
HAPA kwenye Love & Life ni mahali sahihi kabisa pa kupanuana mawazo kuhusu maisha na mapenzi. Ukiwa mdau wa ukurasa huu utaendelea kuimarisha uhusiano wako siku hadi siku.
Napokea pongezi zenu wasomaji, mlizonitumia baada ya makala ya utangulizi wiki iliyopita. Ilikuwa ni mara ya kwanza kuandikia safu hii nikitokea Magazeti ya Risasi Mchanganyiko na Ijumaa.
Naahidi kuboresha zaidi ili mpate kitu kizuri zaidi na uhusiano uwe wenye afya na amani. Marafiki zangu, wiki iliyopita nilianza kwa kueleza tofauti iliyopo kati ya urafiki au uchumba na ndoa.
Mapenzi yale ya urafiki ni tofauti kabisa na kuwa ndani ya ndoa. Kwenye uchumba kuna mambo ya kufurahisha zaidi, lengo kuu huwa kupeana raha na starehe za hapa na pale.
Marafiki, mnapoingia kwenye ndoa, mapenzi yapo tena yanakuwa na nguvu zaidi lakini kuna vitu kidogo vinabadilika. Hata kama ukiona mwenzako kuna vitu hakufanyii, usikasirike, angalia yale ya msingi zaidi kama anakupatia.
Si rahisi akakupa kila kitu, ridhika naye kwa kuwa moyoni umewekeza upendo wako. Vipengele vifuatavyo, vinafafanua zaidi.
HAKUNA RUFAA
Kwanza kabisa unatakiwa kufahamu kwamba, hakuna rufaa katika ndoa. Ukishaingia umeingia. Ni vizuri kuwa mtulivu na kuangalia zaidi mambo ya msingi.
Achana na fikra mbaya kwa mwenzako, wekeza upendo wako kwake. Mwamini na ishi naye kwa akili huku ukijaribu kumshauri mambo mbalimbali ya maisha yenu.
FURAHA YA NDOA
Yapo mambo mengi ya muhimu kwenye ndoa, lakini jambo kubwa na la msingi zaidi ni pamoja na tendo la ndoa. Lazima wanandoa wawe na uhakika wa kupata tendo la ndoa.
Tendo lenyewe linatakiwa kufanyika vizuri na kwa usahihi. Siyo harakaharaka bila ubunifu. Kufanya hivyo ni kuacha mianya ya mmoja wenu kufikiria kutoka nje ya ndoa.
FAMILIA
Majukumu ya familia ni kati ya mambo yanayozidisha furaha ya ndoa. Kama wanandoa wanakuwa makini kuhakikisha familia inakuwa yenye furaha ni jambo zuri.
Lazima watoto wapatiwe elimu bora, uhakika wa lishe, malazi na mambo mengine kama hayo bila kusahau malezi mazuri ya kiimani.
MIPANGO YA BAADAYE
Maisha ni mipango, hamuwezi kufikiria sterehe tena kama ilivyokuwa kwenye uchumba. Kwenye muunganiko wa ndoa kuna suala la maendeleo na mipango ya baadaye.
Hapo mnatakiwa kuwaweka watoto wenu mbele, maana lazima wawe na akiba yao ambayo mtawaachia. Lazima mfikirie kuhusu rasilimali kwa ajili yao.
KUJALIANA
Kila mmoja anaweza kukutana na changamoto kwa wakati wake. Kuna suala la matatizo kazini au msongo wa mawazo. Majukumu ya familia ya upande mmoja au ndugu wa mwenzako.
Mambo kama hayo mkishirikiana kuyatatua huongeza mapenzi ya dhati. Kwa mfano, mmoja wenu anaweza kuugua. Ni jambo zuri sasa kuwa karibu naye na kumpa furaha ili ajione yupo na chaguo lililo kamili.
Maisha ni zaidi ya starehe za kawaida. Majukumu ya familia ni muhimu zaidi kuliko yale mahaba ya mwanzo. Huu ni ukweli ambao wanandoa wengi (hasa wanawake) wanaukimbia. Wiki ijayo nitakuwa hapa na mada nyingine, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitatu vitatu; True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.
No comments:
Post a Comment