Advertisements

Sunday, November 3, 2013

Wanafunzi zaidi ya 100 wadaiwa kufungiwa kwenye chumba

Wanafunzi zaidi ya 100 wa Shule ya Msingi ya kutwa ya St. John Bosco, Kibaha mkoa wa Pwani, wanadaiwa kufungiwa kwenye chumba kimoja cha shule hiyo kwa muda wa saa tano kama adhabu ya kutolipa ada.

Tukio hilo limetokea juzi ambapo wanafunzi hao wanadai kufungiwa katika chumba hicho na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana.

Wanafunzi hao wanadaiwa ada kati ya Sh. 50,000 hadi Sh. 400,000. Ada ya mwaka katika shule hiyo kwa mwanafunzi mmoja ni Sh. 1,300,000.

Wazazi wa wanafunzi hao wakizungumza na NIPASHE jana mjini Kibaha, walisema walipewa taarifa na watoto wao kwamba walifungiwa ndani ya chumba kwa sababu hawajalipa ada ya shule, jambo ambalo limewasikitisha sana na kinyume na haki za binadamu.

“Ukatili waliofanyiwa watoto wetu katika shule hii haujatufurahisha kabisa, kwani shule hii ni ya kidini sasa inakuaje Mwalimu Mkuu anakosa roho ya subira,” walisema wazazi hao ambao walikuwa wamejikusanya kutafakari kwa kina jambo hilo.

Walisema baada ya kupata taarifa kwa barua kutoka kwa uongozi wa shule kwamba wanatakiwa kuwalipia ada watoto wao, waliomba wawasilishe ada hiyo wiki ijayo lakini wameshangazwa na kitendo cha uongozi cha kukosa subira na kuamua kuwafanyia kitendo cha ukatili watoto wao.

“Ada yenyewe tunayodaiwa tulipe imetokana na ongezeko la ada kutoka Sh. 850,000 tuliyokuwa tukilipa awali na kufikia Sh. 1,300,000 kwa mwaka ambayo imepandishwa ghafla, kwanza watoto wenyewe wanapewa chai ya rangi na mikate tu saa 4:00 asubuhi,” walisema wazazi hao waliokuwa na jazba.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Sista Fabiola alipoulizwa kuhusu madai hayo alisema si ya kweli kwa sababu shule haina chumba cha kuweza kuwafungia wanafunzi hao kama inavyodaiwa na wazazi.

Alisema wapo watoto ambao wanadaiwa ada toka Januari hawajalipa na wazazi wao wamekuwa wakipewa barua mara kwa mara kila shule inapofungwa na kufunguliwa, lakini baadhi yao wamekuwa wakorofi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: