usimamizi wa Umma lakini pia mwaka 1991 alisoma ngazi ya cheti hapo hapo Chuo Kikuu, akijikita katika eneo la Historia ya Afrika na Falsafa ya Historia na Masuala ya Maendeleo (Tafsiri yangu).

Hashim aliendelea zaidi kielimu alipoamua kubobea katika sheria, alijiunga na Chuo Kikuu Huria Tanzania na kusoma shahada ya sheria kuanzia mwaka 1996 na kuhitimu mwaka 2003 na mwaka huohuo 2003 akasajiliwa kuwa wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Kwa upande wa ajira, Hashim amefanya kazi na mashirika mbalimbali ya ndani ya nchi. Kwa mfano, kuanzia mwaka 1969 hadi 1973 amekuwa ni Ofisa aliyeajiriwa serikalini na kufanya kazi katika idara mbalimbali za sekta ya umma.

Pia, mwaka 1982 hadi leo amekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Udalali ya Bahari, lakini pia kuanzia mwaka 1990 hadi leo amejiajiri katika kampuni ya Bahari Motors inayojishughuliza na uuzaji wa magari akiwa kama Mkurugenzi Mtendaji

Kisiasa, Hashim aliwahi kuwa mwanachama imara wa TANU kati ya mwaka 1966- 1977 na kisha CCM kati ya mwaka 1977 – 1995. Ndiyo kusema kuwa wakati mfumo vyama vingi unaanzishwa mwaka 1992 yeye alikuwa mwanachama wa CCM kwa miaka mitatu zaidi kabla ya kuhamia NCCR Mageuzi mwaka 1996.

Alipokuwa NCCR alishiriki hatua mbalimbali za chama hicho katika kupigania mabadiliko, lakini alijiondoa NCCR mwaka 2012 na kuanzisha chama cha siasa kinachojulikana kama CHAMA CHA UKOMBOZI WA UMMA (CHAUMMA) na baada ya kuanzisha chama hicho alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kitaifa wa CHAUMMA mwaka 2014 na anashikilia wadhifa huo hadi hivi sasa.

Hashim Rungwe ameoa na ana watoto watano.

MBIO ZA UBUNGE

Hashim Rungwe alianza kushiriki siasa za moja kwa moja kwa maana ya kusaka ubunge mwaka 1995 alipoomba ridhaa ya kuwa mbunge wa jimbo la Kawe kupitia CCM, hata hivyo aliangushwa ndani ya kura za maoni za chama hicho.

Kwa sababu mwaka 1996 alihamia NCCR, alikaa miaka 9 bila tena kuomba nafasi ya ubunge lakini akajaribu tena mwaka 2005 kwa chama hicho hicho katika jimbo la Kinondoni. Katika uchaguzi ule ambao mshindi alitoka CCM kwa asilimia 67.7 (Idd Azzan) na kufuatiwa na Hamis Hassan wa CUF aliyepata asilimia 24.7 ya kura zote, Hashim Rungwe alichukua nafasi ya saba akiwa na asilimia 0.3 ya kura zote. Baada ya uchaguzi huo, hakugombea tena ubunge kwenye uchaguzi mwingine wowote.

MBIO ZA URAIS

Hashim Rungwe ni mmoja wa watanzania waliowahi kuomba ridhaa ya wanachi kutaka kuongoza taifa hili. Alifanya hivyo kupitia NCCR MAGEUZI, mwaka 2010. Rungwe aliibuka wa tano kati ya wagombea saba wa kiti cha rais akipata kura 29,638 sawa na asilimia 0.31 ya kura zote halali.

Alipitwa na Rais Jakaya Kikwete wa CCM (kura 5,276,827 (asilimia 61.17); Dk. Willibrod Slaa wa CHADEMA (kura 2,271,941 (asilimia 26.34); Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF (kura 431,314 (asilimia 5.2); na Peter Mziray wa APPT Maendeleo (kura 96,933 (asilimia 1.12).

Katika ilani yake aliwahakikishia wananchi kwamba atakapoingia ikulu msisitizo wake utakuwa Mtanzania Kwanza katika harakati za kumiliki njia kuu na ndogo za uchumi wa taifa.

NGUVU YAKE

Sifa ya kwanza inayompa nguvu Wakili Hashim Rungwe ni Umahiri katika sekta binafsi na ya umma. Hashim ni mmoja wa watanzania wachache walioweza na kufanikiwa kushiriki katika ukuzaji wa uchumi wa nchi na kutoa ajira kwa watu wengine.

Alianzisha biashara ya magari na kuwa mmoja wa watanzania walioheshimika sana kibiashara katika jiji la Dar Es Salaam miaka ya nyuma, ameniambia kuwa wafanyabiashara wengi wa sasa wamejifunza biashara kutoka kwake, hasa baada ya kumuona akikua kibiashara wakati ambao iliaminika kuwa wafanyabiashara wakubwa lazima wawe wahindi au watu wenye asili ya nje ya Tanzania. Hashim ana umahiri na uelewa wa kutosha wa sekta binafsi kwa sababu ameshiriki kuijenga na kuihuisha, lakini pia ana uzoefu wa kutosha na kufanya kazi serikalini, mambo ambayo yanampa uwezo binafsi na utashi mpana wa kuongoza katika nafasi za juu katika nchi.

Jambo la pili linalompa uwezo na nguvu ni Uthubutu. Hashim ni mtu anayethubutu sana hasa katika maeneo ya elimu, uongozi na biashara. Tumeona namna alivyokuwa mfanyabiashara mkubwa akipambana na wazungu na wahindi enzi hizo. Lakini uthubutu wake uko pia katika elimu, anaeleza kuwa tangu zamani alipenda sana kuwa mwanasheria baada ya kuona watanzania wanababaishwa na vyombo vya dola na kunyimwa haki zao. Pamoja na umri mkubwa, alijitosa tena darasani na kutumia miaka mitano kupata shahada ya sheria na kisha kuwa wakili. Huu ni uthubutu wa hali ya juu.

Kama hiyo haitoshi, alipoteuliwa kuwa mbunge wa Bunge Maalum la Katiba, pamoja na vyama vya upinzani kuonesha kuwa vingemuunga mkono Mhe. Samwel Sitta kutoka CCM, Bado Hashim alithubutu kuchukua fomu, akapambana bila kuungwa mkono sana na wabunge wa upinzani na akapata kura 69. Huu ulikuwa uthubutu mwingine wa hali ya juu na ni sifa kubwa kwa mtu ambaye ana ndoto za kuwaongoza wanachi katika wadhifa wa juu.

Tatu, Hashim Rungwe ni kiongozi Mtulivu na msikilizaji zaidi. Mara kadhaa nilimuona BMK akijenga hoja baada ya kuwasikiliza sana wenzake na hata mngekutana kwenye viunga vya nje ya bunge, huyu angekueleza masuala muhimu mara baada ya kukusikiliza. Kama nilivyowahi kusema mara kadhaa, wanasiasa wengi ni waongeaji sana kuliko kuwa wasikilizaji zaidi. Marais wengi pia duniani huongea zaidi kuliko kusikiliza, Rungwe anabebwa sana na sifa hii.

Sifa ya nne inayompa heshima na nguvu Hashim Rungwe ni tabia ya kusimamia ukweli. Rungwe hana hofu na vitisho wala propaganda, pamoja na kuwa chama chake bado hakina mtandao mkubwa lakini alipokuwa Bunge Maalum la Katiba alijitangaza wazi kama mwanasiasa aliyekomaa na asiyeyumbishwa.

Wanasiasa na viongozi wa baadhi ya vyama vyenye mitandao hafifu walichezeshwa “densi” ya CCM, Rungwe hakucheza densi hiyo. Mathalani, aliposimama kuongelea suala la Muungano aliweka bayana kabisa na kuunga mkono msimamo wa Tume ya Mabadiliko ya katiba na wananchi walio wengi, hakuuma mdomo wala meno. Tokea wakati huo nilimtofautisha sana na viongozi wengi wa vyama visivyo na wabunge ambao kwa hakika wengi wao walitumia jukwaa la bunge lile kusaidia moja kwa moja matakwa ya katiba ya CCM.

Na mwisho, Hashim Rungwe ni mtu mwenye msimamo binafsi. Naomba hapa nieleweke kwamba kuna msimamo na kuna msimamo binafsi. Mfano ni katika Bunge Maalum la Katiba ambako vyama vinavyounda UKAWA vilijiondoa baada ya kuona misingi ya rasimu imeshakiukwa. Hashim Rungwe alibakia bungeni lakini alikuwa na msimamo wa kipekee sana, aliendelea kupinga hila na matakwa ya CCM bila kujali kuwa vyama vikubwa vyenye wabunge na kisicho na mbunge kimoja vimeshaondoka na kuwa vyama zaidi ya 15 visivyo na wabunge vimebakia na wajumbe wake karibia wote wanaunga mkono mipango na matakwa ya CCM.

Rungwe alikuwa mwiba mchungu na baadhi ya watu walionipigia simu wakati ule walihoji kwa nini UKAWA wasirejee wamsaidie mzee huyu. Hakika alionesha msimamo binafsi, hakufungamana na UKAWA katika kuondoka lakini hakukubali kuburuzwa na CCM. Hata katika uongozi mkubwa wa nchi masuala ya namna hii hutokea na huwa yanahitaji msimamo binafsi, ulio thabiti na wazi wa kiongozi.

UDHAIFU WAKE

Moja ya mambo ambayo nayatizama kama udhaifu wa Rungwe ni kutojitengenezea jukwaa la kudumu la kisiasa hadi leo. Sijui ikiwa chama alichomo ndiyo amefika na kwamba hatakwenda tena kwingine. Maana ameshakuwa mwanachama ndani ya CCM, kisha akaenda NCCR na sasa CHAUMMA.

Naliongelea jambo hili kwa kutambua kwamba viongozi wengi wa upinzani wa sasa waliwahi kuwa CCM, lakini walipotoka huko walibakia katika vyama vya sasa na wanaonesha kuwa watadumu humo. Lakini kwa Rungwe hiki ni chama chake cha tatu. Anapaswa kuweka msimamo na kutulia mahali ili ajenge misingi ya uanzishwaji wa vyama anavyoingia maana katika siasa za kiitikadi kama za Tanzania, mwanasiasa anayehama hama vyama hudharaulika na kuchukuliwa kama hana malengo ya kudumu ya ukombozi.

Lakini jambo la pili ambalo ni udhaifu naouona, Hashim Rungwe hajafanikiwa Hajafanikiwa kujiwekea mizizi ya kisiasa katika siasa za Tanzania. Hadi sasa ameshiriki katika siasa kwa miongo mingi na amekuwa maarufu kiasi fulani (hasa kupitia kugombea urais kwa tiketi ya NCCR mwaka 2010 na pia kushiriki ipasavyo katika mchakato wa utengenezaji wa katiba kwenye BMK), lakini naweza kusema kuwa hajawa na mafanikio yoyote makubwa ya kisiasa.

Hata kama tunafuata ile dhana ya wanaojenga hawafaidiki lakini naona bado ana fursa ya kipekee ya kujipanga kwa uimara unaohitajika ili ajenge mafanikio ndani ya miaka michache ijayo. Mfano mdogo tu ni katika uwezo wake, namtizama kama mtu mwenye uwezo mkubwa kuwashinda hata mamia ya wabunge wa CCM, lakini yuko nje ya siasa za juu hadi sasa. Huku ni kutotambua nafasi yake katika taifa ni udhaifu wa moja kwa moja.

NINI KINAWEZA KUMFANYA APITISHWE


Kama CHAUMMA itamsimamisha au kumpitisha Hashim Rungwe kuwa mgombe urais wa chama hicho, kuna mambo kama mawili yanayoweza kuwa sababu:

Jambo la kwanza nadhani ni kwa sababu ya Uzoefu wa kugombea wadhifa huu mwaka 2010 akiwa NCCR. Katika uchaguzi ule Hashim alipata fursa ya kuzunguka maeneo mengi ya nchi na kujinadi, nadhani alifahamika sana na kwamba kama atapewa fursa ya kuzunguka kwa mara nyingine tena, hata kama yuko katika chama kingine, ana fursa ya kupata kura nyingi zaidi.

Na sababu ya pili ni Uenyekiti wa chama. Kwa kufanya tathmini ya kawaida katika nchi nyingi za Afrika, watu wengi waliogombea urais kutoka katika vyama vya upinzani walikuwa ni wenyeviti wa vyama hivyo au watu wenye nyadhifa za juu. Sababu hii inaweza kumbeba moja kwa moja, hasa ikiwa chama chake hakitakuwa na mtu mwingine mwenye sifa za kutosha.

NINI KINAWEZA KUMWANGUSHA KWENYE MCHUJO?

Jambo moja linaloweza kumwangusha Hashim Rungwe katika mchujo wa chama chake wa kutafuta mwanachama anayeweza kukiwakilisha katika ngazi ya Urais ni Matokeo aliyowahi kupata alipowahi kugombea ubunge na Urais.

Nilieleza hapo juu kuwa kiongozi huyu aliwa kugombea ubunge katika jimbo la Kinondoni, hakika hakupata matokeo mazuri sana, na hata alivyogombea urais kupitia NCCR hakupata matokeo mazuri na yenye kuleta hamasa. Huwenda CHAUMM ikawa na hofu kuwa kiongozi huyu hana mvuto unaohitajika kuweza kumudu siasa za sasa ambazo pamoja na kuhitaji nguvu ya mtandao wa chama lakini pia zinabebwa na nguvu binafsi, umaarufu na mvuto wa mgombea.

MIPANGO MINGINE IWAPO HATACHAGULIWA NA CHAMA CHAKE (PLAN B)

Ikiwa CHAUMMA haitampitisha Hashim rungwe kugombea urais wa Tanzania, namuona kiongozi huyu akiwa na mipango kama minne:

Mpango wa kwanza ni kuendelea na kazi ya kuwatetea wananchi kama wakili wa kujitegemea. Tayari ameshafanya kazi ya UWakili kwa miaka zaidi ya 10 na katika fani ya sheria, uzoefu una umuhimu wa kipekee sana. Hashim nadhani ataendelea kujenga taifa kupitia taaluma hii adhimu.

Lakini jambo la pili ni kujikita katika biashara zake. Ukiachilia mbali kampuni mbili anazoziongoza hadi leo kama zilivyotajwa hapo juu, kiongozi huyu ana kampuni nyingine kadhaa zinazofanya biashara zingine mbalimbali. Kutogombea urais kutakuwa na maana ya kujikita zaidi katika biashara na ujasiriamali.

Lakini jambo la tatu ambalo halikwepeki ni kuendelea Kuongoza chama chake. Hashim ndiye kiongozi wa juu wa CHAUMMA wa sasa. Nadhani atakuwa na nafasi nzuri ya kuendelea na uongozi wa chama hadi uchaguzi mwingine utakapoitishwa. Hili halikwepeki.

Na mwisho namuona akiwa mgombea ubunge. Pamoja na kuwahi kugombea mara moja na kushinda, bado ana fursa ya kipekee ya kufanya vizuri. Japokuwa nafasi ya kupata wabunge kwa wagombea wa vyama visivyo na wabunge hadi sasa ni ngumu zaidi katika uchaguzi wa mwaka huu kwa sababu ya nguvu ya UKAWA na ujio wa chama kipya cha ACT ambacho kina nafasi ya kupata kura nyingi ambazo zingechuliwa na vyama visivyo na mitandao mikubwa kwa hivyo chaguo hili la ubunge pia lina madhara yake.

HITIMISHO

Hashim Rungwe anaamini kuwa tatizo la ajira na kukosekana kwa uongozi bora ndiyo mambo makuu ambayo nchi hii haijayashughulikia, anasema kuwa wananchi wakiwa na ajira za uhakika katika sekta binafsi na ya umma, halafu kukawa na uongozi bora, nchi yetu itakwenda mbele bila hofu na kila mwananchi atafurahia kuwa mtanzania.

Pamoja na mawazo haya mazuri ya kifalsafa, Hashim Rungwe na CHAUMMA wanakabiliwa na wakati mgumu mno kisiasa, ana wajibu wa kujipanga mno yeye na chama chake ili kufikia malengo makubwa ya kitaifa ya uanzishwaji wa vyama. Hata hivyo, namtakia kila la heri yeye na chama chake katika kuendea majaribio mengine ya kisiasa yatakayowakabili katika siku za mbele.

MWANANCHI

No comments: