![]() |
| Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye ofisi za CCM Lumumba mjini Dar es salaam |
- Nape : Majibu ya Sefue yana Ukakasi
- Kuteuliwa kwao kusiwe chanzo cha kukaa kimya
- Asema CCM haitosita kuwapongeza Mawaziri wanaofanya vizuri na kuwasema wanaofanya vibaya
Mara baada ya kuundwa kwa
Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa inayoongozwa na Katibu Mkuu Ndg.
Abdulrahman Kinana mwanzoni mwaka mwaka jana, Sekretarieti hiyo imejiwekea
utaratibu wa kufanya ziara mikoani kukutana na wananchi kusikiliza kero
zao,kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuimarisha Chama
mikoani. Utaratibu huu ni agizo la mkutano mkuu wa Taifa wa nane wa CCM
uliofanyika Novemba 2012 mjini Dodoma. Nanukuu azimio hilo;
“ Chama Cha Mapinduzi lazima kiwe
karibu na wananchi, kisikilize changamoto zao na kiwasemee wananchi na hasa
wanyonge” Moja ya maazimio ya Mkutano Mkuu wa nane wa CCM 2012.
Kwa hiyo msingi wa kwanza wa ziara
hizo ni maagizo ya Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ambacho ndicho kikao cha juu
kabisa cha Chama. Msingi wa pili ni ukweli kuwa CCM ndio iliyopewa dhamana na
kuingia mkataba na wananchi kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka
2010/2015, hivyo inayowajibu wa kukagua utekelezaji wa ilani hiyo.
Na bila shaka wote tumeshuhudia
jinsi ziara hizo zilivyoinua uhai wa Chama nchi nzima na kuongeza kasi ya
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na kutatua kero mbalimbali za wananchi kwenye
maeneo yao, kiasi cha kuongeza imani ya wananchi kwa CCM.
Tumeshuhudia makundi mbalimbali
ndani ya jamii yakija kueleza changamoto zao ndani ya Chama. Makundi hayo ni
pamoja na makundi ya wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, wanafunzi na
wafanyakazi hasa walimu. Huu ni uthibitisho wa kuongezeka kwa imani yao kwa
CCM.
Katika mwendelezo wa ziara hizo
mwishoni mwa mwaka jana Katibu Mkuu wa CCM na baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti
walifanya ziara ya siku 26 katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Njombe. Pamoja na
mambo mengine wananchi walilalamikia baadhi ya watendaji wa serikali hasa
baadhi ya mawaziri wakiamini kuwa yapo mapungufu kadhaa yanayotokea kwenye
wizara zao.
CCM kama lilivyo agizo la Mkutano
mkuu la kuwasemea wananchi tulisikiliza kilio chao na kwa kufuata utaratibu,
baadhi ya mawaziri hao waliitwa na kuhojiwa kwenye Kamati Kuu ya CCM mwezi
Disemba 2013.
Utaratibu wa watendaji wa
serikali kutoa taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwenye vikao
vya Chama sio mgeni na wala haujaanza jana. Wakuu wa wilaya hutoa kwenye
wilaya, wakuu wa mikoa hutoa mikoani kwao,hivyo sio utaratibu mpya.
Baada ya mahojiano hayo Kamati Kuu
ya CCM ilitoa ushauri kwa serikali wa namna ya kurekebisha mapungufu
yaliyoelezwa na wananchi. Kwakuwa kwa mujibu wa Katiba ya Nchi mwenye mamlaka
na mawaziri ni Rais mwenyewe, CCM ililiacha suala hili kwake aangalie njia ipi
bora ya kuondoa mapungufu tuliyoyaeleza.
Na kwenye taarifa yetu kwa vyombo
vya habari baada ya kikao hicho tulisisitiza kuwa sio lazima awafukuze mawaziri
husika isipokuwa wanaweza kufanya mabadiliko katika mfumo,sheria nk ili mradi
kuwepo na mabadiliko katika kushughulikia mambo yaliyolalamikiwa na wananchi.
Hivi karibuni Rais amefanya
mabadiliko kidogo kwenye baraza lake la mawaziri na kuwarudisha baadhi ya
mawaziri waliolalamikiwa na wananchi na wabunge, ambao malalamiko hayo
yaliungwa mkono na CCM. Ni kupitia malalamiko hayo ndipo lilipozaliwa jina
la mawaziri mizigo. Baada ya uteuzi huo kukaibuka mjadala mkubwa nchini
wakihoji kulikoni Rais kaamua kutowatimua mawaziri hao.
Kwanza haikua hoja ya CCM kuwafukuza
mawaziri hao bali kuchukua hatua za kurekebisha mapungufu husika. Kufukuza
inaweza kuwa ni njia ya kutatua tatizo lakini sio njia pekee. Hivyo basi CCM
tunaamini kuwa kurudishwa kwao wamepewa fursa ya kurekebisha mapungufu
tuliyoyasema kwa niaba ya wananchi. Tunaamini mawaziri wote hawatabweteka bali
watatimiza wajibu wao na kuhakikisha wanawatumikia wananchi ambao ndio waajiri
wa serikali.
Ifahamike kuwa Chama Cha Mapinduzi
hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mawaziri na watendaji wengine
watakaoshindwa kurekebisha mapungufu na watakaoshindwa kutimiza wajibu wao
vizuri. Wakumbuke kushindwa kwao kutimiza majukumu yao ni hujuma kwa Ilani ya
uchaguzi ya CCM, CCM haitavumilia usaliti huo. Kukaa kimya kwa CCM itakua ni
kujinyonga yenyewe jambo ambalo hatutaruhusu kabisa.
Tunajua wapo baadhi ya watendaji wa
serikali wasiopenda kuhojiwa utendaji wao, tunawasihi kwa moyo safi wasiotaka
kuulizwa juu ya utendaji wao waondoke serikalini wenyewe kwani CCM tutakuwa
wakali sana kwenye mapungufu,kwani tukikaa kimya tutakua tunajihujumu wenyewe.
Tutatumia vizuri wingi wa wabunge
wetu bungeni na wingi wa madiwani wetu kwenye halmashauri kuisimamia vizuri
serikali. Hivyo kuanzia sasa kasi ya CCM kuisimamia serikali, kuisifu
itakapofanya vizuri na kukosoa itakapofanya vibaya itaongezeka mara dufu kwa
kila ngazi.
Tunawaomba watanzania kwa ujumla
tuwape muda wateule hawa wa Rais watimize wajibu wao, lakini tusisite kusema
pale tutakapoona mambo hayaendi kama tunavyotarajia. Uwajibikaji wa kweli ndio
msingi wa mafanikio na maendeleo yetu.
CCM inawatakia kila lakheri kwenye
kutimiza wajibu wao. Tuna matumaini makubwa kuwa wote kwa pamoja hawataisaliti
ilani ya Uchaguzi ya CCM na kwamba hawatayaangusha matumaini ya wananchi kwa
serikali yao.
Akijibu baadhi ya maswali kutoka kwa
waandishi wa habari hasa lile linalohusu majibu ya serikali juu ya mawaziri
mizigo Nape alisema “Majibu ya Katibu Mkuu Kiongozi Sefue yana ukakasi,kwani
changamoto zingine zilizotajwa hazina mashiko, mfano pesa si sababu ya kiongozi
kushindwa kufanya kazi, mbona baada ya kupiga kelele Ruvuma pesa zilienda je?
zilikuwa wapi ?alihoji Ndugu Nape”
Tunajua wapo baadhi ya watendaji wa
Serikali wasiopenda kuhojiwa juu ya utendaji wao Nape alisema “ukienda ukawa
mkulima wa nyanya,ukasukuma matoroli ,ukafanya kazi zako binafsi hautohojiwa na
wananchi,ukikubali kupewa dhamana
dhamana ambayo unalipwa kwa kodi za Watanzania basi ukubali kuhojiwa kama
mambo hayaendi sawasawa”.
Ningetamani Vijana wa Nchi hii
waibebe vita hii utaratibu wa watu
kupewa vyeo ni wakati wa kula ukome uwe wakati wa watu kufanya kazi,hivi
leo tukihesabu safari za waziri Fulani kwenda nje na safari za kwenda
kuwatembelea wananchi zipi nyingi? Tukisema maneno…hivi kwa nini leo madai ya
walimu hayakomi?
Nape alisisitiza asiyetaka kusemwa
aondoke aende kutafuta kazi nyingine.

No comments:
Post a Comment