ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 13, 2013

Sababu za watoto kushindwa kusoma, kuandika na kuhesabu shuleni

Mazingira duni ya kujifunzia kama ilivyo katika darasa hili la shule moja ya msingi katika Kijiji cha Lula Kawala, mkoani Rukwa, yanatajwa kuwa chanzo cha wanafunzi kushindwa kujifunza ipasavyo stadi za kusoma, kuhesabu na kuandika. Picha ya Maktaba

Nje ya darasa la pili katika Shule ya Msingi Ilala iliyopo Manispaa ya Iringa, baadhi ya wanafunzi wanamsimanga mwenzao mmoja kwa kumwita mtoro.

Mmoja anapaza sauti na kusema: “Sharafi hajui kusoma’’ Ni kweli Sharafi (jina siyo lake) anayesoma darasa la pili shuleni hapo, anaelezwa na mwalimu wake kuwa hajui kusoma na pia ni mtoro aliyekubuhu, japo mwenyewe anakana kuwa siku hizi siyo mtoro tena.Mwalimu wake Esther Sanga, anasema baadhi ya wanafunzi darasani mwake wana matatizo ya kutokujua kusoma licha ya kuwa hivi karibuni watamaliza darasa la pili, akiwamo Sharafi anayesema anaweza kukaa hata mwezi mmoja hajaonekana shuleni.

Tukiwa darasani namwomba mwalimu huyo tumjaribu Sharafi kujua uwezo wake wa kusoma. Tunamwandikia ubaoni neno ‘baba’, kwa sekunde zisizozidi 10 analisoma na kulipatia. Kisha tunamwandikia neno ‘iba’, akachukua sekunde zaidi kulisoma na kulipatia.

Neno lingine lilikuwa ‘bobu’. Hapa Sharafi anatafakari zaidi huku akilikazia macho neno hilo. Baada ya sekunde nyingi kupita anafanikiwa kulisoma kwa usahihi japo anaonyesha kutokujiamini na alichokisoma.

Darasa analosoma lina watoto karibu 40 ambao licha ya kubakiwa na muda mchache kujiunga na darasa la tatu, bado hawajaweza kusoma kwa ufasaha hasa herufi mwambatano,

Mwalimu Sanga anasema wanafunzi hao wanasoma, lakini kwa kile anachokiita usomaji wa kudonoadonoa. Anasema: ‘’ Hawa wanasoma kwa kudonoadonoa, hawasomi kwa mfululizo na sababu ni kwamba wako wengi darasani na walikosa walimu wenye ujuzi.’’

Bila shaka wanafunzi hawa ni ushahidi wa kuwapo wanafunzi wengi wanaovuka darasa la pili wakiwa hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu, maarufu kwa kifupi cha KKK au K3

Ilivyo mfumo wa elimu wa Tanzania, unamtarajia mtoto akimaliza darasa la pili awe ana uelewa mkubwa wa stadi hizo -muhimu katika mchakato wa ujifunzaji.

Kisa cha Shule ya Msingi Ilala kinashadadiwa na matokeo ya utafiti uliofanywa mwaka 2010 na Uwezo Tanzania, na kubaini mwanafunzi mmoja kati ya watano wanaohitimu elimu ya msingi, hajui kusoma japo hadithi ya kiwango cha darasa la pili.


Utafiti huo ulioitwa ‘ Je watoto wetu wanajifunza? Ulihusisha sampuli ya watoto 42,033 kutoka kaya 22,800 katika wilaya mbalimbali nchini. Watoto hao walipimwa uwezo wa kusoma na kuhesabu.

Sababu za kutojua kusomaWalimu katika Shule ya Msingi Ilala wanasema sababu kuu inayochangia wanafunzi kufika darasa la pili bila kujua kusoma ni kubadilishwa kwa utaratibu wa ufundishaji wa masomo katika madarasa ya chini.

Wanasema zamani msisitizo ulikuwa kuwafundisha watoto hao stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu pekee. Lakini sasa wanafunzi hao wamebebeshwa mzigo wa masomo yapatayo sita.

Wanataja masomo hayo kuwa ni pamoja na Hisabati, Lugha ya Kiswahili, Lugha ya Kiingereza, Sayansi, Stadi za kazi na Haiba na Michezo. Kinachosikitisha ni kuwa wakati orodha ya masomo ikiongezeka, ufundishaji wa K3 umekosa msisitizo katika shule nyingi.

“Zamani tulijua kusoma, leo kuna masomo mengi, zamani ilikuwa ni kusoma, kuandika na kuhesabu. Nashauri darasa la kwanza na la pili wafundishwe K3 kisha masomo mengine yaendelee madarasa ya juu,’’ anasema mwalimu Tumaini Mungule.

Sababu nyingine ni wingi wa wanafunzi darasani. Wanasema hata kama K3 pekee zitafundishwa tena na walimu mahiri, haitosaidia kama madarasa yataendelea kuwa na mrundikano wa wanafunzi kama ilivyo sasa katika shule nyingi za umma.

“ Kwa shule za mjini idadi ya wanafunzi ni 100, 90 au 80 wakiwa na mwalimu mmoja. Kuwamudu wote haiwezekani, baadhi kama 10 au 15 utawaacha nyuma,’’ anaeleza mwalimu Imelda Ibobo anayefundisha darasa la pili katika Shule ya Msingi Mapinduzi mkoani Iringa.

Anaungwa mkono na Mratibu wa Tathmini ya Uwezo Tanzania kwa Wilaya ya Iringa Mjini, Ellen Binagi anayesema mbali ya wanafunzi hao kuwa wengi, bado mazingira ya madarasa mengi ni duni katika utoaji wa taaluma.

“Sasa hivi wanasukumwa tu bora liende. Darasani watoto wako kama utitiri na wamekaa chini, mwaka huu kuna swali linauliza asilimia ngapi ya wanafunzi wanakaa chini,’’ anaeleza.

Uwezo inayosimamiwa na asasi isiyo ya kiserikali ya Twaweza, kwa miaka kadhaa sasa imekuwa ikiendesha tafiti zinazolenga kupima uwezo wa kusoma na kuhesabu kwa wanafunzi wa umri wa miaka saba hadi 16.

Utoro nao unachangia
Ni dhahiri mtoto asiyehudhuria masomo tangu akiwa madarasa ya chini, ana uwezekano mkubwa wa kutojua kusoma asiposimamiwa barabara. Tafiti na uzoefu vinaonyesha utoro ni moja ya sababu kuu zinazochangia watoto kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu.

Kwa Shule ya Msingi Ilala mfano mzuri wa hoja ya utoro ni mwanafunzi Sharafi anayeelezwa kutoroka hata kwa muda wa mwezi mzima. Uwezo mdogo darasani unaosababishwa na utoro umemfanya aendelee kubaki darasa la pili badala ya darasa la tatu.

Hata hivyo, mwenyewe anasema sababu za kuwa mtoro hasa siku za nyuma ni kuchoshwa na adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shuleni na kurudi. Zamani alikuwa anaishi eneo la Ikonongo ambalo ni zaidi ya kilomita tatu kutoka shuleni.

“Zamani nilikuwa naishi mbali, nilikuwa nakuja siku moja nyingine siji. Wazazi waliponiuliza kama nakuja shule nilisema nakuja,’’ anasema Sharafi ambaye tofauti na maelezo ya mwalimu wake, anadai amebadilika na kuwa mtoto mwema.

Ukiondoa utoro walimu, wazazi na wadau wengine wa elimu wanasema mambo mengine yanayochangia tatizo hili ni ukosefu wa walimu hasa kwa shule zilizopo vijijini na baadhi ya wanafunzi kuwa na matatizo binafsi kama uwezo mdogo wa akili unaosababishwa na magonjwa na mambo mengine.

Wazazi wanasemaje?
Mzazi na mkazi wa Mtaa wa Dabodabo katika Manispaa ya Iringa, Hashim Mori anasema kwa shule za mjini zenye walimu, hali hiyo inaweza kusababishwa na wanafunzi wenyewe kwa kuwa watoro au walimu kutowajibika.

“Walimu hawawajibiki ipasavyo, kwa sababu wizara na ofisa elimu hawawafuatilii, ‘’anasema na kuongeza kuwa kudorora kwa elimu katika shule za umma kunasababishwa pia na viongozi kukosa uchungu kwa kuwa hawana watoto wanasoma katika shule hizo.

Kwa upande wake, mzazi Asha Rajabu anasema walimu wasitupiwe mzigo wa lawama, bali wa kulaumiwa ni wazazi anaosema hawawajibiki ipasavyo kwa watoto wao.

“Mzazi hamfuatilii mwanawe akirudi shule na wala hashirikiani na walimu. Walimu wana mbinu nyingi. Siku za nyuma mwanangu hakuwa anaandika nilipomkagua, nikapiga simu kwa mwalimu na kugundua hakuwa anahudhuria shule, tukaweka mkakati wa kumdhibiti,’’anasema .

Hali mbaya
Ni dhahiri kuwa hali syo nzuri katika shule nyingi nchini, ukitoa ripoti ya Uwezo Serikali imeshakiri kuwepo kwa idadi kubwa ya wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika katika shule za msingi. Cha ajabu wapo wanaofikia hatua ya kumaliza shule na hata kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza.

Kwa mfano, April mwaka jana, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilitangaza kuwabaini wanafunzi 5,200 waliokuwa kidato cha kwanza katika shule mbalimbali nchi nzima lakini hawakujua kusoma wala kuandika.

““Hili ndilo janga la kitaifa sasa. Lazima tujiulize kwa nini watoto wanamaliza darasa la saba wakiwa hawajui kusoma wala kuandika na halafu wanafaulu? ‘’ alisema Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo kama alivyonukuliwa na Mwananchi siku za nyuma.

Tatizo la dunia
Hali ikiwa mbaya kwa shule za Tanzania , huku kiwango cha watu wazima wasiojua kusoma na kuandika nacho kikiongezeka nchini kwa asilimia nane kuanzia mwaka 1990. Ripoti ya kimataifa ya hivi karibuni inasema dunia ina watu 774 milioni wasiojua kusoma na kuandika.

Aidha, ripoti hiyo iliyotolewa Septemba mwaka huu na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), inasema mbumbumbu wengi wapo katika nchi za mabara ya Afrika na Asia.

Kwa Tanzania takwimu zinaonyesha kuwa kumbukumbu zinaonyesha hadi mwishoni mwa mwaka 2002, watu wasiojua kusoma walikuwa milioni sita na laki mbili.

Mwananchi

No comments: