Uchaguzi mwenyekiti Juni 29, 2014
Uwezekano wa kumpata mrithi wa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara iliyokuwa inashililiwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ambaye alivuliwa wadhifa huo mwishoni mwa wiki ni Juni 30 mwakani.
Pia uchaguzi wa Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema ambao umekuwa chanzo cha mzozo ndani ya chama hicho, utafanyika Juni 29, mwakani.
Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi wa nafasi mbalimbali za chama hicho kuanzia ngazi ya vitongoji hadi taifa, wanachama wataanza kuchaguana kuanzia Desemba 15 mwaka huu hadi Janauri 15, mwakani, huku viongozi wakuu wa kitaifa wakipatikana wote ndani ya Juni mwakani.
Ratiba hiyo ilitangazwa jana na Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa chama hicho, Benson Kigaila, katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa katiba ya Chadema, nafasi za katibu mkuu na manaibu wake wawili hupatikana baada ya mwenyekiti kuwasilisha majina mawili kwa kila nafasi kwenye Baraza Kuu kwa ajili ya kupigiwa kura.
Kulingana na ratiba hiyo, uchaguzi huo unamaliza Juni 29, mwakani na uwezekano wa kukutana na Baraza Kuu ni siku moja baada ya kupatikana kwa Mwenyekiti na makamu wake wawili kwa nia ya kuunda sektretariati ambayo huongozwa na Katibu Mkuu akisaidiwa na Manaibu Katibu wakuu wawili, mmoja kutoka Bara na mwingine Zanzibar.
Alisema ratiba hiyo ni utekelezaji wa programu ya ujenzi wa Chadema na mchakato ulianza Novemba 22, mwaka huu kwa kazi ya kusajili wanachama kwenye misingi (ngazi ya vitongoji) yote, ambayo inaendelea hadi Desemba 14, mwaka huu.
Kigaila alisema kwa mujibu wa ratiba hiyo, Desemba 15, mwaka huu hadi Januari 15, mwakani, utafanyika uchaguzi ngazi ya vitongoji na kwamba, Januari 16-30, kitakuwa kipindi cha rufaa na kukagua ukamilifu wa uchaguzi katika ngazi hiyo
Alisema Februari 1-15, mwakani, utafanyika uchaguzi ngazi ya matawi, ambao vijiji kwa vijijini na mitaa kwa mijini na kwamba, Februari 16-29, kitakuwa kipindi cha rufaa na ukaguzi kwenye ngazi hiyo.
Kigaila alisema Aprili 1-10, utafanyika uchaguzi ngazi ya majimbo 139 ya uchaguzi, wakati uchaguzi ngazi ya wilaya utafanyika Aprili 25 hadi Mei 5.
Alisema Mei 20-25, utafanyika uchaguzi ngazi ya mikoa na kwamba, uchaguzi kwenye kanda zote 10 za chama utafanyika Juni 9.
Kwa mujibu wa Kigaila, uchaguzi ngazi ya Taifa Juni 25-30, kwa kuanzia na uchaguzi wa Baraza la Wazee, ambao utafanyika siku moja na ule wa Baraza la Vijana (Bavicha).
Alisema siku ya pili yake (Juni 26) utafanyika uchaguzi wa Baraza la Wanawake (Bawacha) na siku inafuatia (Juni 27) kitafanyika kikao cha Kamati Kuu (CC) inayomaliza muda wake.
Kigaila alisema siku inayofuata (Juni 28) kitafanyika kikao cha Baraza Kuu linalomaliza muda wake kabla mkutano mkuu, ambao utafanya uchaguzi wa viongozi wa kitaifa.
Baadaye, kitafanyika kikao cha Baraza Kuu jipya kwa ajili ya kuchagua CC mpya na siku ya mwisho CC mpya itaweka utekelezaji wa maazimio ya Baraza Kuu na mkutano mkuu kwa kipindi kijacho.
Mapema, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alisema ratiba hiyo imetokana na maamuzi yaliyofanywa na sekretarieti ya chama hicho.
Mnyika alisema kabla ya hapo, CC katika kikao chake cha Novemba 20-22, mwaka huu, ilijadili kuhusu utekelezaji wa programu mbalimbali za chama, ikiwamo ya ‘Chadema ni Msingi’ na operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) kwenye Kanda.
“Kamati Kuu ikapitisha maamuzi juu ya mwendelezo wa operesheni hizi baada ya kupokea mapendekezo kutoka kwa sekretarieti ya chama na sekretarieti ikatakiwa kwenda kufanyia kazi hizi ambazo chama kinaendelea kuzifanya,” alisema Mnyika.
Awali, Kigaila alisema CC katika kikao hicho ilipokea taarifa ya utendaji ya programu ya ‘Chadema ni Msingi’ na kuazimia mambo kadhaa ya namna ya kulipeleka mbele na kuandaa ratiba ya uchaguzi wa ndani ya chama, kuanzia ngazi ya chini hadi taifa.
Alisema Januari 28, mwaka huu, Baraza Kuu la chama lilikaa jijini Dar es Salaam na kupitisha programu ya kugatua mamlaka ya kupanga, kusimamia na kuendesha programu za ujenzi wa chama kutoka makao makuu na kupeleka mamlaka hayo katika ngazi za kanda.
Alizitaja kanda hizo zilizoundwa na Baraza Kuu kuwa ni Ziwa Magharibi, Ziwa Mashariki, Magharibi, Pemba, Unguja, Kusini, Kaskazini, Kati na Nyanda za Juu Kusini.
Alisema mkakati wa kugatua madaraka, una hatua nne; ambazo ni pamoja na kuzindua na kupata uongozi wa kanda, kutoa mafunzo kwa timu za Taifa, kanda, mikoa, majimbo, kata, vijiji/mitaa na vitongoji, kuunda misingi ya chama na kufanya uchaguzi wa ndani ya chama.
Kigaila alisema kanda zote nane za Bara zimekwishazinduliwa na zina uongozi kamili na kwamba, zile za Zanzibar zimekwishawasilisha mkakati wao na zitazinduliwa mwanzoni mwa Desemba, mwaka huu.
Kigaila alisema jana timu 13 ziliondoka makao makuu kwenda katika kanda kushirikiana na kuunda timu kwenda katika majimbo 103 kwa ajili kukagua utekelezaji wa zoezi, kutambua changamoto zilizopo ili kusaidia upatikanaji wa suluhisho na kutoa mafunzo kwa watekelezaji.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment