Na Nicodemus Jonas
BAADHI ya wachezaji na viongozi wa zamani wa Yanga wamekosoa uamuzi wa klabu hiyo kusitisha ajira ya Kocha Ernie Brandts na kusema kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha kuyumba hasa kipindi hiki ambacho inaelekea kwenye michuano ya kimataifa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Championi Ijumaa wachezaji hao wakiwemo Shaban Katwila aliyewahi kuwa kiongozi klabuni hapo, Seleman Mkati ambaye kwa sasa ni Kocha wa National FC na Charles Kilinda aliyewahi kuwa kocha wa JKT Ruvu, wote walipinga uamuzi huo.
Katwila amesema: “Sikupenda hilo lililotokea, Brandts ana rekodi nzuri tangu atue Yanga. Naamini maamuzi hayo yametokana na mechi ya Jumamosi (dhidi ya Simba) lakini wamesahau Yanga ya sasa imejaa wachezaji wapya tena mastaa, hivyo alitakiwa kupewa muda wa kuijenga timu upya.”
Kilinda alisema: “Timu inakabiliwa na michuano ya kimataifa, hivi unafikiri huyo kocha atakayekuja ataweza kuleta mafanikio kama wanayotaka wao?”
Naye Mkati akasema: “Wamekosea kufanya mabadiliko. Yanga sijaona ikifanya vibaya kiasi cha kumtimua mwalimu hasa katika kipindi hiki kuelekea michuano ya kimataifa.”
No comments:
Post a Comment