ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 26, 2013

Dk Kawambwa ajibu makombora ya Nape

Bagamoyo. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa amejibu madai yaliyotolewa hivi karibuni na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kwamba ni mmoja wa mawaziri walioshindwa kazi, hivyo kustahili kung’olewa.
Katika madai yake, Nape alisema Dk Kawambwa ameshindwa kusimamia vyema madai ya walimu na kwamba akiwa Waziri wa Miundombinu, aliingia mkataba na Kampuni ya ujenzi ya Progressive iliyopewa zabuni ya kujenga Barabara ya Namtumbo hadi Tunduru wakati mkandarasi huyo hana uwezo wa kuijenga.
Nape alikaririwa akisema kwamba umefika wakati kwa waziri huyo na wenzake wa Fedha, Dk William Mgimwa; Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza; na Naibu wake, Adam Malima kuhojiwa na Kamati Kuu (CC) ya chama hicho.
Akijibu madai hayo Mjini Bagamoyo jana, Dk Kawambwa alisema anasubiri kwa hamu kuitwa CC kueleza tuhuma zinazomkabili huku akijigamba kuwa yeye ni mti wenye matunda ndiyo maana unapigwa mawe.
Alisema hayo alipokuwa akikabidhi vifaa vya michezo kwa timu 16 zitakazoshiriki michuano ya Kombe la Kawambwa inayofanyika katika Jimbo la Bagamoyo ambalo yeye ni mbunge wake.
“Kuna maneno yanayoendelea hivi sasa eti na mimi mbunge wenu natajwa kuwa fisadi kwa mkataba wa ukandarasi wa barabara, siyo kweli. Wakati mkataba ule unasainiwa mimi nilishatoka kwenye Wizara ya Miundombinu, sihusiki kabisa na mkataba ule,” alisema na kuongeza:
“Mwaka 2010 mimi ndiye niliyeshawishi Ubalozi wa Japan ukatoa fedha kwa ajili ya mradi ule wa Barabara ya Namtumbo - Tunduru lakini mkataba ukasainiwa Desemba 24, 2012 kati ya Wizara na Kampuni ya Progressive.
“Walipovurunda Wizara ikawatimua, mimi sikuhusika hata kidogo kwani wakati wanasaini mkataba ule mimi nilishahamishiwa wizara nyingine.”
“Mimi nipo baridi, nasubiri kwa hamu kubwa kuitwa kwenye Kamati Kuu, mimi si mtu wa kupiga kelele na tuhuma zote dhidi yangu ninaamini si za kweli... wakati mwingine maadui wanatafuta njia za kunichonganisha na chama changu.”
“Wanasema kila wizara ninayopelekwa ninavurunda, nasema, mimi ni mti wenye matunda. Mti wowote ambao unazaa vizuri lazima utapigwa mawe, nasubiri siku hiyo ya kuitwa CC ambako pumba na mchele vitajulikana.”
Akizungumzia ujenzi wa barabara hiyo, Waziri Kawambwa alisema anamshukuru  Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli aliyemfukuza mkandarasi huyo Progressive kwa kushindwa kazi. Hata hivyo, katika madai yake, Nape alisema kumfukuza mkandarasi huyo pekee hakutoshi, bali aliyehusika kumpa mkataba naye anapaswa kuchukuliwa hatua kwani uchunguzi unaonyesha kuwa alishashindwa kazi wakati anapewa mkataba.
Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alikaririwa na Gazeti la The Citizen akisema kuwa Chama Cha Mapinduzi hakina mamlaka ya kuingilia utendaji wa Serikali kwani kinatakiwa kuishia katika ngazi za watendaji wa chama.
Kinana
Wakati huohuo, Lauden Mwambona anaripoti kutoka Tukuyu, Mbeya kwamba, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amewalaumu viongozi wa chama hicho ngazi za mikoa na wilaya kwa kushindwa kuisimamia Serikali na kusababisha Watanzania wengi wakupoteza imani nacho.
Kinana alisema hayo jana alipokuwa akihutubia wakazi wa Halmashauri ya Busokelo wilayani Rungwe katika Mji mdogo wa Kandete katika siku ya pili ya ziara yake  mkoani Mbeya.
Alisema Serikali Kuu inapeleka fedha nyingi kwenye halmashauri na mikoa lakini matokeo yake zinaishia kwenye matumbo ya watu jambo ambalo limewakasirisha Watanzania wengi.
Aliwataka viongozi wa CCM kufuatilia fedha zinazoingia kwenye miradi ya maendeleo na kama Serikali haikutuma fedha hizo, ipo haja ya CCM kufuatilia kwa viongozi wakuu wa nchi.
Kuhusu uchaguzi ndani ya CCM, aliwasihi viongozi hao kuachana na tabia ya kuwapendelea watu wanaotoka mijini au nje ya eneo husika wanaotaka kuwania uongozi badala ya kuwasikiliza kwanza wagombea wanaotokana na wananchi wenyewe.
“Tuachane na tabia ya kuwateua vigogo wenzetu au wenye fedha kugombea nafasi za uongozi ndani ya CCM au Serikali. Tuwasikilize wananchi wanamtaka nani,’’ alisema.
Leo Kinana anatarajia kuendelea kuwahutubia 
Mwananchi

No comments: