ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 1, 2013

Tanzania, Malawi zabadilishana taarifa

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ally
Wakati usuluhishi wa mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi ukiendelea, nchi hizo zimebadilishana taarifa kuhusu mgogoro huo.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ally, alipokuwa akizungumza na NIPASHE kuhusiana na maendeleo ya usuluhishi wa mgogoro huo.

“Taarifa zimeshakuwa tayari, za Malawi tumekabidhiwa sisi (Tanzania) na za kwetu wamekabidhiwa Malawi, ili kila upande uweze kupitia na kujua hoja za mwenzake,” alifafanua Ally.


Kuhusu kutembelewa na wasuluhishi wa mgogoro huo, Aalisema tayari wameshaenda Malawi, lakini kwa upande wa Tanzania bado, na kwamba mbali ya kutoa taarifa ya kuwasili nchini, siku kamili itawekwa bayana na wao wenyewe.

“Tunawasubiri wao kuja kwetu. Wao kama wasuluhishi watakapokuja wanazo hoja watakazotaka kujua au kupata ufafanuzi kutoka kwetu,” alisema.

Wasuluhishi wa mgogoro huo ni marais wastaafu Joachim Chisano (Msumbiji), Thabo Mbeki (Afrika Kusini) na Jose Eduardo dos Santos wa Angola.

Kiasi cha Dola za Marekani milioni 1.4 zilitakiwa kutolewa na serikali zote mbili kwa ajili ya kuchangia mchakato huo wa usuluhishi, huku kila upande ukitakiwa kutoa nusu ya kiasi hicho. Tanzania imeshatoa Dola 350 na Malawi Dola 50.

Julai mwaka jana, Rais Joyce Banda wa Malawi aliibua mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa kwa madai kwamba ziwa hilo linamilikiwa na nchi yake huku Tanzania ikisema kila nchi inamiliki asilimia 50.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: