Juzi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed, aliwasili nchini na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe, na kuelezea msimamo wa Serikali ya Kenya wa kuunga mkono kauli ya Rais Kikwete.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wasomi hao walisema kuwa kitendo hicho kitasaidia kupunguza makali ya mgogoro huo hususani katika kikao kinachotarajiwa kuwakutanisha viongozi wa nchi hizo Novemba 30, mwaka huu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally, alisema kitendo cha Kenya kuiunga mkono Tanzania ni dalili nzuri ya kutovunjika kwa jumuiya hiyo.
Alisema Kenya na Tanzania ndiyo nchi zenye uchumi mkubwa kwa Afrika Mashariki hivyo kama nchi mojawapo kati ya hizo ikijitoa kuna uwezekano wa Jumuiya kuvunjika, na ndiyo maana Kenya ikaamua kuiunga mkono Tanzania.
Aliongeza kuwa kitendo cha Kenya kuiunga mkono Tanzania ni jambo zuri na linaweza kuzishawishi nchi zingine kuiunga mkono Tanzania.
“Diplomasia ni kitu ambacho kina nguvu sana, hivyo tunahitaji kulichukulia suala hili kwa mapana zaidi,” alisema Ally.
Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa UDSM, Dk. Benson Bana, alisema kitendo cha Kenya kuiunga mkono Tanzania kinatoa maana mbili ambayo ni muktadha wa Kenya ilipo kwa sasa na kuonyesha diplomasia inavyofanya kazi.
Alifafanua kuwa kwa kiasi kikubwa hatua hiyo imetokana na kipindi hiki viongozi wa Kenya kuhitajika katika Mahakama ya Kimataifa ya kiharifu ya (ICC) huku Tanzania ikiuunga mkono Kenya kwa kutokubali viongozi wao kwenda katika Makahama hiyo.
Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake, William Ruto wanakabiliwa na kesi ICC iliyoko The Hague, Uholanzi kutokana na tuhuma za kuhusika kupanga ghasia zilizosababisha watu takribani 1,500 kuuawa na wengine zaidi ya 500,000 kupoteza makazi yao baada ya ghasia hizo zilizofuata baada ya kutangazwa kwa matokeo ya urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
“Kile kitendo cha Tanzania kuisaidia Kenya kutokubali Rais wake na Makamu wake kwenda mahakamani nadhani ni mojawapo ya sababu ya Kenya nayo kuiunga mkono Tanzania sasa katika suala hili,” alisema Dk. Bana.
Alisema kitendo cha Tanzania kuiunga mkono Kenya, ndiyo sababu Rais wa Kenyatta naye kuamua kuiunga mkono Tanzania kwa sasa baada ya kuona wanachokifanya siyo sahihi.
Hata hivyo, Dk. Bana alisema kamka Tanzania ingelichukua hadhari tangu mapema baada ya nchi hizo kukaa kikao cha kwanza pasipo kuishirikisha, matatizo yote yanayotokea sasa yasingelikuwapo.
Kadhalika, Dk. Bana alitoa ushauri kwa serikali ya Tanzania kuwa na kiongozi mmoja anayeshughulikia na kuzungumzia suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki kuliko kuzungumziwa na Waziri Membe na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
“Linapokuja suala la Afrika Mashariki nani mwenye kauli ya kulitolea maamuzi je, ni Membe au Sitta?” alihoji Dk. Bana.
Mtafiti wa Uchumi na Mhadhiri wa UDSM, Dk. Haji Semboja, alisema ni jambo zuri lililofanywa na Kenya kuiunga mkono Tanzania.
Alisema Kenya inajali zaidi kimaendeleo hususani masuala ya kibishara, hivyo wameona kutoiunga mkono Tanzania katika jumuiya kutazorotesha mipango yao ya kupiga hatua.
Akihutubia taifa Alhamisi iliyopita kupitia Bunge, Rais kikwete alielezwa kushangazwa na hatua za mataifa hayo matatu ya kuvunja makubaliano ya mkataba wa Afrika Mashariki na kuzitenga Tanzania na Burundi.
Katika hotuba hiyo, Rais Kikwete alitaja maeneo manane ambayo mataifa hayo yameanza ushirikiano wa walio tayari (Coalition of the willing) na kusisitiza miongoni mwayo, manne yanavunja moja kwa moja makubaliano ya jumuiya hiyo.
Mambo hayo ni, moja ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa-Kigali-Bujumbura-Sudan Kusini; mbili ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya-Uganda-Sudan Kusini; tatu ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta; nne ushuru wa forodha wa pamoja; tano kuharakisha shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki; sita viza ya pamoja ya utalii ya Afrika Mashariki; saba kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria; nane uzalishaji na usambazaji wa umeme wa pamoja.
Katika hayo, Rais Kikwete alitaja manne ambayo hayagusi makubaliano ya pamoja ya jumuiya kuwa ni bomba la mafuta, kiwanda cha kusafisha mafuta, umeme na reli ya kisasa. Hata hivyo Tanzania ina maslahi ya moja kwa moja katika miradi hiyo, lakini haijui kwa nini haikushirikishwa.
Hata hivyo, Rais kikwete alisema Tanzania haitajitoa EAC na itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu kwa kuwa imetumia muda wake mrefu na rasilimali nyingi kwani inachangia Dola za Marekani milioni 12,000 kila mwaka.
Mara baada ya waziri huyo kukutana na Membe, jijini Dar es Salaam juzi, katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, alisema ziara yake ya siku moja nchini, ilikuwa na lengo la kuonyesha namna Kenya ilivyoguswa na kuridhishwa na kauli ya Rais Kikwete kuhusiana na suala la EAC.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
Kwa mara ya kwanza baada ya kipindi kirefu Tanzania immeipita Kenya kweye mapato ya-nayotokana na Utalii. Hawa jamaa ni majirani wetu lakini pai ni washindani wetu kibiashara mfano kkt Utalii.
Uwamuzi wao wa maksudi wa kumchagua Uhuru Mtuhumiwa wa mauaji ya kikabila kuwa Rais wao It's in our advantage economically, I hope our leaders can see that.
Post a Comment