
Machakos. Kikosi cha Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kinashuka kwenye Uwanja wa Kenyatta mjini Machakos leo kwa lengo moja tu la kusaka ushindi dhidi ya wenyeji Kenya katika nusu fainali ya kwanza ya Kombe la Chalenji.
Kilimanjaro Stars itacheza saa 7.30 mchana kwenye uwanja huo ambao katika mchezo wa kwanza ilicheza hapo na kutoka sare ya bao 1-1 na Zambia ambayo itacheza na Sudan nusu fainali ya pili mjini Mombasa.
Katika uwanja ambao Kili Stars itachezea dhidi ya Harambee Stars una huduma za kifahari vyumbani kama runinga za kisasa zilizounganishwa na digitali, vinywaji laini vya kila aina, chai na maji ya moto ya kuoga jambo ambalo linaufanya uwe tofauti na viwanja vingine vya Afrika Mashariki na Kati ingawa bado nyasi haziridhishi haswa inaponyesha mvua.
Kocha wa Kili Stars, Kim Poulsen amesisitiza kwamba katika mchezo huo watashambulia kama walivyofanya dhidi ya Uganda mjini Mombasa.
Kim alisema; “Ni mchezo mgumu ulioko mbele yetu, lakini naamini kwamba tupo tayari kushinda katika mazingira yoyote yale, nina kikosi imara ambacho kimeimarika kimchezo, tuna imani tutavuka.”
“Hakutakuwa na mabadiliko makubwa sana kikosini kwa vile tuna wachezaji wengi ambao wapo tayari kwa mchezo, lengo sasa ni kucheza fainali na ninaamini huo uwezo upo tuna washambuliaji wazuri, mabeki na viungo.
“Tutacheza mchezo kwa staili tofauti zaidi, tunajua Kenya itakuwa na faida ya uenyeji kuanzia mashabiki na kila kitu, lakini haitatusumbua, tutafanya kazi yetu uwanjani,”alisisitiza Poulsen.
Pigo pekee kwa Kim leo ni kumkosa kiungo wake Salum Abubakari ‘Sure Boy’ anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata katika robo fainali dhidi ya Uganda.
Habari za ndani zinadai kwamba Kenya ilifanya mpango wa kuhamisha mchezo huo kutoka kwenye Uuwanja wa Mombasa na kuipelekaushusha Machakos kutokana na hali ya hewa.
Mombasa ni joto hali ambayo Tanzania wameizoea, lakini Kenya inawapa taabu kutokana na wachezaji wake kuzoea baridi ya Nairobi.
Kocha Adel Amrouche alisema; “Tanzania ni ngumu ina washambuliaji wazuri, tunajua inaingia ikiwa na morali ya kumtoa bingwa mtetezi, lakini sisi tutacheza soka yetu na ninaamini Kenya kiufundi iko sawa tayari kwa fainali.”
Kenya itakuwa ikiwategemea washambuliaji wake Allan Wanga na Jacob Kelli huku Kili Stars ikiwa na ukuta imara wa Kelvin Yondani na Said Morad na kipa Ivo Mapunda.
Kiungo cha Stars huenda akasimama Athuman Iddi na Frank Domayo ambao watakuwa wakitengeneza mipira kwa wachezaji wa pembeni Amri Kiemba na Mrisho Ngassa.
Stars imeonyesha mabadiliko makubwa kiuchezaji haswa baada ya uwaepo wa washambuliaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu ambao wameonyesha kujiamini na wanacheza soka ya kiwango cha juu.
Stars wakongwe waifuata Harambee Stars
Timu ya wachezaji wa zamani wa Tanzania, ‘Tanzania All Stars’ wanaondoka leo kwenda Nairobi, Kenya kucheza mechi maalumu ya kirafiki dhidi ya wachezaji wa zamani wa Kenya ‘Wazee wa Kazi’, mechi iliyopangwa kufanyika kwenye Uuwanja wa Nyayo siku ya fainali ya michuano ya Chalenji.
Wachezaji hao walioondoka chini ya nyota wa zamani, Kitwana” Popat” Manara ambao walikuwa wakijifua kwenye Uuwanja wa Leaders Club kujiandaa na mechi hiyo.
Mbali ya Kitwana, wachezaji wengine ni Khalid Abeid, Omari Gumbo, David Mwakalebela, Lawrence Mwalusako, Mohamed “Mmachinga” Hussein, Thomas “Uncle Tom” Kipese na Idd Seleman.
Wengine ni Mahmoud Uledi, Ken Mkapa, Shaaban Katwila, Maulid Kinapo, Abdallah Maulid, Ali Yusuph Tigana, Rashid Idd Chama, Habib Kondo, Abdallah Kaburu, Idd Seleman, Naftali Goha na Bita John. Kiongozi wa timu hiyo ni Hassan Mnyenye.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment