ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 18, 2013

Majambazi yawabaka mama, wanawe watatu

Watu wanaokadiriwa kufikia saba wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa na mapanga na marungu, wamevamia nyumbani kwa mkazi wa kijiji cha Kaduda kata ya Katoro wilayani Geita na kuwabaka kwa zamu mama na wanawe watatu kwa zaidi ya saa mbili.

Hali kadhalika, watu hao walimjeruhi mmoja wa watoto wake wa kiume aliyekuwa akishuhudia unyama huo ukifanyika.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Desemba 15, mwaka huu baada ya kuvamia na kuvunja mlango wa nyumba walimokuwa wamelala wakati baba mwenye mji huo akiwa safarini.

Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Jumanne Faida, alisema baada ya kutekeleza ukatili huo, mama na watoto hao walipiga yowe kuomba msaada.

Faida alisema kuwa watu hao walikuwa wakimbaka mama huyo na wanawe hao wenye umri wa kati ya miaka 14, 10 na 17 kwa kupokezana mbele ya mtoto wa kiume ambaye walimjeruhi kwenye paji la uso kumcharanga kwa panga.

Mganga wa zamu wa Kituo cha Afya cha Katoro, Dk. Daneil Izengo, alithibitisha kuwapokea mama na watoto wake hao kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi na wa kiume kwa matibabu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, hakupatikana kuzungumzia tukio hilo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Omary Mangochie, alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, alisema polisi walikuwa hawajamfahamisha rasmi.

Hata hivyo, Mangochie aliahidi kufuatilia ili waliohusika wasakwe na kukamatwa kisha kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.
 
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

mhh Tanzania tunaelekea wapi? huu unyama wa aina gani? tumekua kama sodoma na gomoro kama umekuja kuiba iba uondoke kwa nini unawadhalilisha wanawake kiasi hiki? walikukosea nini duniani mpaka ufikie kuwafanyia unyama wa aina hii? unabaka mama mbele ya familia yake na unawabaka watoto wake kweli duniani binadamu tunawezaje kumkosea mungu wetu kiasi hiki? mlaaniwe mliofanya unyama huu mlaaniwe nyinyi na vizazi vyenu