
Kocha Mkuu wa Simba, Abdallah Kibadeni.
Simba ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 21, Yanga (25), huku Azam na City zikiongoza kwa pointi 26
Dar es Salaam. Simba inafahamu kwamba inahitaji ushindi ili kutuliza hasira za mashabiki wake itakapokabiliana na Ashanti United leo katika pambano la Ligi Kuu litakalopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambalo pia litaamua hatima ya benchi la ufundi likiongozwa na Abdallah Kibadeni.
Pambano hilo ni miongoni mwa michezo minne kati ya saba ya raundi ya 13 ya mwisho ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara itakayotimua vumbi leo katika viwanja vinne tofauti.
Patashika zingine ni Mtibwa Sugar itakayoumana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini, wakati Kagera Sugar itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kupepetana na Mgambo Shooting, JKT Ruvu itaonyeshana umwamba na Coastal Union katika pambano litakalopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Wekundu hao wa Msimbazi Simba, wanakamata nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo, wakiwa na pointi 21, baada ya kushuka uwanjani mara 12 na kuibuka na ushindi mara ya tano, sare sita na kuambulia kichapo kimoja.
Mahasimu wao wakuu, Yanga wapo katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 25, wakati Azam FC inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 26, ikifuatiwa na Mbeya City inayolingana nayo pointi katika nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao.
Simba ambayo mashabiki wake walizusha vurugu kubwa baada ya timu yao kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar katika mechi iliyopita, kama itaifunga United itafikisha pointi 24, hivyo kuikimbia Mtibwa Sugar inayokamata nafasi ya tano ikiwa na pointi 19 na ambayo kama itaifunga Ruvu Shooting itafikisha pointi 23.
Hata hivyo, Simba italazimika kucheza kwa hadhari ili isiweze kuumbuliwa na United ambayo kwa siku za karibuni imekuwa ikicheza soka la mipango na kushinda mechi kadhaa.
Lakini, Kocha wa Simba, Kibadeni amewatoa hofu mashabiki wake na kusema kikosi chake kipo katika hali nzuri ya kimwili na kisaikolojia.
TFF YAISHANGAA TOTO
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema Erick Kyaruzi ni mchezaji halali wa klabu ya Kagera Sugar na kudai kuwa malamamiko ya Toto Africans ya Mwanza hayana msingi.
Kauli ya TFF imekuja baada ya juzi uongozi wa Toto Africans kuibuka na kudai kuwa mchezaji huyo ni mali yao na kwamba Kagera inamtumia isivyo halali.
Katika kusisitiza, uongozi wa Toto ulidai kuwa uliwahi kumtumia Kyaruzi katika mojawapo ya mechi za Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2013-14, hivyo kushangazwa na kitendo cha mchezaji huyo kuichezea Kagera katika pambano la hivi karibuni dhidi ya Simba.
Lakini jana, Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Saad Kawemba alisema madai hayo ya klabu ya Toto si ya kweli na yanalenga kusababisha migongano isiyo ya lazima.
“Hivi kweli TFF inaweza kumwidhinisha mchezaji klabu mbili ndani ya msimu mmoja? TFF ni chombo makini hakiwezi kufanya jambo kama hilo Toto wanadanganya.
“Hebu waambie jamani hao Toto wawape leseni ya huyo mchezaji kama wanayo lakini ukweli ni kwamba hawawezi kuwa nayo,” alisema Kawemba na kuongeza:
“Kagera ndiyo wenye leseni ya huyo mchezaji iliyotolewa na TFF na ndiyo wenye uhalali wa kumtumia, Toto walileta fomu za maombi ya usajili wa mchezaji huyo lakini kwani kinachozingatiwa ni taratibu kama hazikufuatwa hawezi kupitishwa”.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment