ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 2, 2013

Ni wiki ya majanga kwa Maghembe,Chiza,Malima

Watakiwa kutoswa bungeni kwa kuwa mzigo

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kitatumia fursa ya Mkutano wa 14 wa Bunge unaoanza kesho, kushinikiza mawaziri waliotuhumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushindwa kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia Watanzania, wawajibishwe na Rais Jakaya Kikwete, kwa kuwa ni ‘mizigo’ kwa serikali.

Aidha, wakati Mkutano huo wa Bunge ukisubiriwa, Chadema imeitaka CCM ianze kuwaelekeza wabunge wake wawe wa kwanza kuunga mkono hatua za kuwashughulikia mawaziri hao pindi wale wa Chadema watakapoanza kutoa hoja bungeni kuhusiana na suala hilo.

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alisema hayo wakati akizindua Rasimu ya Sera ya Chama hicho ya Mabadiliko ya Tabianchi, jijini Dar es Salaam jana na kusema kutokana na ukubwa wa ‘mizigo’ iliyopo ndani ya Baraza la Mawaziri la Rais Kikwete, alipaswa kulivunja.

Mawaziri hao, ambao Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, aliwatuhumu kushindwa kazi na kupendekeza wang’olewe ni pamoja na Dk. Shukuru Kawambwa (Elimu na Mafunzo ya Ufundi).

Wengine ni Christopher Chiza (Kilimo, Chakula na Ushirika); Adam Malima (Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika), Profesa Jumanne Maghembe (Maji) na Dk. William Mgimwa (Fedha).

Nape alipendekeza hilo katika Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma, mwezi uliopita na kusema anasikitishwa na kitendo cha mawaziri hao waliopewa dhamana, kushindwa kutambua wajibu wao.

Kutokana na hali hiyo, Nape alisema umefika wakati wa mawaziri hao kuhojiwa na Kamati Kuu (CC) ya CCM ili wachukuliwe hatua kwani bila kufanya hivyo aibu itarudi kwa chama chake.

Naye Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema katika kikao cha CC kitakachofanyika mwezi huu, kitamuandikia barua Rais Kikwete ili mawaziri wake waende mbele ya kikao na kueleza kwa nini wasifukuzwe kwa kushindwa kazi.

Jana Mnyika aliwaambia waandishi wa habari kuwa pamoja na uzinduzi uliofanyika na kusubiri maoni ya wanachama kuhusu rasimu hiyo, Chadema inaanza utekelezaji wa kuibana serikali kabla hawajaingia madarakani juu ya sera hiyo.

Alisema kwa sababu hiyo, chama tayari kimekwisha kuwasiliana na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ili mawaziri vivuli wa sekta zote zilizoko kwenye sera hiyo, wafanye kazi hiyo katika Mkutano wa Bunge unaoanza kesho.

Mnyika alisema katika sera hiyo, kuna wajibu wa Wizara ya Elimu kwenye kuhakikisha Watanzania wanaandaliwa kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi na kuyadhibiti.
Hata hivyo, alisema wanafunzi bado hawajaandaliwa hivyo kwa sababu ya ubovu wa mitaala na mfumo wa elimu uliopo.

Alisema zaidi ya hivyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliunda kamati kuchunguza tatizo la elimu nchini, lakini ripoti yake mpaka sasa imefanywa kuwa siri.
“Kwa hiyo, waziri wetu kivuli wa elimu atakwenda kumbana Waziri mzigo wa Elimu ndani ya Bunge,” alisema Mnyika.

Mnyika alisema Waziri Kivuli wa Elimu atambana waziri halisi wa wizara hiyo siyo kwenye mabadiliko ya tabianchi, bali atafanya hivyo kwa upana wake.

Alisema hiyo ni pamoja na kutaka ripoti ya kamati ya waziri mkuu iwekwe hadharani ili uboreshaji wa mitaala na huduma katika sekta ya elimu ufanyike na athari zake ziwe katika sekta zote.

“Na katika mambo yatakayoguswa katika jambo hili ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi kwa sababu ni suala mtambuka,” alisema Mnyika.
Alisema sera hiyo pia inagusa masuala ya wakulima na wafugaji na kwamba, Waziri Chiza amesemwa na chama chake cha CCM, ingawa Chadema walishawahi kufanya hivyo muda mrefu.

Mnyika alisema baya zaidi CCM imekuwa ikikwepa kumsema Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Mathayo David, kiasi ambacho nchi imekuwa ikikabiliwa na majanga ya wakulima na wafugaji na majanga mengine ya namna hiyo.

“Kwa hiyo waziri wetu kivuli wa kilimo na waziri wetu kivuli wa mifugo na wao kwa upande wao watatumia njia za kibunge kuibana serikali. Kwa sababu tatizo la mabadiliko ya tabianchi, athari kubwa zaidi zinawakabili wakulima wa nchi hii, wafugaji wa nchi hii, na wananchi kwa ujumla wake. Kwa hiyo, hili ni eneo lingine ambalo tutalisimamia tukienda bungeni,” alisema Mnyika.

Alisema chanzo kikuu cha mabadiliko ya tabianchi duniani kote ni ongezeko la hewa ya ukaa, ambalo vyanzo vyake vikubwa cha kwanza kikiwa ni matumizi ya nishati zenye kusababisha hewa ya ukaa, hasa mafuta ya petroli yanayotumika viwandani na kwenye magari.

Mnyika alisema asilimia 50 ya hewa ukaa duniani inachangiwa na vyombo vinavyotumia mafuta.

Alisema chanzo kikuu cha pili cha ongezeko la hewa ukaa, ni ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira katika maeneo ya misitu, ambayo ingenyonya hewa hiyo katika maeneo mbalimbali.

Hivyo, akasema ufumbuzi unahitaji, ikiwa ni pamoja na kuwa na mikakati ambayo ndani ya sera hiyo imeelezwa kwa kiasi kikubwa ya kuwa na nishati mbadala na isiyokuwa na madhara, iwe ni gesi au nishati jadidifu au nishati nyingine.

“Lakini wakati huo huo kuhakikisha kwamba tunawekeza katika kuhakikisha tunapunguza hewa ya ukaa. Hasa mimi ni waziri kivuli wa nishati na madini, chama kilipotoa maelekezo, kati ya watu ambao tumejulishwa na chama kwenda kusimamia hili jambo bungeni ni pamoja na mimi vilevile kwa nafasi yangu nyingine kama waziri kivuli wa nishati madini,” alisema Mnyika.

“Kwa hiyo, tutakwenda kuhakikisha tuibana serikali bungeni juu ya uongo unaosemwa kuhusiana na masuala ya sera ya gesi, sheria ya gesi, ufisadi kwenye gesi, ujenzi wa bomba la gesi na masuala yanayohusiana na mgawo wa umeme na miradi ya umeme kwa ujumla.Yote haya tutakwenda kuibana serikali bungeni.”

“Na tunawaambia wabunge wa CCM kama CCM kweli haikuwa inafanya unafiki, kama Kinana na Nape hawakuwa wanafanya unafiki, walipokuwa wanasema kuna mawaziri mizigo, waanze kabisa kuwaelekeza wabunge wao, Bunge linapoanza wabunge wa Chadema watakapoanza kuleta hoja au maelezo au maswali au masuala mengine, wabunge wao wawe wa kwanza kuunga mkono hatua za kuwashughulikia mawaziri mizigo.”

Mnyika alisema iwapo CCM itakwepa kuchukua hatua watajua kwamba ni kama ambavyo walishindwa kujivua magamba ya ufisadi pamoja na kupiga kelele muda mrefu kuhusu suala hilo.

Alisema pia sekretarieti mpya ya CCM iliwahi kusema ingewashughulikia wanachama wake waliotoa rushwa kwenye uchaguzi, lakini haikuwashughulikia.

Aliongeza: “Kama kuna mawaziri mizigo Bunge liwe ndiyo la kwanza kuwawajibisha au Rais aliyewateua awe wa kwanza kuwafukuza kazi mawaziri wote mizigo. Na ukubwa wa mizigo iliyoko ndani ya Baraza la Mawaziri la Rais Kikwete, ni wazi Rais alipasa alivunje Baraza hili la Mawaziri.”

Alisema kitendo cha CCM kukimbilia kulipeleka suala la mawaziri hao kwenye vikao vya CC yake, siyo sahihi kwa sababu vikao hivyo ni vya siri, hivyo wanataka kwenda kuficha udhaifu ulioko ndani ya serikali.

“Kama kweli wanajua udhaifu ulioko ndani ya serikali waruhusu wabunge jambo hili liende kuanzia bungeni,” alisema Mnyika.

Alisema chama kimetoa nafasi kwa wanachama na wananchi wote kwa jumla kutoa maoni kuhusu rasimu ya sera hiyo kuanzia ilipozinduliwa jana hadi mwishoni mwa mwezi huu.

Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Ziwa Magharibi, Dk. Rodrick Kabangila, jana katika uzinduzi wa sera hiyo, alitangaza kung’atuka kwa hiari yake nafasi zake za kuongoza madaktari na watumishi wengine wa afya.

Dk. Kabangila, ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya tiba, tafiti za huduma za afya na epidemiolojia, alikuwa ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (Mat) na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Katoliki cha Afya na Sayansi (Cuhas).

Alisema uamuzi wake huo umepata baraka ya Halmashauri ya Mat na kwamba, amefikia uamuzi huo pamoja na mambo mengine ili kuwakumbusha watumishi wote wenye taaluma mbalimbali kuwa kushiriki katika harakati za kisiasa ili kuiondoa CCM siyo kosa la jinai.
CHANZO: NIPASHE

No comments: