
Lazima kichwa kifanye kazi sawasawa, ufikirishe akili yako vyema ili ujihakikishie maelewano ya kudumu katika uhusiano wako. Rafiki zangu, wapenzi kuishi mbalimbali bado ni tatizo kwa baadhi ya watu.
Hapa kwenye Let’s Talk About Love najaribu kuweka mbinu bora zaidi ambazo kwa namna moja ama nyingine zitasaidia kuwaweka karibu kihisia na hivyo kuziba mwanya wa usaliti. Wiki iliyopita niliishia katika kipengele cha kumwamini mpenzi wako.
Uaminifu ni jambo zuri lakini ni vizuri zaidi kuonyesha kuwa unamwamini mwenzako katika kiwango cha mwisho. Mfano, ukimtumia meseji au kumpigia halafu asipokee au asijibu kwa wakati, usikasirike.
Usimwandikie meseji ya kumlaumu badada yake unaweza kuandika mfano wa meseji kama ifuatayo;
“Najua ni majukumu mengi uliyonayo muda huu ndiyo yanayosababisha ushindwe kupokea simu yangu, usijali kwa hilo. Nakupenda sana na natambua kuwa mimi ndiye mwenye jukumu la kuhakikisha nakuwa karibu na wewe kwa kila kitu, nakupenda mpenzi wangu, kazi njema.”
Ujumbe huo utamfurahisha, kama alikuwa na nia ya kukusaliti, hawezi kufanya hivyo kwani atakuwa anajua kwamba anamsaliti mwenzi ambaye anamwamini katika kiwango cha mwisho. Kumwamini kwako kutamfanya aone ni jinsi gani ambavyo wewe mwenyewe unajiamini na usivyo na wazo la kumsaliti! Kwa nini yeye akufanyie hivyo? Lazima atabadilisha wazo lake.
Usimwandikie hivi: “Najua upo na wanawake zako huko... ama kweli fimbo ya mbali haiui nyoka, endelea kunisaliti tu.” Meseji ya aina hii haifai kabisa kwani utamfanya azidi kukusaliti na kama alikuwa hana wazo hilo, anaweza kujikuta anafanya hivyo.
Kubwa zaidi ni kwamba atafikiria kuwa, ikiwa wewe unamuwazia hivyo, basi kuna uwezekano mkubwa kwamba hata wewe unamsaliti huko ulipo.
Hapo sasa bila shaka wazo la kutafuta mwenzi mwingine linaweza kumwingia. Kwa nini uruhusu hali hiyo?
FANYA SAFARI YA MSHTUKIZO
Kufanya safari ya mshtukizo (surprise) ni kati ya mambo ambayo yatamfanya mwenzi wako afurahi. Lakini lazima uwe makini kabla ya kufanya jambo hilo. Ni vyema kuwa na hakika kwamba mna kipindi kirefu hamjakutana na kila mmoja (hasa yeye) ana shauku na mwenzake.
Nenda bila kumtaarifu, fikia hotelini, kisha mpigie simu ukijifanya upo sehemu ambayo alikuacha (unapoishi). Baada ya hapo, ukishahakikisha umeteka hisia zake vyema, sasa unaweza kumweleza ukweli kwamba upo katika makazi yake mapya.
Hakika itakuwa furaha kubwa, ingawa pia inawezekana ikawa huzuni, hasa kama alikuwa anakusaliti.
Kama ikiwa hivyo, si haba kwani angalau utakuwa umefahamu ukweli kwamba mwenzi wako hakuwa wako, kwani ni msaliti na aliyekuwa anakupotezea muda wako.
Baada ya kugundua kuwa ni msaliti, bado utakuwa na hamu ya kuendelea naye? Hapana kabisa... kaa pembeni. Wako yuko njiani. Naamini mada hii imekubadilisha na sasa utakuwa mpya.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.
GPL
No comments:
Post a Comment