ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 16, 2013

PROF.MUHONGO "WATANZANIA NI WAVIVU WA KUFIKIRI, WAVIVU KUSOMA NA WASHAMBA WA UWEKEZAJI"

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ameingia katika mgogoro mwingine wa uzembe wa matumizi ya ulimi. Hilo lilitokea juzi katika ukumbi wa Classic Ubungo Plaza mbele ya viongozi wa dini kutoka kote nchini ambapo waziri huyo alikuwa akiwahutubia viongozi hao kuhusiana na sekta nzima ya madini na rasilimali za nchi. Kongamano hilo liliandaliwa na Kamati ya Kudumu ya viongozi wa dini inayojishughulisha na utetezi wa rasilimali za nchi na haki za wananchi.
Viongozi waliohudhuria walitoka Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Tume ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) pamoja na asasi za kiraia za haki madini, Policy Furum, Norwegian Church Aid, Ongea na wawakilishi wa taasisi za elimu ya juu hapa nchini.

Kauli ya Askofu Benson mwenyekiti wa mkutano
Mwenyekiti wa mkutano huo, Askofu Benson Bagonza wa Dayosisi ya Karagwe, katika ufunguzi, alimweleza Muhongo kuwa licha ya uwekezaji mkubwa katika uvunaji wa rasilimali za madini, wananchi wanaoishi katika maeneo ya migodi ni maskini wa kutupwa. Alisema kuwa haki zao za kibinadamu haziheshimiwi na mazingira yameharibiwa sana huku akirudia wito wa kamati yake kuitaka serikali kuweka wazi mikataba ya madini na kuondokana na usiri unaoghubika sekta hiyo.

Majibu na matusi toka kwa Waziri Muhongo kwa maaskofu na watanzania
Akijibu hotuba hiyo waziri huyo alikanusha vikali akisema mikataba yote ya madini iko wazi na kwamba ilipelekwa kwenye ofisi ya Spika ili wabunge waweze kuisoma lakini cha ajabu wabunge hao wameshindwa kuisoma huku wakiendelea kulalamika kama ilivyo kwa Watanzania wengi.

Akionekana kutamba na kujigamba mbele ya viongozi hao, Prof. Muhongo alisema Watanzania ni wavivu wa kufikiri, wavivu wa kusoma na washamba sana katika masuala ya uwekezaji. Aliwalaumu watu mbalimbali mara kadhaa bila kuwataja majina kuwa wanapenda kutumia ‘vihela’ vya familia zao kudai wapendelewe kupewa vitalu vya gesi huko Mtwara lakini akasema chini ya uongozi wake hilo halitatokea.

“Hawa wanaodai wapendelewe kwa kuwa ni wazawa, wakiishatajirika watasababisha vita kwa sababu watu maskini hawatavumilia kuona matajiri wakineemeka wakati wao ni maskini wa kutupwa,” alisema.
Katika hotuba yake iliyochukua masaa mawili, Prof. Muhogo aliendelea kutumia maneno kama ‘kukurupuka’, ‘upuuzi’, ‘ushamba’, ‘uzushi’, “non performers” na mara kadhaa alionekana kuwaponda Watanzania kuwa hawasomi ndio maana wanaishia kulalamika kila kukicha.

Askofu Oscar wa Newala/Mtwara ampa wakati mgumu Muhongo
Ndipo katika kipindi cha maswali na majibu alipokumbana na hasira ya wanakongamano ambapo wa kwanza alikuwa ni Askofu Oscar Mn’unga wa Dayosisi ya Newala na Mtwara. Askofu huyo alimwambia Waziri Muhongo kuwa ana lugha za kibabe na dharau kwa Watanzania.

“Umekuja umejihami na ubabe wako lakini ujue wananchi wa Mtwara si wajinga tena hata kama wako kimya,” alisema askofu huku akishangiliwa kwa vigelegele.

Mwenyekiti wa mkutano ampa Muhongo ushauri wa busara
Mwenyekiti wa mkutano, Askofu Bagonza, kwa kutumia hekima kubwa alimshauri Muhogo kuazima hekima na uzoefu wa viongozi wa dini.

“Ukiona mtu anakuja kwako akiwa peke yake ujue mtu huyo ana matatizo; lakini ukiona kundi la wawili au watatu wanakuja kwako kiongozi, uwe na uhakika kuwa una matatizo na uwasikilize,” alisisitiza Askofu Bagonza.

Askofu huyo aliendelea kumshauri waziri kuelewa kuwa viongozi wa dini wana wajibu wa zaidi ya kulinda kundi lisishambuliwe na mbwa mwitu na kwamba ni wajibu wao pia kuwaonyesha watawala vichaka vyenye mbwa mwitu katika sekta ya madini.
Profesa Muhongo alipopwaya kuendekeza ubabe
Kilele cha malumbano kati ya Waziri Muhogo na Askofu Oscar kilifika pale askofu huyo alipoituhumu serikali kwa kushusha mabomba ya gesi katika bandari ya Dar es Salaam badala ya Mtwara.

Alisema hatua hiyo ilisababisha yasombwe na malori yanayoharibu barabara zao, kauli iliyomwinua Waziri Muhogo na kumwita askofu huyo kuwa ni mwongo.

“Huo ni uwongo na aibu kwa askofu kusema uwongo,” alisema waziri kisha akaongeza:

“Mimi siendi kanisani mara kwa mara lakini sisemi uongo kama watu wanaoenda kanisani kila siku.”

9 comments:

Anonymous said...

Huyu Muhogo ni nani hapa Tz???Hapo ndipo tunapomkumbuka baba wa taifa,alihutubia kuwa cheo ni dhamana!!!

Anonymous said...

Nakubakiana wewe kabbisa. Sisi tunasoma magazeti ya udaku (Diamond na Wema).Mtu anaita waandishi wa habari eti kujibu tuhuma zilizoandikwa magazetini kwa sababu wasomaji wanaziamini. Watu wanapenda title, party 24/7, kufuatilia mambo yasiyowahusu, majungu, ufisadi, rushwa za ngono na ujanjaujanja. Jumuiya ya Afrika mashariki itatuanika, maana wakenya watamiliki kila kitu chetu na kututumikisha.

Anonymous said...

Ni dhahiri Prof. muhongo sio kiongozi bora, nina mengi ya kusema ila tu kwa kifupi niseme "he is the house nigga" and he don't value the rest of us who are in plantation.

He has to look back on where he came from....na elimu aliyoipata ni jasho la watanzania hao hao ambao leo hii anawakanyaga.

Mimi nadhani kwa Elimu yake na exposure aliyoipata angekuwa ni miongoni mwa watu ambao wangetoa a very clear direction kwa watanzania ni nini kifanyike ili kuhakikisha rasilimali ya nchi yetu inalinufaisha taifa letu na wake. Ninachokiona kwake ni kiongozi analala akiwaza ni wazungu gani awalete kuwekeza nchini kwetu.

It is time kwa watanzania wenzangu tuamke na tuanzishe mapambano kwa viongozi kama hawa. Ni ukweli usiopingika Prof. anafaa kufundisha tuu lakini sio kuongoza wizara katika nchi yetu.

Sometimes ulefu wa CV zetu does not guarantee our performances as we see from this individual.

Anonymous said...

Je Mawaziri hao si Watanzania? Kwa mantinki hiyo Mawaziri nao ni wavivu wa kufikiri na washamba wa uwekezaji na wavivu wa kusoma kwa sababu wanafuatisha interest zao na si za wananchi.Nawakilisha.

Anonymous said...

Yap hilo la uvivu wa kusoma na kufikiri...wala si ajabu watanzania sisi ni WAVIVU wa kufikiri, kusoma na zaidi sana tunajua KUIGA, KULALAMIKA.....

Anonymous said...

Huyu MUHOGO UUPS MUHONGO NAONA ANATUYUMBISHA, Mheshimiwa Rais hebu mpumzishe ajifunze kuwatumikia wananchi arudi 2020. Tafadhali punguza makali ya rasilimali zetu.

Anonymous said...

it is high time huyu jamaa awajibike/shwe.. he is not where he is to be defensive, a good leader always listens.. so far amekuwa ni mtu wa kukanusha na kushutumu hatuoni solutions ambazo ni za faida kwa watanzania.. Hivi ni kitu cha siri kwamba mabomba ya gesi yalipelekwa mtwara kwa malori??
Mhe. Muhongo tafadhali swaiba kashike chaki tena hukoooo wala sio hapa nchini kwetu nendaga baba utuacheeeeee..na ushamba, uzushi, ujinga, na uvivu wetu. kumbuka hata wewe umetokea huku huku na pasi shaka kwa kodi za watanzania sisi sisi.

Sammy said...

Ni kweli mabomba yalipelekwa na malori na Professor hapo hakanushi.Anapokanusha Professor kwa kusema ni Uongo ni pale Askofu anaposema Barabara ziliharibika kutokana na zoezi hilo,kwa maana nyingine anasema hakuna Uharibifu wa barabara wowote uliotokea.
Pia,anaposema ni wavivu kusoma anamaana kwamba Watanzania(Wabunge) ni wavivu kusoma mikataba ya uwekezaji wa madini ambayo Serikali imekubaliana na Wawekezaji.Mikataba hiyo iko pale Bungeni kwa Mbunge kuweza kusoma na kuweza kuikosoa kwa kutoa kasoro kufuatia vipengele vya makubaliano katika mikataba hiyo.Hana maana ya kwamba Watanzania hawajasoma kama inavyopotoshwa na Vyombo vya habari vyenye mielekeo tofauti.

Anonymous said...

Alimwita askofu muongo leo ameaibika yeye alishauriwa vyema sana juu ya ubabe na lugha za kejeli imedhihirika juzi kuwa hakuna prof muongo kama Prof Muhongo maana alipoambiwa ukweli na viongozi wa dini aliwaita waongo duuuh!!!!!!!