ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 9, 2014

Chadema kumpinga Zitto Mahakama ya Rufani

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kiko katika harakati za kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, uliompa ushindi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zitto Kabwe.
Zitto ambaye pia ni Mbuinge wa Kigoma Kaskazini, juzi aliibuka mshindi katika maombi yake ya kuizuia Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kumjadili na au kuchukua uamuzi wowote kuhusu uanachama wake, hadi kesi ya msingi kuhusu suala hilo itakapokuwa imesikilizwa.
Kadhalika, chama hicho kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Mawasiliano na Uenezi, John Mnyika kimesema kinaendelea na utekelezaji wa uamuzi wa Kamati Kuu wa kutompa Zitto ushirikiano wa aina yoyote.
Wakili wa Chadema, Peter Kibatala, alisema jana kuwa japo wanauheshimu uamuzi wa Mahakama, hawajaridhika nao na kwamba wanakusudia kwenda Mahakama ya Rufani kuupinga.
“Ingawa uamuzi huu ni Interlocutory (uamuzi usiomaliza kesi), lakini sisi hatukuridhika nao. Hatukuridhika na uamuzi wa kutupilia pingamizi letu la awali, hati ya kiapo na hata amri yenyewe ya zuio la muda,” alisema Wakili Kibatala na kuongeza:
“Kuna namna nyingi za kufanya kupinga uamuzi huo, kama vile kukata rufaa, kuomba marejeo au namna nyinginezo. Kwa hiyo kwa sasa tunaangalia namna bora ya kwenda Mahakama ya Rufani bila kuathiri matakwa ya kisheria.”
Wakili Kibatala ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alisema kuna haja ya kuiomba Mahakama ya Rufani kuuchunguza uamuzi huo kwa kuwa una athari si kwa Chadema tu, bali hata vyama vingine dhidi ya wanachama wake.

Kauli ya Mnyika
Mnyika kwa upande wake alisema kutompa ushirikiano Zitto ni uamuzi wa Kamati Kuu ambao ulitokana na hatua yake ya kwenda mahakamani kwa masuala ya chama, kinyume cha matakwa ya Katiba ya Chadema na Kanuni zake.
Mnyika alikuwa akirejea taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, baada ya kikao hicho akiwataka viongozi wa ngazi zote za chama hicho, wanachama, mashabiki na wapenzi wake, kutoshiriki wala kusaidia kwa namna yoyote mikutano yote ya nje, ndani au shughuli nyingine yoyote ya kisiasa itakayofanywa na Zitto na mawakala wake.
Ushindi wa Zitto
Katika maombi hayo namba 1 ya 2014, Zitto kupitia kwa Wakili Albert Msando, Zitto aliiomba Mahakama itoe zuio hilo la muda kwa CC ya Chadema, hadi kesi yake ya msingi namba 1 ya 2014 aliyoifungua mahakamani hapo itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Awali, mawakili wa Chadema, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu na Kibatala walipinga maombi hayo wakidai kuwa hayajakidhi matakwa ya kupewa zuio la muda.
Katika uamuzi wake juzi, Jaji John Utamwa alikubaliana na hoja za Wakili Msando kuwa maombi hayo yametimiza matakwa yote ya kupewa zuio hilo.
Maombi hayo ya Zitto yaliyotolewa uamuzi juzi yalitokana na kesi ya msingi aliyofungua mahakamani hapo Januari 2, 2014, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa Chadema.
Katika kesi hiyo anaiomba mahakama ikizuie chama hicho, wakala wake na vyombo vyake vya uamuzi kumchukulia hatua zozote au kumjadili kuhusiana na uanachama wake, hadi hapo rufaa anayokusudia kuikata Baraza Kuu la chama hicho kupinga kuvuliwa nyadhifa, itakaposikilizwa.
Pia aliiomba Mahakama Kuu imwamuru Katibu Mkuu wa Chadema ampatie mwenendo na taarifa za CC za kumvua nyadhifa zake zote alizokuwa nazo ndani ya chama na iwazuie walalamikiwa kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu yake kama Mbunge wa Kigoma Kaskazini. Kesi hiyo ya msingi imepangwa kutajwa mahakamani hapo Februari 13, mwaka huu.
Mwananchi

2 comments:

Anonymous said...

Hawa mawakili wa CDM kweli waropokaji na wanakurupuka kutoa statements ambazo zinawaharibia wenyewe. wanavalidate madai ya ZZK kutokana na umbumbu wao wa hiyo elimu dunia ya sheria wanayojigamba wanayo. Dr Slaa vilevile mbumbumbu anatowaje maagizo wanachama wa CDM wasishiriki katika vikao na mikutano inayomhusu Zitto uku anajua madai ya Zitto ndio maamuzi yaliyotolewa na mahakama kama athari za yeye Zitto individually na wapiga kura wake. Sijui lakini hawa viongozi wa CDM wanafikiri mahakama za Tanzania ziko chini uendeshaji wa kina Swai kama vile wanavyofanya vikao vyao kamati kuu sebuleni kwa Mbowe, Dr Slaa, na Mtei.
Wao wakubali tuu ZZK haondoki CDM na dhamira yake ya kugombea uenyekiti iko palepale. Kwanini wanaogopa shauri lake hilo la uhaini waliompandikizia lisikilizwe na baraza kuu la CDM? Wanajua kuwa maamuzi ya umma wa CDM sio wa kikanda na hawatakuwa na kura za kutosha kumtoa CDM
Mbona Hillary Clinton alikubali yaishe kwa Obama, Thabo Mbeki alimpisha Mandela kuwa rais SA. Its Zitto time na ni bora hawa viongozi wa CDM wajue hivyo ili kukinusuru chama chao.

Anonymous said...

Acha ushabiki mbao ambao hauna maana. Tanzania kuna vyama vingi tu...kwanini asitangaze kukihama CDM nakujiunga na CCM?...watampokea tu....akapambane nao huko mbele kwa mbele. Ni vizuri CDM wakapoteza kiti cha kigoma kuliko kukaa na ndumila kuwili ndani ya chama. Mimi sina chama na wala sishakii chama chochote,lakini kwa mtizamo wangu,Zitto hafai kukaa ndani ya chama cha CDM kama kiongozi.