ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 23, 2014

Gari lagonga wanafunzi, laua wanne papo hapo

Wengine 21 wajeruhiwa vibaya
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen

Wanafunzi wanne wa Shule ya Sekondari ya Mustapha Sabodo iliyoko katika kijiji cha Msijute Halmashauri ya Mtwara Vijijini, mkoani Mtwara wamekufa papo hapo baada ya kugongwa na gari wakati wakikimbia mchakamchaka jana alfajiri.

Wanafunzi hao walikufa baada ya kugongwa na gari aina ya Mercedes-benz namba T174 AED jirani na eneo la shule.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen, alisema jana kuwa ajali hiyo ilitokea alfajiri saa 11:40 katika maeneo ya shule hiyo barabara kuu ya Dar es Salaam-Lindi na kwamba gari hilo lililokuwa katika mwendo wa kasi, lilikuwa linaendeshwa na Baraka Mgengwe (50) wakati likitokea Mtwara kwenda Lindi.

Kamanda Stephen hakutoa maelezo zaidi kuhusiana na mazingira ya ajali hiyo, mbali ya kusema kuwa wanafunzi hao walipatwa na mkasa huo wakati wakigeuka kurejea shuleni.
Alisema kuwa wanafunzi 21 walijeruhiwa huku wengine 26 waliopata mshtuko, walitibiwa kisha kuruhusiwa.

Alisema dereva wa gari hilo anashikiliwa na Polisi kwa ajili ya mahojiano.
Kamanda Stephen aliwataja wanafunzi waliokufa kuwa ni Khairath Mohammed, Mwanahamis Mohammed, Hasma Mpunja na Hilda Mathias.

Maiti zimehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara, Ligula.
Alisema polisi walipata taarifa muda mfupi baada ya ajali hiyo na kufika eneo la tukio na kushiriki kuwapeleka majeruhi hospitali.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Vijijini, Wilman Ndile, alisema uongozi wa wilaya yake umeunda kamati inayoongozwa na mganga wa wilaya na ofisa elimu kushughulikia mipango ya kusafirisha miili kwenda katika maeneo yao kwa ajili ya mazishi.
Mganga Mkuu wa Hospitali Rufaa ya Ligula, Dk. Shaibu Maarifa, alithibitisha kupokea majeruhi na maiti.

Dk. Maarifa alisema madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo walijipanga kuhakikisha wanaokoa maisha ya majeruhi na kwamba wanaendelea vizuri, isipokuwa mwanafunzi mmoja wa kike hali yake siyo nzuri.
CHANZO: NIPASHE

No comments: