
Raia wa China aliyefahamika kwa jina la Wangi Jian(47), amefariki dunia baada ya kuzama kwenye bwawa la kuogelea katika hoteli ya Golden Tulip, jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, jana alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, majira ya saa 7:30 mchana na kutaja namba ya hati ya kusafiria ya raia huyo ni G25317143.
Alisema raia huyo alikuwa na wenzake katika hoteli hiyo wakisherehekea sikukuu ya Krismas.
“Baada ya kuzidiwa na maji wenzake walimchukua na kumkimbiza Hospitali ya Ami, iliyopo Kata ya Masaki na kuamishiwa Hospitali ya Aga Khan na badaye wakati anapelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili alifariki dunia,” alisema Wambura.
Wakati huo huo, katika tukio jingine mkazi wa Banana, Ally Sheki (18), amefariki wakati akiogelea katika ufukwe wa Coco Beach jijini humo.
Alisema kijana huyo alikutwa na mauti majira ya saa 9:00 alasiri, baada ya kubebwa na wimbi zito la maji lililomchukua na kumzamisha akiwa anaogelea. Hata hivyo, aliokolewa na wasamaria wema lakini baada ya kuokolewa kutoka baharini alikuwa ameshafariki dunia.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Mwananyamala na upelelezi unaendelea.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment